Tafuta

Vatican News
Kanisa litaendelea kuunga mkono jitihada za wafanyakazi katika kada ya afya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19 Kanisa litaendelea kuunga mkono jitihada za wafanyakazi katika kada ya afya katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu inayosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19  (Vatican Media)

Mshikamano wa Kanisa katika mapambano dhidi ya Corona!

Kardinali Peter Turkson na ujumbe wake wamekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa afya hospitalini hapo ambao wako mstari wa mbele kwa sasa katika mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19. Amewapelekea salam kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayefuatilia kwa karibu sana mwenendo wa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID sehemu mbali mbali za dunia.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Katika vita dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19, Mama Kanisa anapenda kuwahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema: Kufunga na kusali; kushiriki Ibada ya Misa Takatifu kwa nia mbali mbali. Kujenga na kudumisha utamaduni wa kutafakari Neno la Mungu linalonafsishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili pamoja na Ibada ya Rozari Takatifu, ili kuwajengea watu imani, matumaini na mapendo katika kipindi hiki kigumu cha historia ya mwanadamu sanjari na kukimbilia faraja na wokovu kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Huduma ya Maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu, akiwa ameandamana na Monsinyo Segundo Tejado Muñoz, Katibu mkuu msaidizi pamoja na Padre Nicola Riccardi, Ijumaa tarehe 3 Aprili 2020 wametembelea Hospitali ya Agostino Gemelli iliyoko mjini Roma.

Hii ni nyumba ya tiba na afya ya mwanadamu katika mapambano dhidi ya magonjwa yanayomwandama mwanadamu! Kardinali Peter Kodwo Appiah Turkson na ujumbe wake wamekutana na kuzungumza na wafanyakazi wa sekta ya afya hospitalini hapo ambao wako mstari wa mbele kwa sasa katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa homa ya mapafu unaosababishwa na Virusi vya Corona, COVID-19. Amewapelekea salam na matashi mema kutoka kwa Baba Mtakatifu Francisko anayefuatilia kwa karibu sana mwenendo wa maambukizi ya Virusi vya Corona, COVID sehemu mbali mbali za dunia. Katika mapambano haya, watambue kwamba, Kanisa linaendelea kuwaunga mkono kwa kutumia amana na utajiri wake wa maisha ya kiroho. Mwishoni mwa mkutano wao, Kardinali Turkson amewapatia zawadi ya Rozari zilizobarikiwa na Baba Mtakatifu Francisko pamoja na kuwahakikishia uwepo wake wa karibu katika mapambano dhidi ya janga hili! Hii ni vita inayogusa na kutikisa mwili wa mwanadamu pamoja na undani wa maisha yake kiroho!

Kardinali Turkson

 

04 April 2020, 13:39