Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin anasema, mapambano dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona yanahitaji umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya mafao ya wengi. Kardinali Pietro Parolin anasema, mapambano dhidi ya homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona yanahitaji umoja na mshikamano wa kimataifa kwa ajili ya mafao ya wengi. 

Kardinali Parolin: Janga la Virusi vya Corona, COVID: Mshikamano

Katika kipindi hiki cha mahangaiko ya ndani, watu wengi wanaonekana kutaharuki, kuchanganyikiwa na wana hofu juu ya hatima ya maisha yao kwa siku za usoni. Inaonekana kwamba, watu wengi wamesongwa na pingu za magonjwa na kifo kiko malangoni pao! Hawana tena mahali pa kuwaombolezea ndugu, jamaa na rafiki zao, Corona, COVID-19 imesababisha maafa makubwa duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, yanahitaji: umoja na mshikamano wa kimataifa, sadaka na majitoleo kwa ajili ya ustawi,  maendeleo na mafao ya wengi. Mama Kanisa kwa upande wake, anapenda kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema: Kufunga na kusali; kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali. Kujenga na kudumisha utamaduni wa kutafakari Neno la Mungu linalonafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu.

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican katika mahojiano maalum na Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano anabainisha kwamba, Kanisa liko karibu pamoja na wale wote wanaoteseka kutokana na  athari za maambukizi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Mama Kanisa anapenda kuwapatia watu wa Mungu ulinzi na tunza yake ya kimama wagonjwa na wale wote ambao wameathirika kutokana na ugonjwa huu ambao haubagui wala hauchagui. Katika kipindi hiki cha shida na mahangaiko ya ndani, watu wengi wanaonekana kutaharuki, kuchanganyikiwa pamoja na kuingiwa na hofu juu ya hatima ya maisha yao kwa siku za usoni. Inaonekana kwamba, watu wengi wamesongwa na pingu za magonjwa na kifo kiko malangoni pao! Hawana tena mahali pa kuwaombolezea ndugu, jamaa na rafiki zao, Corona, COVID-19 imesababisha maafa makubwa duniani.

Huzuni, simanzi na majonzi vimetanda kila pembe ya dunia! Kama ilivyokuwa kwa Martha na Maria, hata leo hii, Kristo Yesu anataka kuwaita waja wake kama alivyofanya kwa Lazaro, rafiki yake, kwa kumuita “Lazaro, njoo huku nje”. Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi hiki kigumu cha historia na maisha ya binadamu katika ulimwengu mamboleo anaendelea kuwahamasisha watu kuwa na imani, matumaini na mapendo; ili kujenga na kudumisha ari na mwamko mpya wa kusaidiana na kushikamana kama ndugu katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Baba Mtakatifu anaendelea kujitahidi kuwa karibu na watu wengi zaidi, ili kuwafariji, kuwaombea na kuwatia shime katika mahangaiko yao ya ndani kwa kufungua amana na hazina ya maisha ya kiroho.

Baba Mtakatifu kwa muda wa majuma mawili hivi amekuwa akitolea Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya nia mbali mbali! Sektretarieti kuu ya Vatican iko karibu na Makanisa mahalia ili kufuatilia yale yanayoendelea kujiri sehemu mbali mbali za dunia. Ugonjwa huu unaleta changamoto kwa watu wa Mungu kubadili sera, mtindo wa maisha na vipaumbele vyao, ili kujenga na kudumisha umoja, udugu wa kibinadamu na mshikamano wa kweli kwa kutambua kwamba, hakuna binadamu aliye mkamilifu, wote wanategemeana na kukamilishana. Binadamu ametambua kwamba, ni kiumbe tu na hatima ya maisha yake iko mikononi mwa Mwenyezi Mungu na wala si mtalawa wala mmiliki wa maisha yake kwani maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayopaswa kupokelewa, kulindwa na kudumishwa na wote! Ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 imewapigisha magoti watu wote duniani. Mbele ya changamoto zinazosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, mwanadamu ameonja kwamba, “hapa duniani si mali kitu”! Amekuwa mnyonge na mdogo kuliko hata “kidonge cha Pilton”. Mwanadamu hana uhakika wa usalama wake na wala hawezi kujihami dhidi ya ugonjwa huu kwa kutumia silaha za moto!

