Tafuta

Harakati za watawa na watu wenye mapenzi mema katika kuwaandalia mahitaji muhimu watu wahitaji katika kipindi cha covid-19 Harakati za watawa na watu wenye mapenzi mema katika kuwaandalia mahitaji muhimu watu wahitaji katika kipindi cha covid-19 

Ask.Mkuu Jurkovič:Mataifa yazingatie afya kama mahitaji msingi ya binadamu!

Katikati ya janga hili,sote tumeshangazwa ukarimu ulivyo na uwezo wetu wa kukabiliana na janga katika nyanja zake zote katika kila sehemu ya ulimwengu,huku tukitazamia siku zijazo kwa ubunifu na tumaini.Ni kwa kutoa ushuhuda wa mshikamano halisi ambao ni muhimu katika kushughulikia changamoto za ulimwengu wa nyakati zetu.Ni kwa mujibu wa Askofu Mkuu Jurkovič mwakilishi wa Kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa huko Geneva kwenye Mkutano wa 73 wa Shirika la Afya Ulimwenguni.

Na Sr. Angela Rawezaula-Vatican

Hotuba ya Askofu Mkuu Ivan Jurkovič Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa zilizoko jijini Geneva, katika Mkutano 73 Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) uliofanyika tarehe 18-19 Mei 2020, ambapo amesisitia juu ya afya kama msingi wa pamoja unaohitaji mshikamano. Akianza hotuba yake amesema, mazingira ambayo wamejikuta wanafanyia mkutano, mbali na umati wa kawaida walio uzoea kwenye Jengo la Kimataifa na ajenda kama hiyo, ni ukumbusho mzuri na tosha kwa kile ambacho Papa Francisko alieelezea kuwa ni “usiku wa ulimwengu ambao tayari umekabiliwa na changamoto kubwa ya wakati na sasa tumekandamizwa na janga lililojaribu sana familia yote ya wanadamu”. 

Uwakilishi wake amesema Askofu Mkuu Jurkovič, unaendelea kuzingatia jitihada za jamuiya ya kimataifa ya kuhamasisha majibu ya dharura katika kila sehemu ya ulimwengu. Hali hii isiyo ya kawaida inaleta nuru mpya ya kuegemea kati ya Mataifa hasa juu ya umuhimu wa kuzingatia afya kama faida msingi wa pamoja ambayo inahitaji mshikamano na hatua zinazoratibiwa kwa ngazi ya ulimwengu. Katika wito wa mara kwa mara wa  Papa Francisko, Vatican bado inabaki kusisitiza kwamba “walio hatarini zaidi na ambao ni kaka na dada zetu wanaoishi katika miji na mipaka ya kila sehemu ulimwenguni, wasiachwe peke”.

Kiukweli Askofu Mkuu amefafanua kuwa nchi nyingi ziko hatarini sana kuhusu matokeo ya mgogoro huu  wa janga  ambao unaweza kusababisha njaa zaidi na kukosekana kwa utulivu, hasa katika maeneo hayo ambayo yameshapata hali ya dharura. Kwa kuthibitisha amesema duniani kote baadhi ya hospitali 5,000  Katoliki,   zaidi kliniki 16,000 za madhehebu mengine ya Kanisa, zinakamilisha na kuimarisha juhudi za serikali katika kutoa huduma ya afya kwa wote, kwa kuwahakikishia watu maskini zaidi na waliotengwa zaidi ambao wana mahitaji msingi  kama dawa na uwezekano wa huduma bora za afya. Katika maeneo mengi, Amesema Askofu Mkuu Jurkovič, Kanisa limefanya vifaa vipatikane ili kusaidia kutoa majibu ya ulimwengu kwa janga la covid-19.

Tangu mwanzo wa kuzuka, tukio hili Mashirika mengi ya kidini, parokia na mapadre wamekuwa mstari wa mbele, kuwatunza wale ambao wameambukizwa na familia zao. Kwa kuongezea, Vatican imeahidi kutoa mchango wa Mfuko wa Dharura kwa Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) katika kusaidia usambazaji wa Vifaa vya kinga Binafsi (PPE) kwa wafanyakazi na wahudumu  wa matibabu na  ambapo pia tayari wametoa michango mbali mbali kwa Kanda inayohitaji msaada wa haraka. Ushiriki wa Kanisa katika juhudi hii ya pamoja umeimarishwa hivi karibuni na uundaji wa Tume ya Vatican ya  Covid-19 na Papa Francisko. Tume hii imekwisha zindua miradi kadhaa ya kusaidia idadi ya watu walioathiriwa zaidi na janga hilo. Katika kipindi hiki cha mateso na shida, Ujumbe wake Askofu Mkuu Jurkovič  pia ameshukuru juhudi za Shirika la Afya Ulimwenguni (WHO) kubaki kwenye mazungumzo na viongozi wa dini na mashirika yanayoongozwa na dini katika jitihada za pamoja kuhakikisha kuwa mikusanyiko ya kidini inafanyika lakini kwa hatua zote za usafi kuwapo.

“Katikati ya janga hili, sote tumeshangazwa na kuona ukarimu ulivyo na uwezo wetu wa kukabiliana na janga hili katika nyanja zake zote na katika kila sehemu ya ulimwengu kwa kutazamia siku zijazo kwa ubunifu na tumaini ili  kushuhudia kwa mshikamano halisi ambao ni muhimu kwa kushughulikia changamoto za ulimwengu wa nyakati zetu. Uamuzi fulani katika ngazi ya kimataifa utakuwa na athari kwa afya ya mwili na kiakili kwa watu ambao walikuwa tayari wanaishi hali ngumu ya kibinadamu hata kabla ya janga. Katika mantiki hii, Vatican imependa kurudia kuunga mkono wake wito wa Katibu Mkuu wa ‘kusitisha mapigano kwa haraka ulimwenguni na katika pembe zote za ulimwengu’. Na hii ni pamoja na ‘kukomesha aina zote za uadui, kukuza uundaji wa njia za misaada ya kibinadamu, uwazi wa kidiplomasia na kuwasikiliza wale ambao wako katika mazingira hatarishi”.

Katika hili  Aidha Askofu Mkuu amesema ni sawa na Papa Francisko ambaye aliwaalika kuhusu ‘vikwazo vya kimataifa viweze kulegezwa, kwani  vinafanya iwe ngumu kwa nchi ambazo zimetengwa ili kutoa msaada wa kutosha kwa raia wao’. Kwa kuhitimisha Askofu Mkuu Jurkovič amependa kurudia kuonyesha matumaini kama aliyo nayo Papa Francisko kwamba utafiti unaosababishwa na janga la COVID-19 utafanywe  kwa njia zilizo wazi na isiyo kuwa na mawaa ili kuweza kupata chanjo  ya haraka na matibabu, wakati huo huo kuhakikisha ufikiaji wake unakuwa kwa watu wote kwa teknolojia muhimu ambazo zitamwezesha kila mtu aliyeambukizwa, katika kila sehemu ya ulimwengu, anapata huduma ya afya inayofaa.

20 May 2020, 16:26