Tafuta

Vatican News
Ushemasi ni Daraja ya Huduma: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma: kiroho na Kimwili Ushemasi ni Daraja ya Huduma: Neno la Mungu, Sakramenti za Kanisa na Matendo ya Huruma: kiroho na Kimwili 

Frt. M. Lusato na wenzake kupewa Ushemasi, Roma: 24 Mei 2020

Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Jumapili tarehe 24 Mei 2020 anatarajia kutoa Daraja ya Ushemasi wa Mpito kwa Frater Michael Kanwagale Lusato kutoka Jimbo Katoliki la Bunda, nchini Tanzania, Frt. Kingsley Chukuebuka kutoka Jimbo Kuu la Onitsha nchini Nigeria na Frt. Carlos G. Cortez kutoka Jimbo Kuu la San Salvador nchini Salvador), katika Seminari ya Sedes Sapientiae!

Na Frt. Michael Kanwagale Lusato, -Roma.

Mashemasi hushiriki kwa namna ya pekee utume na neema ya Kristo Yesu mfufuka. Sakramenti ya Daraja Takatifu imegawanyika katika Madaraja makuu matatu: Daraja ya Uaskofu, Upadre na Ushemasi. Daraja ya Ushemasi “Diakonia” huwapa chapa isiyoweza kufutwa na hufananishwa na Kristo aliyejifanya Shemasi, yaani mtumishi wa watu, kama ilivyojionesha siku ile iliyotangulia kuteswa kwake, alipowaosha miguu Mitume wake kielelezo cha Injili ya upendo unaomwilishwa katika huduma makini kwa watu wa Mungu kama anavyosema Baba Mtakatifu Francisko. Dhamana na wajibu wa Shemasi katika maisha na utume wa Kanisa ni kuwa: Shuhuda na chombo cha huduma ya upendo na huruma ya Mungu inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Shemasi ni mhudumu wa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa.

Mashemasi wanawekwa wakfu kwa ajili ya huduma ya upendo kwa watu wa Mungu; ni mashuhuda wa utakatifu wa watu wa Mungu unaopata chimbuko lake katika maisha ya Sala za Kanisa; tafakari ya Neno Mungu na nidhamu katika maisha ya utii, useja na ufukara. Hiki ni kielelezo makini cha ufuasi wa Kristo Yesu kwa njia ya maisha ya wakfu! Utume na dhamana ya Mashemasi katika maisha ya Kanisa ni kwamba, wao ni wasaidizi wa karibu wa Maaskofu mahalia katika huduma ya Neno la Mungu, Mafumbo ya Kanisa kadiri ya daraja lao na hasa zaidi wadau wakuu katika utekelezaji wa matendo ya huruma kwa maskini, na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, watu ambao Kristo Yesu aliwapatia kipaumbele cha kwanza. Huu ni wito na mwaliko wa kujitoa bila ya kujibakiza kwa ajili ya Mungu, Kristo na Kanisa lake. Wito huu ni kwa ajili ya mafao ya Kanisa na wala si fursa ya mtu kujitafuta mwenyewe.

Askofu mkuu Jorge Carlos Patròn Wong, Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa kwa ajili ya Wakleri anayeshughulikia majiundo ya Majandokasisi, Jumapili tarehe 24 Mei 2020, Sherehe ya Kupaa Bwana Mbinguni, sanjari na Maadhimisho ya Siku ya 54 ya Upashanaji Habari Ulimwenguni anatarajia kutoa Daraja ya Ushemasi wa Mpito kwa Frater Michael Kanwagale Lusato kutoka Jimbo Katoliki la Bunda, nchini Tanzania, Frt. Kingsley Omenyi Chukuebuka kutoka Jimbo Kuu la Onitsha nchini Nigeria na Frt. Carlos Galdamez Cortez kutoka Jimbo Kuu la San Salvador nchini El Salvador) katika Seminari Kuu ya Bikira Maria Kikao cha Hekima. Ibada ya Misa Takatifu inaanza saa 11:30 jioni kwa saa za Ulaya. Lakini kutokana itifaki ya kudhibiti maambukizi ya homa kali ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya COVID-19, Ibada hii itahudhuriwa na wawakilishi tu! Kwa mara nyingine tena, COVID-19 imetunyima fursa ya kushiriki Ibada ya Misa Takatifu! Hakuna “Punga” baada ya kukaa karantini kwa miezi miwili na kwa hakika, vile vidogori kutoka Ukerewe, havitasikika. Mashemasi wanawakaribisha kuwasindikiza kwa sala na sadaka zenu, ili waendelee kujifunza kutoka katika Shule ya Bikira Maria, Kikao cha Hekima!

