Tafuta

Vatican News
Mafungo ya Kiroho: Nyakati za Mashaka: Mang'amuzi na Unabii ni muhimu sana! Mafungo ya Kiroho: Nyakati za Mashaka: Mang'amuzi na Unabii ni muhimu sana!  (Vatican Media)

Mafungo ya Kiroho: Nyakati za mashaka: Mang'amuzi na Unabii!

Nyakati za mashaka zinahitaji mang’amuzi ya kina na unabii. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu daima yuko kati pamoja na wanafunzi wake wanaosikiliza na kutii, amri na maagizo yake, bila ya kujifungia katika ubinafsi. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua karama na utajiri waliokirimiwa katika maisha na utume wao, lakini pia wawe wepesi kukiri udhaifu na mapungufu yao!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mafungo ya kiroho wakati wa kipindi hiki cha Kwaresima kwa wasaidizi wa karibu wa Baba Mtakatifu Francisko yaani, “Curia Romana” kuanzia tarehe 1 Machi hadi Ijumaa tarehe 6 Machi, 2020 huko Ariccia nje kidogo ya mji wa Roma, mkazo zaidi umekuwa ni: Kuhusu mapambano ya maisha ya kiroho kwa kutumia silaha ya sala! Viongozi wa Kanisa wanapaswa kusimama kidete kuwalinda, kuwatetea na kuwaendeleza watu wa Mungu katika maeneo yao. Kanisa katika Ulimwengu mamboleo linakabiliana na mashambulizi makali dhidi ya maisha na utume wake. Ushuhuda wa imani umwilishwe katika huduma makini kwa watu wa Mungu. Tafakari hii imeongozwa na Padre Pietro Enrico Bovati, SJ, Katibu mkuu wa Tume ya Kipapa ya Biblia na Mtaalam wa Sayansi ya Maandiko Mtakatifu. Kauli mbiu ilikuwa ni: “Kile kijiti kiliwaka moto: mkutano kati ya Mwenyezi Mungu na binadamu mintarafu mwanga wa Kitabu cha Kutoka, Injili ya Mathayo na Sala ya Zaburi”.

Padre Pietro Enrico Bovati  katika tafakari aliyoitoa kama hitimisho ya tafakari ya Kipindi cha Kwaresima kwa wafanyakazi wa “Curia Romana”, Ijumaa, tarehe 6 Machi 2020 alisema, nyakati za mashaka zinahitaji mang’amuzi ya kina na unabii. Hii inatokana na ukweli kwamba, Kristo Yesu daima yuko kati pamoja na wanafunzi wake wanaosikiliza na kutii, amri na maagizo yake, bila ya kujifungia katika ubinafsi. Viongozi wa Kanisa wanapaswa kutambua karama na utajiri waliokirimiwa na Mwenyezi Mungu katika maisha na utume wao, lakini pia wawe wepesi kukiri udhaifu na mapungufu yao ya kibinadamu. Hata katika mazingira na hali kama hii, watambue kwamba, Kristo Yesu yuko pamoja nao hadi utimilifu wa nyakati.

Waamini watambue kwamba, Mwenyezi Mungu yuko pamoja na kati yao, kwani Yeye ndiye Emmanueli yaani, Mungu pamoja nasi!  Huyu ni Mwenyezi Mungu anayefunga safari na kuambatana na waja wake Jangwani kama ilivyokuwa kwa Waisraeli katika Agano la Kale. Daima, Musa aliwaongoza Waisraeli kwa kuwaonesha uwepo endelevu wa Mungu katika maisha yao. Akabahatika kupata neema na baraka ya kuongoza, kiasi cha kujenga mahusiano na mafungamano ya karibu na Mwenyezi Mungu. Ili kufanikisha azma hii, Kristo Yesu anawataka wafuasi wake wakitaka kuzungumza vyema na Mwenyezi Mungu wanapaswa kuingia katika undani wa maisha yao, kwani Baba yao wa mbinguni aliyeko sirini, atawasikiliza.

