Tafuta

Vatican News
Maaskofu Katoliki Ukanda wa Bahari ya Mediterrania wanasema, Kanisa bado lina dhamana ya kutangaza Injili na kurithisha imani licha ya changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza! Maaskofu Katoliki Ukanda wa Bahari ya Mediterrania wanasema, Kanisa bado lina dhamana ya kutangaza Injili na kurithisha imani licha ya changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza!  (ANSA)

Mchango wa Kanisa katika ujenzi wa amani Ukanda wa Mediterrania

Pamoja na mambo mengine, Maaskofu Katoliki kutoka katika Ukanda wa Mediterrania wakiwa mjini Bari, wamepembua kuhusu: changamoto ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo, mahusiano ya waamini wa dini mbali mbali na jamii katika ujumla wake; umuhimu wa waamini kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maaskofu Katoliki kutoka katika nchi zinazozunguka Ukanda wa Bahari ya Mediterrania wamekuwa na mkutano wa siku nne kuanzia tarehe 19-23 Februari 2020 kwa kukutana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Nicholaus wa Bari, Kusini mwa Italia. Pamoja na mambo mengine, Maaskofu wamepembua kuhusu: changamoto ya kutangaza na kushuhudia imani ya Kikristo, mahusiano ya waamini wa dini mbali mbali na jamii katika ujumla wake; umuhimu wa waamini kuwa ni vyombo na wajenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa. Kardinali Gualtiero Bassetti, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI katika hotuba yake elekezi amekazia kwa namna ya pekee kabisa umuhimu wa kudumisha majadiliano ya kidini na kiekimene mintarafu maono ya Giorgio La Pira, changamoto iliyovaliwa njuga na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Waamini wa dini mbali mbali wanapaswa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha uhai wa binadamu kwa sababu maisha ya binadamu ni matakatifu na Mwenyezi Mungu ndiye muasisi wake. Hii imekuwa ni fursa ya kukutana, kusikilizana na kujadiliana katika ukweli na uwazi. Maaskofu wamepata nafasi ya kusikiliza shuhuda mbali mbali kutokana na historia pamoja na uwapo wa watu mbali mbali. Maaskofu wameshirikishana utajiri unaobubujika kutoka katika Liturujia, tunu msingi za maisha na utume wa Makanisa mahalia; maisha ya kiroho; mambo yanayoshuhudia amana na utajiri wa Kanisa katika umoja na utofauti wake. Hii imekuwa ni fursa ya kuendelea kuimarisha dhana ya Sinodi katika maisha na utume wa Kanisa.

Kwa upande wake, Kardinali Vinko Puljić, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Vrhbosna na Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki la Bosnia-Erzegovina amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kuadhimisha Ibada ya Misa Takatifu katika Jimbo kuu la Bari, lenye historia kubwa katika maisha na utume wa Kanisa. Katika mkutano wao, anasema, Maaskofu wamegusia kuhusu changamoto ya wahamiaji; usawa pamoja na uhuru wa kuabudu. Wamekuwa ni sauti ya maskini na wanyonge wanaosukumiziwa pembezoni mwa jamii kutokana na nyanyaso, dhuluma za kidini pamoja na aina mbali mbali ya kinzani na mipasuko ya kijamii. Kuna makundi makubwa ya wakimbizi na wahamiaji wengi wao wakiwa ni vijana wanaokimbia: vita, umaskini na athari za mabadiliko ya tabia, lakini hata bado kuna vijana wanaothubutu kubakia katika nchi zao kama kielelezo cha uzalendo. Kuna wazee ambao wanaendelea kuwa ni rejea ya matumaini kwa Mwenyezi Mungu, huku wakiendelea kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kukazia haki msingi za binadamu na usawa; upendo na mshikamano.

Maaskofu wamepembua mambo yanayoendelea kuwatumbukiza watu katika malimwengu pamoja na ulaji wa kupindukia unaoathiri maisha ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Inasikitisha kuona kwamba, kuna baadhi ya Makanisa yameanza kuuzwa kutokana na kundi kubwa la Wakristo kuanza kukengeuka na kutopea katika malimwengu kiasi cha kushindwa kuona tena umuhimu wa kusali. Umefika wakati wa kukazia utamaduni wa Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo. Ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kuna haja kwa viongozi wa kidini kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na kukuza ushirikiano wa kidugu.

Wakati huo huo Askofu mkuu Pierbattista Pizzaballa, Msimamizi wa Kitume na Patriaki wa mji wa Yerusalemu amekazia mosi, umuhimu wa kusikilizana badala ya kuendekeza vita ya biashara na uchumi; uchu wa kupora nishati na madini; pengo kati ya maskini na matajiri. Badala yake, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi vipewe kipaumbele cha kwanza. Kanisa bado linayo dhamana ya kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo. Licha ya dhuluma na nyanyaso za kidini, bado kuna Wakristo ambao wameendelea kubaki imara huko Mashariki ya Kati. Hawa wanapaswa kuwezeshwa kwa hali na mali, kama kielelezo cha uaminifu na mshikamano wa Kikristo na kiutu!

Jumuiya za Wakristo zinataka kuendelea kuwa ni chemchemi ya amani, maendeleo na ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili kwa njia ya huduma makini ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Kanisa linataka kuendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini na kiekumene, ili kudumisha udugu wa kibinadamu katika ukweli wa kinabii na uhuru kamili. Maaskofu wanasema, kuna haja ya kuendelea kujenga utamaduni wa kukutana, ili kushirikishana mang’amuzi ya Kikristo, kuganga na kuponya madonda ya dhuluma, ili hatimaye, kuimarisha misingi ya umoja, haki na amani.

Naye Askofu mkuu Paul Desfarges, S.I. wa Jimbo kuu la Alger, nchini Algeria ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Kaskazini mwa Afrika, CERNA, kwa niaba ya Maaskofu Katoliki kutoka Ukanda wa Bahari ya Mediterrania, amemshukuru Baba Mtakatifu Francisko na kwa namna ya pekee, Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, CEI ambalo limehusika kikamilifu katika maandalizi ya mkutano huu. Changamoto kubwa kwa sasa ni wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji; majadiliano ya kidini na kiekumene pamoja na ekolojia. Ukanda wa Mediterrania unapaswa kuendelezwa ili kuwa ni chemchemi ya amani badala ya kuwa ni makaburi ya wakimbizi na wahamiaji pamoja na taka za sumu zinazohatarisha maisha ya watu wengi. Amemshukuru Baba Mtakatifu kwa ushuhuda wa maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa kujielekeza zaidi katika utu, heshima, ustawi na haki msingi za binadamu!

Amani Ukanda wa Mediterrania
24 February 2020, 09:16