HISTORIA FUPI: Mimi Michael Kanwagale Lusato, natokea Parokia na Mtakatifu Yosefu Baba mlishi wa Yesu Kristo, Nansio, Ukerewe, Jimbo Katoliki la Bunda, nchini Tanzania, Afrika Mashariki. Nilizaliwa mnamo tarehe 25/07/1990 katika kijiji cha Bukiko (baba yangu alikuwa mwalimu wa shule ya msingi) kiwasani Ukara, Wilayani Ukerewe Mkoa wa Mwanza, nikiwa ni mtoto wa nne kati ya watoto saba wa Baba Laurent Kafunkulu Lusato (mwalimu mstaafu wa shule ya msingi) na mama Theopista Tabu Mazige (marehemu kwa sasa – alifariki 03/04/1999). Wanaonitangulia kuzaliwa ni kaka Paschal Lusato, dada Elisabeth Lusato (marehemu kwa sasa), kaka Nicholas Lusato, wadogo zangu ni Msegena Lusato, Welima Lusato na wa mwisho Elias Lusato. ELIMU: Nilianza masomo ya awali miaka miwili (1996-1997) na elimu ya msingi (1998-2005) vyote katika shule ya msingi Muhula wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza, kisha kujiunga na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Bukanda ambayo ni shule ya KATA (2006-2009) wilayani Ukerewe mkoa wa Mwanza. Nilipata elimu ya juu ya sekondari (Advanced edecation) katika shule ya sekondari ya wavulana Tarime iliyoko wilayani Tarime mkoa wa Mara (2010-2012) kwa mchepuo wa Sayansi katika masomo ya Fisikia, Kemia na Hisabati (PCM).

MWANZO WA WITO: Nilianza mafundisho ya Ukatekumeni mwaka 2000-2003 ambapo nilipokea Sakramenti ya Ubatizo mnamo tarehe 16/04/2003 na kupokea Sakramenti ya Komunyo ya kwanza na Kipaimara siku hiyo hiyo katika Kigango cha Mtakatifu Maria wa Rozari Takatifu Namasabo Parokia ya Nansio. Tangu nikiwa mdogo, nilizoea kwenda Kanisani pamoja na mama yangu, kaka zangu na dada zangu katika Kigango cha Mt. Maria wa Rozari Muhula ambapo ndipo mahali tulikuwa tunaishi kwa sababu baba yetu alikuwa mwalimu wa shule ya msingi Muhula. Tangu udogo wangu nilivyokuwa nikienda kanisani wakati wa Misa (mara moja kwa mwezi) mimi na watoto wengine tulikuwa tunakaa mbele karibu na Altare na nilipenda kumwangalia sana Padre alipokuwa akiendesha Misa na hasa wakati wa kipindi cha mageuzo. Kuna maneno ambayo yalikuwa yananigusa pale Padre alipokuwa akitamka: “Fanyeni hivi kwa kunikumbuka mimi”, na nilikuwa nikijiuliza kwa nini Padre anasema tufanye hivi kwa kumkumbuka? Nilifikiri anasema tufanye hivyo baada ya kufa kwake. Nilipenda sana kutumikia lakini kwa sababu nilikuwa ningali mdogo sikuweza kuanza kutumikia.

Baada ya kupokea Sakramenti ya Ubatizo, Komunyo ya kwanza na Kipaimara nilianza kutumikia mnamo mwaka 2003-2010 na hasa nilipenda kutumikia nikiwa nimeshika chetezo, ile harufu ya ubani, ilinifikirisha sana kuhusu sadaka. Mbali na hayo, nilianza kuvutiwa kuimba kwaya kwa sababu kaka yangu Nicholas alikuwa mwanakwaya tangu akiwa mdogo na kwa sababu pia nyumbani kwetu ndipo kilitunzwa kinanda. Sikuweza kujiunga na kwaya kwa sababu niliona aibu na ndipo baada ya kuanza masomo ya sekondari nilianza rasmi kuimba kwenye kwaya ya shule na ya kigangoni. Nilivyokuwa darasa la saba nilipenda kufanya mtihani wa kujiunga na seminari ndogo maana naweza kusema kuwa hapo ndipo nilipoanza kusikia wito huu bila mimi kujua. Baba yangu hakuwa tayari kulipa ada ya mtihani kwa kigezo kuwa hakuwa na fedha. Niliumia sana lakini sikuwa na namna nyingine ya kufanya kwa sababu nilikuwa bado mdogo.