Sala si fursa kwa mwamini kutaka “kujimwambafai” na kujikutukuza mbele ya watu, bali iwe ni Ibada ya kutaka kumwabudu, kumshukuru, kumwomba na kumtukuza Mwenyezi Mungu. Matokeo yake ni upendo kwa Mungu na jirani kama ilivyokuwa kwa Musa, Mtumishi wa Mungu. Musa daima alipanda kwenda Mlimani ili kukutana na Mwenyezi Mungu. Uwepo wa Mungu katika maisha ya mwamini humkirimia: nguvu, neema na Roho Mtakatifu ili kuweza kutekeleza dhamana na wajibu wake. Kupanda Mlima wa Bwana ni changamoto endelevu inayohitaji moyo wa sadaka na majitoleo, ili hatimaye, kuweza kuinuliwa na Mwenyezi Mungu. Musa alionesha unyenyekevu na utii wa ndani na kamwe hakuomba kulipwa kwa kazi aliyoitenda, muujiza au kupewa ahadi kwa siku za usoni. Ilimtosha Musa kuwa ni shuhuda na chombo cha Mungu katika kazi ya kuwaokomboa Waisraeli kutoka utumwani Misri. Alikuwa ni Nabii wa Mungu, aliyejiaminisha kwake, ili Mungu aweze “kumfinyanga” kadiri alivyotaka, tayari kumtuma kutekeleza mapenzi yake.

Hivi ndivyo inavyopaswa kuwa kwa wakleri na watawa walioitwa, wakawekwa wakfu na kutumwa kwenda kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Musa alikuwa ni sauti ya watu wasiokuwa na sauti, faraja na kitulizo kwa Waisraeli waliokuwa wanaogopa hatima ya maisha yao mbele ya Waamaleki. Musa katika maisha na utume wake, alisaidiwa na watu kama Haruni, Huri na Joshua walioitegemeza mikono yake wakati wa sala na alipokuwa anatoa hukumu ya haki. Alipata ushauri kutoka kwa Baraza la wazee. Kwa ufupi hii ndiyo dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa! Yaani mchakato unaoliwezesha Kanisa kuwa na nia na lengo moja katika kupanga na kutekeleza sera na mikakati ya maisha na utume. Ni katika muktadha huu, watu wa Mungu wanaweza kusaidiana na kukamilishana kama ushuhuda makini wa uwepo endelevu wa Mungu kati ya waja wake.

Katika shida, magumu na changamoto katika maisha na utume wa Kanisa, kuna haja ya kujenga na kudumisha mang’amuzi ya kinabii, ili kutekeleza mpango wa Mungu. Wamtambue na kujiaminisha kwa Mwenyezi Mungu aliyewachagua na kuwaita kwa majina, ili watekeleze kazi yake ya ukombozi. Viongozi wa Kanisa wawe na ujasiri wa kuwapeleka watu wa Mungu kwenye maisha ya uzima wa milele. Amri za Mungu ni dira na mwongozo wa maisha adili na matakatifu. Amri hizi zinapaswa kufafanuliwa ili watu wa Mungu waweze kuzimwilisha katika uhalisia wa maisha yao. Mang’amuzi ya kinabii yanafumbatwa katika maisha ya sala; mazingira, historia na vipaumbele vya watu husika sanjari na kusoma alama za nyakati ili kutambua mapenzi ya Mungu ili kuweza kuyatekeleza.

Mang’amuzi ya kinabii anasema Padre Pietro Enrico Bovati ni uzoefu unaojengeka siku kwa siku, ili kuwasaidia watu kufanya maamuzi sahihi. Kumbe, hii ni zawadi ambayo viongozi wa Kanisa wanapaswa kuiendeleza katika wito na maisha yao; kwa kutambua kwamba, elimu haina mwisho! Mwenyezi Mungu anaendelea hata leo hii kuwatumia watu na mazingira ili kuweza kufikisha ujumbe wake. Mwinjili Mathayo katika Sura ya 28:16-20 anamwonesha Yesu Mfufuka akikutana na wanafunzi wake kumi na mmoja, kule Galilaya, chanzo na chemchemi ya wito na maisha yao ya kitume. Yesu akawaambia “Basi enendeni, mkawafanye mataifa yote kuwa ni wanafunzi”. Kwa hakika, Kristo Yesu alimwaga Damu yake azizi kwa ajili ya wengi. Kwa sasa ndiye Mchungaji mkuu wa kondoo wake, anawahimiza wachungaji na wafuasi wake kuwa kweli ni vyombo na mashuhuda wa huruma na upendo wa Mungu kwa walimwengu.

Mafungo: Unabii
07 March 2020, 14:22