Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 mjini Vatican, hakutakuwepo na mahujaji wala waamini kutokana na kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19 kutishia usalama na maisha ya watu! Maadhimisho ya Juma Kuu kwa Mwaka 2020 mjini Vatican, hakutakuwepo na mahujaji wala waamini kutokana na kusambaa kwa virusi vya Corona, COVID-19 kutishia usalama na maisha ya watu! 

Ibada za Juma Kuu 2020 mjini Vatican: Hakutakuwa na mahujaji

Papa Francisko ataadhimisha Juma kuu bila ya uwepo wa waamini na mahujaji. Hata hivyo, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wataweza kufuatilia maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii. Hadi tarehe 12 Aprili 2020, Katekesi, Sala ya Malaika wa Bwana na Tafakari yake zitatolewa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano ya kijamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jumapili ya Matawi, Siku ya Vijana Ulimwenguni katika ngazi ya kijimbo ambayo inaadhimishwa tarehe 5 Aprili, 2020 kwa kuongozwa na kauli mbiu: “Kijana, nakuambia: Inuka”, Familia ya Mungu inamshangilia Kristo Yesu anapoingia mjini Yerusalemu kama Mfalme na Masiha, huku watoto wa Wayahudi wakitandaza nguo zao njiani! Jumapili ya Matawi ni mwanzo wa Juma kuu, ambamo Mama Kanisa anaadhimisha Mafumbo makuu ya Kanisa yaani: mateso, kifo na ufufuko wa Kristo Yesu kutoka kwa wafu, kiini cha imani na matumaini ya Kanisa. Kristo Yesu kwa njia ya utii wake anatimiza sadaka yake Msalabani.

Taarifa kutoka Vatican inabainisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko ataadhimisha Juma kuu bila ya uwepo wa waamini na mahujaji waliokuwa wanaomba fursa hii kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Hata hivyo, waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema wataweza kufuatilia maadhimisho haya kwa njia ya vyombo vya mawasiliano pamoja na mitandao ya kijamii. Hadi tarehe 12 Aprili 2020, Katekesi, Sala ya Malaika wa Bwana na Tafakari yake zitatolewa kwa njia ya vyombo vya mawasiliano na mitandao ya kijamii. Baba Mtakatifu Francisko ataendelea kuongoza Ibada ya Misa Takatifu kila siku itakayokuwa inarushwa kutoka kwenye Kikanisa cha Mtakatifu Martha, kilichoko mjini Vatican kuanzia saa 1:00 kwa saa za Ulaya. Zote hizi ni jitihada za Vatican pamoja na Serikali ya Italia kutekeleza kwa dhati itifaki ya mapambano dhidi ya Virusi vya Corona, COVID-19 ambavyo vinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao.

Kimsingi, Alhamisi kuu, tarehe 9 Aprili 2020, Kanisa linaadhimisha Siku ile Yesu alipoweka Sakramenti ya Ekaristi Takatifu na Sakramenti ya Daraja Takatifu na kuwapatia wafuasi wake kielelezo na mfano bora wa kuigwa katika upendo unaomwilishwa katika huduma makini, hasa kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili hata wao waweze kuonja huruma na upendo wa Mungu katika maisha yao! Ijumaa Kuu, 10 Aprili 2020 Kanisa linaadhimisha kumbu kumbu ya mateso na kifo cha Kristo Yesu kilichosababishwa na dhambi za binadamu kadiri ya Maandiko Matakatifu. Jumamosi kuu, 11 Aprili 2020 ni kipindi cha Mkesha, tayari kuadhimisha Siku kuu ya Pasaka, yaani Ufufuko wa Kristo Yesu, kutoka kwa wafu!

Juma Kuu 2020
16 March 2020, 10:56