Niliendelea na masomo ya sekondari katika shule ya sekondari Bukanda. Wakati nikiendelea na masomo ya sekondari (tukiwa ndio waanzilishi wa shule hiyo) tuliunda kwaya ambapo tulipata nafasi ya kuimba kwenye misa mbalimbali za vigangoni na hata Parokiani Nansio, na tulianzisha Chama cha YCS tukisaidiwa na shule ya sekondari Bukongo wilayani Ukerewe. Nilipata nafasi ya kuwa Katibu wa YCS shuleni kwetu tangu kidato cha kwanza hadi cha nne. Nilipata pia nafasi ya kuwa makamu mwenyekiti wa YCS kanda ya Nansio. Natambua kuwa Mungu alikuwa ananiita katika wito wa upadre japo nilikuwa sijatambua vizuri kwa sababu nakumbuka nilikuwa najisemea moyoni kuwa “kama Mungu anapenda mimi niwe Padre basi siku moja nitakuwa Padre.” Baada ya kumaliza kidato cha nne mwaka 2009 nilifaulu na kuendelea na masomo ya juu ya sekondari (Advanced edecation) katika shule ya sekondari Tarime iliyoko wilayani Tarime mkoa wa Mara (2010-2012). Wakati nikiwa Tarime sekondari nilipata nafasi ya kuwa Katibu wa YCS shuleni hapo na katibu mkuu wa YCS Kanda ya Tarime! Hapa yataka moyo kweli kweli si utani!

Katika kipindi cha Dini shuleni, tulipata nafasi ya kufundishwa Katekismu na Masista wa Shirika la Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (Ivrea) ambao wana nyumba yao Gamasara Parokia ya Tarime Jimbo Katoliki la Musoma. Tulikuwa pia tunapata nafasi ya kushiriki Misa za Dominika katika Parokia ya Tarime Mjini na nilijiunga pia na Chama cha Moyo Mtakatifu wa Yesu parokiani hapo, na mimi pamoja na wenzangu wawili tulipata ruhusa ya kuwa tunashiriki Misa siku ya jumamosi pamoja na sala za wanachama wa Moyo Mtakatifu wa Yesu. Kwa njia hii nikakuza na kudumisha moyo wa sala! KUANZA KUGUNDUA WITO: Wakati nikiwa kidato cha tano, siku moja tulienda kuwatembelea Masista wa Ivrea kwenye nyumba yao siku ya Jumapili baada ya misa, mimi na marafiki zangu watatu, kati yao wawili waliongea na Sr. Oliva Emmanuel ambaye ndiye aliyekuwa anatufundisha katika kipindi cha Dini shuleni, kuwa wangependa kujiunga na Shirika la Mapadre wa Mateso (Passionist Fathers) baada ya kuhitimu kidato cha sita. Ndipo Sr. Oliva aliponiuliza mimi: Michael, wewe, Je? Kwa mara ya kwanza alinigusa sana kuhusu wito wa upadre ingawa nilimwambia kuwa ngoja nitafikiria. Niliporudi shuleni nilitafakari sana lakini baadaye sikuwa na maamuzi.

Nilivyorudi nyumbani likizo (nikiwa kidato cha tano), siku moja katekista mmoja (Deusdedit Bagonza) ambaye alikuwa ananifahamu (kwa sababu alikuwa anahudumia kigangoni kwetu) aliniambia kuwa ananiombea sana ili niwe padre, nilimshukuru lakini bado sikusikia kuitwa katika wito wa upadre. Nilianza kuwa nashiriki misa za asubuhi (misa za wiki jumatatu hadi jumamosi) parokiani kwetu Nansio wakati nikiwa likizo kwa sababu nilikuwa naishi kwa kaka yangu mkubwa Paschal Lusato ambapo ilikuwa takribani umbali wa kilometa moja na nusu kufika parokiani na nilianza kuwa nasoma somo la kwanza na zaburi wakati wa Misa. Inaonesha wazi kuwa Mungu alikuwa ananiita lakini mimi nilikuwa bado sijatambua sauti yake (1Samweli 3:7). Ndipo nilivyomaliza kidato cha tano 2011 Februari na kurudi likizo nyumbani, siku moja baada ya misa ya asubuhi katekista huyohuyo aliyeniambia mwanzo kuwa ananiombea ili niwe padre, aliniambia tena kuwa ananiombea niwe padre. Safari hii maneno yake yalinigusa sana moyoni na kusikia kuwa hakika Mungu ananiita katika wito wa upadre kiasi kwamba nilishindwa hata kujisomea kwa kuhangaishwa na sauti hii. Ndipo nilipomshirikisha dada yangu kuhusu mahangaiko ya sauti hii ya kuwa padre, yeye akanishauri kuwa napaswa kusali kumuuliza Mungu kama kweli ananiita au nasikia sauti nyingine.

