Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limetoa Waraka kwa Ajili ya Familia Kanisa Dogo la Nyumbani ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika kipindi hiki kigumu! Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha limetoa Waraka kwa Ajili ya Familia Kanisa Dogo la Nyumbani ili kutangaza na kushuhudia Injili ya familia katika kipindi hiki kigumu! 

Waraka kwa Familia, Kanisa Dogo la Nyumbani: Mambo Msingi!

Huu ni wakati wa kugundua tena: Ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia kudumisha mafungano, ili kweli mahusiano ya wanandoa yaendelee kuziimarisha familia, Kanisa dogo la nyumbani. Papa Francisko anasema, Kristo Bwana, huwajia wanandoa Wakristo katika Sakramenti ya Ndoa na kubaki nao, katika tafakari ya Neno la Mungu, Sala na katika hali zote za maisha.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa tangu mwanzo limekuwa likitoa kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa familia, kwa kutambua kwamba, Familia ni Kanisa dogo la nyumba, shule ya upendo, huruma, haki na ukarimu. Ni mahali patakatifu ambapo tunu msingi za maisha ya kiroho, kiutu na kitamaduni zinarithishwa, tayari kuunda jamii inayowajibikiana na kutegemezana. Huu ndio mwelekeo wa pekee uliotolewa na Mababa wa Mtaguso mkuu wa Pili wa Vatican, changamoto inayofanyiwa kazi na Baba Mtakatifu Francisko, ili kweli familia ziweze kuwa ni mashuhuda wa Injili ya familia, kielelezo cha ukomavu wa imani. Mama Kanisa anawahimiza waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuhakikisha kwamba, kweli wanakuwa ni vyombo na mashuhuda wa Injili ya Ndoa na Familia, kwa kutangaza na kushuhudia: Ukuu, ukweli, uzuri, utakatifu na dhamana ya maisha ya ndoa na familia katika jamii. Lakini, familia katika ulimwengu mamboleo inakabiliwa na changamoto pevu kama zilivyoainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”.

Injili ya Kristo ni chemchemi inayowapatia wanafamilia ari, nguvu na jeuri ya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa nyakati hizi kwa kuzingatia tunu msingi za Injili ya familia mintarafu Mafundisho ya Kanisa. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika Waraka wake kwa wanandoa na familia sehemu mbali mbali za dunia katika kipindi hiki kigumu cha mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 anagusia elimu ya kiroho kuhusu ushirika wa Kimumgu kama inavyofafanuliwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Wosia wake wa Kitume, “Amoris laetitia” yaani “Furaha ya upendo ndani ya familia”: Uwepo wa Bwana hukaa katika familia halisi na imara, pamoja na shida na mahangaiko yao yote ya kila siku, furaha na matumaini yao. Familia ni amana na utajiri mkubwa katika maisha na utume wa Kanisa.

Mwenyezi Mungu daima amekuwa akiwasindikiza waja wake kwa ujumbe mahususi na anaendelea hata katika kipeo hiki cha maambukizi makubwa ya Virusi vya Corona, COVID-19. Watu wamelazimika kujifungia majumbani mwao, Ibada zimesitishwa kutokana na hatari kubwa iliyoko na watu wengi wanajisikia kuwa wapweke. Huu ni wakati wa kugundua tena: Ukuu, ukweli, uzuri na utakatifu wa maisha ya ndoa na familia, kwa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungano, ili kweli mahusiano ya wanandoa yageuke na kuendelea kujenga na kuziimarisha familia, Kanisa dogo la nyumbani. Baba Mtakatifu anasema, Kristo Bwana, huwajia wanandoa Wakristo katika Sakramenti ya Ndoa na kubaki nao, katika tafakari ya Neno la Mungu, Sala na katika hali zote za maisha.

Huu ni wakati muafaka wa kutangaza na kushuhudia familia kuwa ni Kanisa dogo la nyumbani, linalojengwa na kuimarishwa na wanandoa wenyewe katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwa kutambua kwamba, Kristo Bwana, yuko daima pamoja nao! Huu ni muda muafaka wa kufanya mazoezi na kumwilisha Injili ya huruma, upendo na msamaha. Ni wakati wa kukaa pamoja na wanafamilia ili kukazia malezi bora na utu wema. Ni wakati wa kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kusikilizana, kuheshimiana na kuthaminiana. Ni muda wa kuratibu vyema rasilimali muda kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia. Umefika wakati kwa wanandoa kuangaliana usoni bila kupepesa pepesa macho ili kujenga na kuimarisha upendo na urafiki wao wa dhati, daima wakimwachia nafasi Kristo Yesu. Mazoezi haya yasaidie kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya kiroho na kiutu. Ni muda wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Ni wakati muafaka wa kusali na kutafakari pamoja Neno la Mungu, ili janga la Virusi vya Corona, COVID-19 litakapopita na waamini kurejea tena Kanisani, wawe na ari na mwamko mpya.

Liturujia ya Kanisa la nyumbani ipewe uzito na msukumo wa pekee, ili kuachana na tabia ya kufanya mambo kwa mazoea. Maisha ya familia yageuzwe kuwa ni Liturujia ya Ndoa kwa njia ya Sala zinazowashirikisha wanafamilia wote, kwa kugawana majukumu; kwa kusoma na kushirikishana tafakari ya Neno la Mungu; kwa kusali kwa ajili ya mahitaji msingi ya familia pamoja na Kanisa katika ujumla wake, bila kusahau kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Mungu na Kanisa. Njia za mawasiliano ya jamii, ziwezeshe familia nyingi kuweza kuunganika kwa njia ya sala pamoja na kuwashirikisha watoto katika Liturujia hii ambayo inapaswa kuwa ni Liturujia shirikishi.

Wanandoa wanakumbushwa kwamba Sakramenti hii ni kwa ajili ya kuwatakatifuza na kuwakomboa wanandoa. Kwa sababu hiyo, wanandoa ni ukumbusho wa daima kwa Kanisa juu ya kile kilichotokea Msalabani; nao ni mashuhuda wa wokovu wanaoushiriki kwa njia ya Sakramenti kila mmoja mbele ya mwenzake na watoto wao. Wanandoa ni mashuhuda wa: unabii na utangazaji wa Habari Njema ya Wokovu unaomwilishwa katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku, kielelezo makini cha zawadi kama alivyofanya Kristo Yesu. Kardinali Kevin Joseph Farrell, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Walei, Familia na Maisha katika Waraka wake kwa wanandoa na familia anawahimiza wanandoa na familia kukigeuza kipindi hiki kuwa ni fursa ya neema katika mchakato wa ujenzi wa familia, kama Kanisa dogo la nyumbani.

Waraka kwa Familia

 

 

21 March 2020, 17:06