Tafuta

Vatican News
2020.04.14 Askofu Mkuu Camillo Ballin na Papa Francisko 2020.04.14 Askofu Mkuu Camillo Ballin na Papa Francisko  

Askofu Mkuu Ballin aliyekuwa balozi wa Saudi Arabia ameaga dunia

Askofu Mkuu Camillo Ballin alitumikia maisha yake kati ya Misri,Sudan na Kuwait na amekuwa Balozi wa kitume nchini Saudi Arabia.Aliteuliwa na Papa Mstaafu Benedikto XVI kunako 2011.Katika siku ya ufufuko wa Bwana ameitwa kwake mbinguni!

Na Sr. Angela Rwezaula – Vatican

Mmisionari na askofu aliyetambua kujituma katika maisha yake kwa kumwiga  na kumfuasa Yesu katika huduma ya jumuiya za kikristo zilizoko katika Nchi za Saudi Arabia, ambapo sehemu kubwa ya wazalendo ni waislam. Huyo ni Askofu Mkuu Camillo Ballin, aliyeaga dunia Jumapili ya Pasaka, tarehe 12 Aprili 2020 mjini Roma kwa sababu ya ugonjwa. Askofu Mkuu Ballin ameacha peno na ishara muhimu katika Kanisa, kwa sababu alikuwa Balozi wa Kwanza wa Kitume Nchi za Saudi Arabia Kaskazini. Papa Mstaafu Benedikto XVI alikuwa amemteuwa kunako tarehe 31 Mei 2011 na kwa maana hii alikuwa amemkabidhi majukumu ya kuongoza Jumuiya Katoliki zilizopo katika maeneo ya Bahrain, Kuwait, Qatar na Saudi Arabia.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka shirika la habari za kimisionari Fides, Askofu Mkuu Ballin alikuwa amezaliwa huko Fontaniva wilaya ya Padua, Italia kunako tarehe 24 Juni 1944 na kuingia kwenye seminari ya kwanza ya Vicenza ambapo baadaye kunako mwaka 1963, akajiunga na Shirika la Wamisionari wa Kikomboni wa Moyo wa Yesu, mahali ambapo alifunga nadhiri zake za milele kunako tarehe 9 Septemba 1968.

Kunako tarehe 30 Machi 1969 alipewa daraja Takatifu la Upadre. Na baadaye kuanza safari ya kwenda nchini Lebanon na Siria kujifunza kiarabu. A alitoa huduma nchini Misri na baadaye kwa miaka 10 alikuwa nchini Sudan na kunako mwaka 2005 akateuliwa kuwa balozi wa kitume huko Kuwait.

Kwa miaka 15 amekuwa Balozi wa kitume huko Saudi Arabia ya Kaskazini, huku akihudumia jumuiya zilizotawanyika, ambazo ni matunda ya uhamiaji, kutoka nchini Ufilippini na India karibu watu milioni mbili na nusu na ambamo milioni moja na nusu wanaishi huko Saudi Arabia.

Akihojiana na Radio Vatican kunako mwaka 2014  kuhusiana na suala la ubinadamu na dini za watu wachache Askofu Ballin alikuwa amesema kuwa watu wote hata kama ni wachache ni lazima wasaidiwe, kwa kuwa kila mtu ni kiumbe wa Mungu, awe mkristo au la. Hata waislam wanayo makundi yaliyo madogo. Kila kikundi kidogo kina haki ya kuwapo, ya kuishi, kwa sababu kila mtu ni mtu kwa nini asongwe na kukandamizwa, kuwawa, anyongwe, waibiwe na wasurutishwe kubadili dini?

Kila mtu lazima awe na uhuru wa kuchagua dini anayoitaka, aishi kwa mujibu wa kuheshimiwa kama binadamu, jamii ya kibinadamu kwa mujibu wa haki za kibinadamu. Kila mtu ameumbwa na Mungu, hivyo kama kiumbe wa Mungu anayo haki ya kuishi maisha yake ya kibinadamu na kidini kama anavyotaka. Askofu Mkuu Camillo Ballin atakumbukwa sana kwa maana alikuwa ni mwanaume makini na mwenye busara. Katika mahojiano tena na Radio Vatican kunako  2016 alikuwa ametoa mwaliko kwa uislam wa kisasa, ili wasema ‘hapana’ kukubali misimamo mikali!

14 April 2020, 16:43