Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Idara ya Rasilimali Watu itakayokuwa chini ya Baraza la Uchumi la Vatican, kama sehemu ya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Baba Mtakatifu Francisko ameanzisha Idara ya Rasilimali Watu itakayokuwa chini ya Baraza la Uchumi la Vatican, kama sehemu ya mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican.  (AFP or licensors)

Papa Francisko aanzisha Idara ya Rasilimali Watu mjini Vatican

Baba Mtakatifu Francisko kwa kufuata ushauri wa Baraza la Uchumi la Vatican, ameanzisha Idara ya Rasilimali Watu itakayokuwa chini ya Sekretarieti kuu ya Vatican kwa ajili ya kuratibu rasilimali watu. Benki Kuu ya Vatican, IOR, Viwanda, Mashirika pamoja na Mifuko mbali mbali ambayo iko chini ya uongozi na usimamizi wa Vatican. Hii ni sehemu ya mageuzi makubwa ndani ya Vatican.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sekretarieti ya Uchumi mjini Vatican inaratibiwa na Baraza la Uchumi la Vatican lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 24 Februari 2014 kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni: huduma makini, ukweli, uwazi na nidhamu katika matumizi ya rasilimali fedha za Kanisa ambazo kimsingi ni kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili kwa watu wa Mataifa. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuandaa bejeti ya Vatican na taasisi zake. Udhibiti wa matumizi ya fedha za Kanisa utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kwamba, kiwango cha bajeti kilichotengwa kinaheshimiwa kama sehemu ya maboresho ya huduma kwa watu wa Mungu kwa kuzingatia nidhamu, tija, weledi na ufanisi bora.

Ni katika muktadha huu, Baba Mtakatifu Francisko  kwa kufuata ushauri wa Baraza la Uchumi la Vatican, ameanzisha Idara ya Rasilimali Watu itakayokuwa chini ya Sekretarieti kuu ya Vatican kwa ajili ya kuratibu matumizi ya rasilimali watu. Hawa ni wafanyakazi kutoka katika: Benki Kuu ya Vatican, IOR, Viwanda, Uongozi, Mashirika pamoja na Mifuko mbali mbali ambayo iko chini ya uongozi na usimamizi wa Vatican. Hii ni taarifa ambayo imetolewa, Ijumaa tarehe 6 Machi 2020 kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa yanayoendelea kufanywa na Baba Mtakatifu Francisko kwa kushirikiana na Baraza la Makardinali Mashauri kwa kusoma alama za nyakati, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya Kanisa katika ulimwengu mamboleo.

Wakati wowote kuanzia sasa, Baba Mtakatifu anatarajiwa kumtangaza Mkurugenzi Mkuu wa Idara ya Rasilimali Watu mjini Varican. Idara hii itaendelea kushirikiana kwa karibu zaidi na Ofisi ya Kazi ya Vatican, Serikali ya Mji wa Vatican pamoja na Tume Huru ya Ajira ya Wafanyakazi Walei, (CIVA). Idara hii itakuwa na madaraka ya kimkakati; itachunguza na kutekeleza sera na mikakati ya ajira kutoka katika Idara na Mabaraza mbali mbali ya Kipapa. Ni Idara itakayoratibu wafanyakazi wote wa Vatican, sehemu mbali mbali za dunia. Ni matumaini ya Baraza la Makardinali Washauri kwamba, Idara hii itaweza kupokelewa kwa moyo wa shukrani na wale wote wanaohusika!

Idara ya Rasilimali Watu mjini Vatican

 

06 March 2020, 16:26