Niliamua kusali novena kwa muda wa siku 9 kumwomba Mungu anifunulie kama ni kweli ananiita au la. Baada ya kumaliza novena bado sauti hii iliendelea kunihangaisha na kwa muda wote huo sikuweza kujisomea. Ndipo nilipotambua kuwa hii ni sauti ya Mungu. Niliamua kwenda kwa Paroko (wakati huo alikuwa Padre Andreas Msonge) kumueleza hamu yangu ya kuanza malezi ya upadre baada ya kumaliza kidato cha 6. Baada ya kuongea na Paroko na kukubali ombi langu (na kwa sababu alinifahamu kupitia VIWAWA) na kuniambia niandike barua ya maombi kwenda kwa Mkurugenzi wa Miito Jimboni, ndipo sikupata mahangaiko tena ya ile sauti. Kuanzia hapo nikawa na uhakika kuwa kweli Mungu ananiita nimtumikie. Niliwaeleza wazazi wangu na ndugu zangu na nafurahi kuwa hawakuwa na kikwazo kwangu, bali walifurahi kuwa Mungu ananiita katika wito huu. Niliendelea na masomo ya kidato cha sita na kumaliza. Baada ya kumaliza nilirudi nyumbani na kwenda parokiani ili kujua majibu ya Mkurugenzi wa Miito na kukuta barua ya kuwa Mkurugenzi amekubali. Paroko aliniambia nijiandae kwa ajili ya kwenda kuanza malezi Jimboni Bunda. Ndipo nilipoingia nyumba ya malezi Uaskofuni Bunda mnamo tarehe 08-03-2012.

Baada ya mwezi mmoja wa malezi kwa Baba Askofu Renatus Leonard Nkwande wakati huo akiwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Bunda, alinituma nikaendelee na malezi katika shule ya sekondari ya wavulana Murutunguru wilayani Ukerewe ambayo inamilikiwa na Jimbo Katoliki Bunda. Wakati nikiwa Murutunguru sekondari tulikuwa tunalelewa wawili chini ya mlezi Padre Robert Ibengwe ambaye ndiye aliyekuwa Mkuu wa shule. Wakati huohuo nilipewa pia kufundisha somo la Kemia kwa kidato cha kwanza na kusaidia kufundisha Hisabati kwa kidato cha pili na mara kadhaa kusaidia kufundisha Kemia kidato cha tatu na cha nne. Baada ya malezi nilichaguliwa kujiunga na masomo ya Falsafa katika Seminari Kuu ya Bikira Maria Malkia wa Malaika, Kibosho Jimbo Katoliki Moshi (2012-2015). Baada ya masomo ya Falsafa mwaka 2015 nilibaki Jimboni kwa utume na ndipo mwaka 2016 Baba Askofu Nkwande alinipa nafasi ya kwenda kusoma masomo ya taalimungu nchini Italia katika Mji wa Roma, katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu na kuhitimu mnamo mwaka 2019 mwezi Juni.

