Tafuta

Vatican News
Kardinali George Pell ameshinda rufaa aliyokata kwenye Mahakama Kuu nchini Australia na kufutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yanamkabili, sasa ni mtu huru! Kardinali George Pell ameshinda rufaa aliyokata kwenye Mahakama Kuu nchini Australia na kufutiwa mashtaka yote yaliyokuwa yanamkabili, sasa ni mtu huru!  (AFP or licensors)

Kardinali George Pell, ashinda rufaa na kuachiwa huru!

Vatican imepokea taarifa ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Nchini Australia kwa kushinda kesi yake dhidi ya mashitaka yote yaliyokuwa yanamkabili, yaani nyanyaso dhidi ya watoto wadogo kwa imani kubwa! Kardinali Pell, mbele ya vyombo vya sheria nchini Australia aliendelea kukiri kwamba, hana hatia dhidi ya shutuma na hatimaye, hukumu iliyotolewa dhidi yake, sasa yuko huru.

Na Padre Richard A. Mjigwa, - Vatican.

Tangu mwanzo wa mchakato wa kesi dhidi ya Kardinali George Pell, Vatican ilionesha imani yake kwa vyombo vya sheria na mahakama nchini Australia. Vatican imepokea taarifa ya hukumu iliyotolewa na Mahakama Kuu Nchini Australia kwa kushinda kesi yake dhidi ya mashitaka yote yaliyokuwa yanamkabili, yaani nyanyaso dhidi ya watoto wadogo kwa imani kubwa! Kwa sasa Kardinali George Pell ni mtu huru asiyekuwa na hatia. Kardinali George Pell, mbele ya vyombo vya sheria nchini Australia aliendelea kukiri kwamba, hana hatia dhidi ya shutuma na hatimaye, hukumu iliyotolewa dhidi yake. Tangu wakati huo, alianza Njia ya Msalaba, akisubiri kwa imani na matumaini, ukweli uweze kudhihirika na haki kutendeka. Vatican inaendelea kukazia umuhimu wa viongozi wa Kanisa kusimama kidete kulinda na kutetea utu, heshima na haki msingi za watoto kwa kudhibiti vitendo vyote vinavyoweza kupelekea nyanyaso za kijinsia, kashfa ambayo imechafua maisha na utume wa Kanisa sehemu mbali mbali za dunia!

Itakumbukwa kwamba, Mahakama ya Victoria nchini Australia Mwezi Agosti, 2019 ilitupilia mbali rufaa iliyokuwa imetolewa na Kardinali George Pell aliyekuwa anatuhumiwa kwa kesi ya nyanyaso za kijinsia dhidi ya watoto wadogo na hivyo kupatikana na hatia. Kardinali Pell, ikamriwa kwamba,  aendelee kutumikia kifungo cha miaka sita jela, adhabu ambayo aliianza tangu tarehe 27 Februari 2019 kwenye gereza lenye ulinzi mkali nchini Australia. Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari akabainisha kwamba, Vatican inaheshimu na kuthamini hukumu iliyotolewa na Mahakama nchini humo. Kardinali Pell, daima amekuwa akijitetea kuwa hana hatia katika shutuma zote zinazoelekezwa dhidi yake na kwamba, kwa wakati huu, ameamua kukata rufaa kwenda kwenye Mahakama kuu nchini Australia. Vatican inaungana na Kanisa mahalia nchini Australia kuonesha uwepo wake wa karibu kwa wahanga wa nyanyaso za kijinsia pamoja na familia zao.

Vatican inaendelea kuwataka viongozi wa Kanisa kuhakikisha kwamba, wakleri wao wanawajibika barabara. Baraza la Kipapa la Mafundisho Tanzu ya Kanisa linasubiri kukamilika kwa kesi hii na hatimaye liweze kutoa maamuzi mintarafu Sheria, kanuni na taratibu za Kanisa. Baba Mtakatifu Francisko amekwisha kutoa maelekezo kwamba, kadiri ya Sheria, taratibu na kanuni za Kanisa, Kardinali George Pell haruhusiwi tena kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa hadharani wala kukaribiana na watoto wadogo. Dr. Matteo Bruni Msemaji mkuu wa Vatican katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alibainisha kwamba, Kardinali George Pell amesikitishwa sana na hukumu iliyotolewa dhidi yake, kati ya Majaji watu, wawili peke yao ndio waliomkuta na hatia. Kardinali George Pell anaendelea kukiri kwamba, hana hatia dhidi ya shutuma na hatimaye, hukumu iliyotolewa dhidi yake.

Baraza la Maaskofu Katoliki nchini Australia lilisema wakati ule kwamba, kwa hakika kila mtu ni sawa mbele ya sheria za nchi, lakini hukumu iliyotolewa dhidi ya Kardinali Pell imewashangaza wengi. Kumekuwepo na utata mkubwa katika kutafuta, ili kuweza kuupata ukweli wenyewe. Mawazo na sala zao, zinaelekezwa kwa wale waliopeleka shitaka hili mahakamani. Kanisa litaendelea kumpatia Kardinali Pell huduma za maisha ya kiroho na kichungaji kama ilivyo hata kwa wafungwa na maabusu wengine nchini Australia.

Kardinali Pell
07 April 2020, 14:14