Katika muktadha na mazingira kama haya anasema Kardinali Pietro Parolin, waamini wamepata fursa ya kugundua tena ndani mwao tunu msingi za maisha ya ndoa na familia na kwamba, familia ni Kanisa dogo la nyumbani, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana kwa hali na mali! Ndiyo maana Baba Mtakatifu anaendelea kuwaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuungana katika sala ili kukimbilia ulinzi, huruma na upendo wa Mungu, kwa kusali na kufunga kama ilivyokuwa ile Sala ya Kiekumene ya Baba Yetu iliyowashirikisha waamini kutoka Makanisa mbali mbali. Mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia, yawasaidie kuadhimisha Juma Kuu kwa moyo wa ibada na uchaji, ili kukuza na kuimarisha imani, matumaini na mapendo! Watambue kwamba, Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu ni chemchemi ya maisha na uzima wa milele.

Hiki ni kipindi cha kuimarisha sera na mikakati ya shughuli za kichungaji inayosimikwa katika ubunifu, kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali muda, vitu na watu inatumika vyema kwa ajili ya kuokoa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Watu wajenge umoja na mshikamano wa udugu wa kibinadamu, ili kamwe asiwepo mtu anayepoteza maisha katika hali ya upweke na kiza kinene katika maisha yake. Kardinali Pietro Parolin anasema kwamba, ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, “umekwisha kupiga hodi mjini Vatican na hivyo kulazimika kusitisha huduma za afya kwenye Zahanati ya Vatican. Kuna zaidi ya watu saba ambao wamekwisha kuambukizwa ugonjwa huu, lakini wanaendelea vyema kwa kupata dawa na tiba. Vatican inaendelea kufuatilia takwimu za maambukizi, vifo na wale wanaobahatika kupona na kurejea tena katika maisha ya kawaida. Baba Mtakatifu Francisko ameguswa na mateso ya watu wa Mungu sehemu mbali mbali za dunia kiasi hata cha kuchangia fedha katika huduma ya afya nchini China, Italia, Iran na Hispania. Kwa sasa Vatican inaendelea kutafakari hatua muhimu za kutekeleza kama sehemu ya mchango wake katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19.

Huu ni muda muafaka wa kutangaza na kushuhudia Injili ya upendo na mshikamano kwa waathirika wa Virusi vya Corona, COVID-19. Kutenga muda wa sala kwa ajili ya kuwaombea wagonjwa, wahudumu na wale wote waliotangulia mbele ya haki, wakiwa na imani na matumaini ya ufufuo na uzima wa milele. Kanisa linawahamasisha waamini kujiandaa vyema ili kuweza kupokea Rehema Kamili inayotolewa na Mama Kanisa kwa nyakati kama hizi. Waamini watumie fursa hii kujenga utamaduni wa kusoma, kutafakari na kumwilisha Neno la Mungu katika uhalisia wa maisha yao! Tafakari hii iwe ni shirikishi ili familia nzima iweze kujisikia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani.Ugonjwa huu umeibua changamoto kubwa katika maisha na utume wa Kanisa hasa katika huduma ya Sakramenti. Kuna wagonjwa wengi wanaoitupa mkono dunia bila ya huduma ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini walei wanaotekeleza dhamana na utume wao hospitalini na kwenye nyumba za wazee kuwa ni alama ya imani, matumaini na mapendo, kwa wagonjwa na wale wote walio kufani!

Huu ni ugonjwa ambao umezishambulia nchi tajiri na maskini. Mama Kanisa ana wasi wasi mkubwa ikiwa kama janga hili linavyoonekana katika nchi kama Italia, Hispania na Marekani, madhara yake pia yatatua na kutikisa nchi maskini duniani. Kanisa litaendelea kuonesha upendo na mshikamano na Makanisa yote mahalia, ili baada ya dhoruba hii kali, watu waweze kuwa na mwelekeo mpya na mpana zaidi katika maisha. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anahitimisha mahojiano yake kwa kusema, umefika wakati kwa viongozi mbali mbali kuwajibika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi badala ya kumezwa na utaifa usiokuwa na mashiko wala mvuto! Viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa waangalie njaga la ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 kwa kuzingatia hekima inayowawajibisha kulinda na kudumisha tunu msingi za maisha ili kukuza: uhuru, haki, amani, ustawi na maendeleo ya wengi!

Kardinali Parolin: Virusi vya Corona
06 April 2020, 13:49