Baada ya kumaliza masomo ya taalimungu Baba Askofu aliomba nafasi ili nisome Shahada ya uzamili (master’s degree) katika sheria za Kanisa katika Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu, ambapo ndipo naendelea hadi sasa na Mungu akijalia nitapewa Daraja ya Ushemasi mnamo tarehe 24/05/2020 pamoja na wengine wawili (Kingsley Omenyi Chukuebuka kutoka Jimbo Kuu la Onitsha nchini Nigeria na Carlos Galdamez Cortez kutoka Jimbo Kuu la San Salvador nchini El Salvador) hapa katika Seminari Kuu ya Bikira Maria Kikao cha Hekima. SHUKRANI: Namshukuru Mungu kwa kunijalia wito huu bila mastahili yangu. Nawashukuru wazazi wangu kwa kunilea na kukubali niweze kufuata wito huu. Nawashukuru ndugu zangu kwa sala na ushauri wao wa kunitia moyo katika safari hii. Namshukuru sana baba Askofu Mkuu Renatus Leonard Nkwande wa Jimbo Kuu la Mwanza na Askofu wa kwanza wa Jimbo la Bunda kwa kunipokea, kunilea, kunisaidia na hatimaye kunipa nafasi ya kuja kusoma Roma kwa masomo ya taalimungu na kwa sasa shahada ya uzamili katika Sheria za Kanisa. Ametulea kwa upendo wa kibaba na kila mara tulijisikia kuwa tunaye Baba katika Jimbo. Mungu amzidishie siku nyingi katika kuwachunga kondoo aliokabidhiwa. Daima nitamkumbuka kwa upendo wake mkubwa.

Nawashukuru mapadre wa Jimbo la Bunda kwa namna ya pekee Padre Andreas Msonge ambaye ndiye aliyekuwa paroko wa parokia yangu ya nyumbani wakati naanza safari hii kwa ushauri wake mbalimbali na malezi yake. Nawashukuru mapadre walionilea na kunifundisha Kibosho Seminari, hapa nilipo Seminari Kuu ya Bikira Maria kikao cha Hekima (Collegio Ecclesiastico Internazionale, Sedes Sapientiae) na Chuo Kikuu cha Kipapa cha Msalaba Mtakatifu kinachomilikiwa na Mapadre wa Opus Dei, “Kazi ya Mungu” chini ya uongozi wa Monsinyo Fernando Ocariz. Nawashuruku masista wa Shirika la Upendo wa Bikira Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili (Ivrea) kwa malezi, sala zao, ushauri wao na msaada wao tangu nilipogundua wito huu wakati nikiwa kidato cha tano mpaka sasa, kwa namna ya pekee Sr. Christiana Seda na Sr. Oliva Emmanuel kwa ushauri wake na sala zake bila kuchoka. Mungu azidi kuwajalia mdumu katika wito wenu. Nawashukuru wafadhili wangu wanaonisomesha mpaka sasa kwani bila wao jimbo lisingeweza kunisomesha hapa Roma kutokana na gharama kuwa kubwa. Nawashuruku watu wote walionisaidia na wanaoendelea kunisaidia kwa hali na mali hata kwa kile kidogo. Mungu awabariki na kuwazidishia mema mengi mnayohitaji hapa duniani na kwa marehemu awajalie pumziko la milele Mbinguni.

UJUMBE KWA VIJANA: Ujumbe wangu kwa vijana ni kuwa, ili kutambua wito ambao Mungu anakuitia kwanza huna budi kusali kumuomba Mungu aweze kukufunulia ni wito gani anaotaka uishi. Lakini haiishii kusali tu, bali unapaswa pia kuomba msaada wa watu wazima katika imani wakiwemo wazazi ili wakuombee uweze kutambua wito wako kwa sababu Mungu anaweza kukuita kupitia kwa watu wengine kama ilivyotokea kwangu. Zaidi ya hapo, kijana anapaswa kuomba maaongozi ya walezi wa kiroho yaani mapadre ambao wako karibu naye kwa mfano paroko wake. Lakini pia kuomba maongozi na sala za watawa (masista) kwani hutolea muda wao mwingi kwa sala kuwaombea watu mbalimbali wakiwemo na vijana ili waweze kutambua wito wao. Mwisho niwaalike vijana wanaosikia kuitwa katika wito wa upadre wasiogope kwani Kanisa bado linahitaji wachungaji wengi sana ili kuendeleza kazi ya uinjilishaji ambao Kristo aliwaachia Mitume wake (Rej. Mt. 28:18-20; Mk. 16:15-16). Ni wazi kuwa uinjilishaji ni wajibu wa kila mkristo mbatizwa lakini kwa wakleri na watawa wanao wajibu mkubwa zaidi. Hivyo tunapaswa kuomba ili Bwana wa mavuno apeleke watenda kazi katika mavuno yake maana watenda kazi ni wachache (Mt. 9:38; Lk. 10:2).

Mashemasi Watarajiwa 2020
22 May 2020, 13:53