Tafuta

Vatican News
Mafungo ya Kipindi cha Kwaresima 2020: Ukimya unarutubusha maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu Mafungo ya Kipindi cha Kwaresima 2020: Ukimya unarutubusha maisha ya sala na tafakari ya Neno la Mungu  (Vatican Media)

Mafungo ya Kiroho: Ukimya unaorutubisha sala na tafakari ya kina ya Neno la Mungu!

Hatua ya kwanza katika maisha ya sala na tafakari inajengwa katika mazingira ya kufahamiana kwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kama inavyokaziwa kwenye maisha ya kiroho. Huu ni mchakato unaomwezesha mwamini kuona na kuonja mpango wa upendo na ukarimu wa Mungu unaotekelezwa katika maisha ya mwanadamu. Ukimya unarutubisha maisha ya sala na tafakari ya kina!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Tafakari wakati wa mafungo maisha ya kiroho kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu, “Curia Romana” kuanzia tarehe 1 Machi hadi 6 Machi, 2020 huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma, inaongozwa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Tema ya mafungo ni “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”. Utamaduni wa kumsikiliza Mwenyezi Mungu kutoka katika undani wa maisha ya mtu ni mang’amuzi ya kinabii kama yanavyofafanuliwa kwenye Maandiko Matakatifu. Vielelezo vikuu hapa ni kijiti kilichokuwa kinawaka moto pamoja na Neno la Mungu lililokuwa linatoka katika moto huu na kuiangazia njia hii ya maisha.

Kutokana na sababu zilizo nje ya uwezo wake, Baba Mtakatifu Francisko hataweza kushiriki katika mafungo ya Kipindi cha Kwaresima kwa mwaka 2020. Lakini katika barua aliyomwandikia Padre Pietro Enrico Bovati, amewatakia heri na baraka wote wanaoshiriki katika mafungo haya. Baba Mtakatifu anaendelea kushiriki mafungo haya akiwa chumbani kwake kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha, mjini Vatican. Baba Mtakatifu anawaomba pia washiriki wa mafungo haya kumsindikiza kwa sala katika maisha na utume wake. Mhusika mkuu katika tafakari hii ni Musa mtumishi wa Mungu, aliyeonja urafiki wa karibu sana na Mwenyezi Mungu, muumba wake. Jambo la msingi ni ukimya unaorutubisha hija ya maisha ya kiroho kama inavyosimuliwa katika Kitabu cha Kutoka.

Musa alitakiwa kuacha yote ili kuweza kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yake. Kijiti kilichokuwa kikiwaka moto bila ya kuteketea, ilikuwa ni hatua ya kwanza ya kutaka kuonana na Mwenyezi Mungu kwani: Kijiti hiki ni alama ya sala na mang’amuzi ya kinabii yanayobubujika kutoka katika ukimya wa ndani. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu alikuwa anazungumza na Musa kama marafiki. Hatua ya kwanza katika maisha ya sala na tafakari inajengwa katika mazingira ya kufahamiana kwa karibu zaidi na Mwenyezi Mungu, kama inavyokaziwa kwenye maisha ya kiroho. Huu ni mchakato unaomwezesha mwamini kuona na kuonja mpango wa upendo na ukarimu wa Mungu unaotekelezwa katika maisha ya mwanadamu. Kijiti kilichokuwa kikiwaka moto bila ya kuteketea ni kilele cha ufunuo wa Mungu kwa binadamu katika karama, udhaifu na umaskini wake, lakini huu ni ubinadamu ambao umegubikwa na nguvu ya maisha.

Huu ni moto aliokuwa anazungumzia Kristo Yesu katika mahubiri yake, ambao angependa kuuona unawaka kati ya waamini, yaani moto wa sala na ibada ya kweli kwa Mwenyezi Mungu. Huu ndio moto ambao walimwengu wanauhitaji kwa wakati huu. Watu wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya maisha ya kiroho, kwa hakika wanahitaji nguvu ya uponyaji inayoweza kutolewa na Mwenyezi Mungu. Mama Kanisa daima anapenda kuona watoto wake wakipyaisha maisha yao, kwa kujikita katika toba na wongofu wa ndani, ili kuwajibika zaidi katika maisha na utume wa Kanisa. Kama waamini na wafuasi wa Kristo wanaalikwa kwenda chumba cha juu, ili kusali na kutafakari Neno la Mungu, liweze kuwa kweli ni dira na mwongozo wa maisha! Kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu, kuna haja ya kuvua viatu, kwani hapa ni mahali patakatifu, panahitaji utulivu wa akili na mawazo, ili kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao!

Kwa mwamini kuweza kufikia hatua hii anasema, Padre Pietro Enrico Bovati, anapaswa kuwa na utambulisho wake kwa kutambua kwamba, ameumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Huu ni mwaliko kwa waamini kutafakari asili ya maisha, wito na utume wao, unaowapatia changamoto ya kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano ya dhati na Mwenyezi Mungu; jambo msingi katika maisha ya kiroho. Musa, mtumishi wa Mungu aliteuliwa kuwaongoza Waisraeli kutoka utumwani Misri, kama ilivyokuwa kwa Kristo Yesu, kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti, kama sehemu ya mchakato wa mpango wa ukombozi. Hiki ni kielelezo cha zawadi ya upendo wa Mungu kwa watoto wake wateule, walioumbwa kwa sura na mfano wake kwa makusudi maalum na wala si kwa bahati mbaya tu!

Musa alipambana na kifo tangu utoto wake, akalindwa na Mwenyezi Mungu, ili aweze kutekeleza mpango wake wa ukombozi, kielelezo cha huruma na upendo wake usiokuwa na kifani. Kuna vifo vya aina mbali mbali, kwa mfano kifo cha mwili na hata wakati mwingine kuna kifo cha maisha ya kiroho. Mwamini anapookolewa kwenye matukio haya ni lazima atambue kwamba, hiki ni kielelezo cha cha upendo wa Mungu. Ukombozi ni alama ya upendo wa Mungu kwa waja wake, kama unavyojidhihirisha katika Sakramenti ya Ubatizo. Ni katika sala, mwamini anaweza kutambua kwamba, kwa hakika anapendwa na Mungu anayetaka kumwokoa. Mwanadamu anaokolewa na Mungu kama ilivyokuwa kwa Musa, kielelezo cha huruma na upendo wake wa daima unaowawezesha kuwa ndugu zake Kristo Yesu.

Historia ya Musa inaonesha nguvu ya wanawake wanaojitokeza “kifua mbele” ili kumwokoa Musa, lakini katika Agano Jipya, Mtakatifu Yosefu anatumwa na Mungu kumwokoa Mtoto Yesu. Mtakatifu Yosefu ni mfano bora wa kuigwa katika maisha na utume wa kila mwamini kwa: kuonesha fadhila ya unyenyekevu na utayari wa kuisikiliza sauti ya Mungu na kutekeleza mapenzi yake kwa dhati. Waamini wajifunze kupenda na kujitoa sadaka kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kristo Yesu kwa njia ya Fumbo la Umwilisho, alirutubisha maisha yake kwa ushuhuda wa maneno na matendo ya watu mbali mbali walioshiriki katika majiundo yake kama binadamu. Zaburi ya 139 sala ya kujihifadhi na waovu imehitimisha tafakari iliyotolewa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu, tangu mwanzo wa mafungo haya, hadi Jumatatu, asubuhi, tarehe 2 Machi 2020.

Mafungo Ariccia

 

03 March 2020, 11:15