Tafuta

Vatican News
Tarehe 1 Machi 2020 Kanisa limeadhimisha Siku ya Wamisionari kutoka Hispania wanaotekeleza dhamana na utume wao Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Tarehe 1 Machi 2020 Kanisa limeadhimisha Siku ya Wamisionari kutoka Hispania wanaotekeleza dhamana na utume wao Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean.  (Vatican Media)

Siku ya Wamisionari wa Hispania wanaofanya Kazi Amerika ya Kusini

Kanisa Katoliki nchini Hispania linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, kwa kuchangia kwa hali na mali, shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Wamissionari kutoka Hispania huko Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Furaha ya Injili ni chemchemi inayobubujika kutoka kwa Yesu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kuanzia mwaka 1959, Kanisa linaadhimisha Siku ya Wahispania wanaofanya utume wao wa kimisionari Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, sherehe ambayo  imeadhimisha Jumapili, tarehe Mosi Machi, 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu “ Ili waweze kuwa na maisha tele kutoka kwa Mwenyezi Mungu”. Huu ni mwelekeo unaotoa msingi thabiti kwa waamini wanaoshirikishwa maisha ya Mwenyezi Mungu, ili nao kwa wakati wao, waweze kutoka kifua mbele kwa ajili ya kuwamegea pia jirani zao. Hii ni hija ya kimisionari inayotekelezwa na Mama Kanisa na kwa njia ya maisha, anakuwa kweli ni chemchemi ya maisha mapya anasema Kardinali Marc Armand Ouellet, Rais wa Tume ya Kipapa kwa ajili ya Amerika ya Kusini.

Hii ni siku ambayo Kanisa Katoliki nchini Hispania linawahamasisha waamini na watu wote wenye mapenzi mema, kuonesha mshikamano wa upendo na udugu wa kibinadamu, kwa kuchangia kwa hali na mali, shughuli mbali mbali za kichungaji zinazotekelezwa na Wamissionari kutoka Hispania huko Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean. Furaha ya Injili ni chemchemi inayobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa lake na Wainjilishaji wanapaswa kuwashirikisha wale wanaowainjilisha. Kumbe, Uinjilishaji wa watu hauna budi kujikita katika furaha, ukarimu na upendo wa dhati, huku Wainjilishaji wenyewe wakionesha ushupavu wa kutangaza Injili pasi na kukata tamaa wala kuchoka.

Takwimu zinaonesha kwamba, hadi kufikia mwaka 2020 kuna wamisionari 208 wanaoendelea kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Katika kipindi cha Mwaka 2019, kiasi cha Euro 58, 342, 43 zilikusanywa. Kardinali Marc Armand Ouellet katika ujumbe wake kwa maadhimisho ya Siku ya Wahispania wanaofanya utume wao wa kimisionari Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, anapenda kuwatia shime, ili wavumilie katika utekelezaji wa dhamana na wito wao wa kimisionari licha ya changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya utume wao wa kimisionari, Kristo Yesu anaendelea kukutana na waja wake katika imani, ili kuwakirimia maisha katika utimilifu wake.

Siku hii inahamasishwa kwa namna ya pekee kabisa na Baraza la Maaskofu Katoliki Hispania kwa kushirikiana na Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Amerika ya Kusini na Visiwa vya Caribbean, CELAM. Kanisa pamoja na mambo mengine linapania kushiriki kikikamilifu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, yatakayowawezesha watu wa Mungu kukutana na Kristo Yesu, anayewakirimia utimilifu wa maisha. Ushuhuda wa kimisionari unasimikwa kwa namna ya pekee katika upendo wa kimisionari unaotekelezwa na Mama Kanisa katika uhalisia wa vipaumbele vya maisha ya watu wa Mungu. Kumbe, mchakato wa uinjilishaji wa kina unagusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili, kama ushuhuda wa Kiinjili na ujenzi wa Ufalme wa Mungu.

Dhamana na wito huu unakwenda sanjari na changamoto inayotolewa na Baba Mtakatifu Francisko kuhusu umuhimu wa utekelezaji wa ekolojia fungamani katika maisha ya watu, kwa kushirikiana na wadau mbali mbali, ili kulinda na kudumisha kazi ya Uumbaji, yaani mazingira nyumba ya wote. Kimsingi, hii mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina unaopania kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu; mshikamano; majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni ili kujenga maisha mapya yanayobubujika kutoka katika tunu msingi za Kiinjili. Katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko katika hotuba yake ya kufunga maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Katoliki Ukanda wa Amazonia, alikazia kwa namna ya pekee, umuhimu wa Kanisa kutembea kwa pamoja, kwa kusikilizana na kushirikishana tunu msingi zinazobubujika kutoka katika amana na utajiri wa Kanisa.

Kardinali Marc Armand Ouellet katika ujumbe wake, amegusia pia changamoto za uinjilishaji Amerika ya Kusini na kwenye Visiwa vya Caribbean. Changamoto hizi ni pamoja na kushamiri kwa mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo; ukwapuaji wa rasilimali na utajiri wa maeneo haya kwa mafao ya watu wa chache; ukosefu wa usawa na haki. Ni eneo ambalo linakumbwa sana na vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kisiasa, kijaami na kiuchumi na matokeo yake ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: hifadhi, uhakika wa usalama wao pamoja na maisha bora zaidi. Ukoloni wa kiitikadi unaanza kujipenyeza kwa nguvu sana huko Amerika ya Kusini. Licha ya mateso na mahangaiko ya watu wa Mungu Amerika ya Kusini, bado furaha ya wamisionari katika kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu inaendelea kujionesha kama chombo cha neema ya Mungu. Huu ni ushuhuda wa upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo Yesu na Kanisa, changamoto na mwaliko wa kuendelea kutangaza na kushuhudia tunu msingi za Kiinjili katika Ukanda huu!

Wamisionari Amerika ya Kusini

 

02 March 2020, 11:03