Tafuta

Vatican News
Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, vyuo vikuu vina dhamana na wajibu wa kujenga na kudumisha diplomasia ya amani duniani. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, vyuo vikuu vina dhamana na wajibu wa kujenga na kudumisha diplomasia ya amani duniani. 

Wajibu wa Vyuo Vikuu Katika Ujenzi wa Diplomasia ya Amani!

Chuo kikuu kinapaswa kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani. Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora, ujuzi na maarifa. Chuo Kikuu cha Kikatoliki kinapaswa kupima mafanikio, matatizo na changamoto zinazojitokeza, ili kiweze kuchangia katika mchakato wa maendeleo fungamani, ukuaji wa uchumi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” Jimbo kuu la Milano, kilianzishwa ili kujibu hitaji la mahali pa malezi na majiundo makini ya vijana nchini Italia, changamoto iliyovaliwa njuga na Padre Agostino Gemelli na wasaidizi wake wa karibu akina Armida Barelli na Giuseppe Toniolo. Na matokeo yake katika kipindi cha uhai wake, Chuo hiki kimeendelea kukua na kupanuka na hatimaye, kuwa ni jukwaa la malezi na majiundo ya kielimu kitaifa na kimataifa! Ni kati ya vyuo vikuu vya kikatoliki maarufu sana Barani Ulaya. Kuna wanafunzi 43, 302 wanaopata elimu bora inayokidhi viwango vya soko la ajira Barani Ulaya. Ni chuo ambacho kimewekeza sana katika tafiti makini, ili kuendelea kusoma alama za nyakati. Haya ni matokeo ya sadaka kubwa ya akili na ukarimu inayotekelezwa na wadau wa Jumuiya ya Chuo Kikuu, bila kusahau kwamba, wanafunzi wana imani na wanathamini sana mchango huu.

Kumbe, kuna haja ya kukazia ari na mwamko wa kimisionari, tayari kutoka na kuanza kufanya tafiti za ukweli, ustawi na maendeleo ya wengi. Chuo Kikuu kiwe ni mfano bora wa kuigwa katika ukarimu, huduma makini kwa wanafunzi, kwa kutafuta na kuambata mafao ya wengi, sanjari na kupambana na changamoto mamboleo kuhusu: utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote, wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji duniani; mifumo mbali mbali ya ubaguzi, ukosefu wa haki, amani, maridhiano na umaskini duniani. Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, Alhamisi, tarehe 28 Novemba 2019 amezindua Mwaka wa Masomo wa Chuo Kikuu Cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore” kwa mwaka 2019-2020 na kukazia umuhimu wa Chuo kikuu kujikita katika diplomasia kwa ajili ya ujenzi wa amani duniani. Mama Kanisa anapenda kujielekeza zaidi katika sekta ya elimu ili kuwasaidia wanafunzi kupata elimu bora, ujuzi na maarifa pamoja na kuhakikisha kwamba, Chuo Kikuu cha Kikatoliki, mara kwa mara kinapima mafanikio, matatizo na changamoto zinazojitokeza, ili kiweze kuchangia katika mchakato wa maendeleo fungamani, ukuaji wa uchumi, majiundo makini pamoja na kuwajengea wanafunzi uwezo wa kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni katika muktadha huu, Chuo Kikuu kinapaswa kujielekeza zaidi katika kutoa nadharia ambayo inamwilishwa katika vitendo. Kwa kutambua changamoto zilizoko mbele yao na hivyo kutafuta nyenzo zitakazosaidia kupambana na matatizo pamoja na changamoto hizi ili hatimaye, suluhu ya kudumu iweze kupatikana kwa njia ya masomo yanayowapatia ujuzi, weledi na maarifa yanayotokana na tafiti makini za kisayansi. Kardinali Parolin amegusia umuhimu wa mahusiano ya kidiplomasia kati ya Vatican na mataifa mbali mbali duniani na kwamba, yanatekelezwa kwa uvumilivu mkubwa, hata sehemu ambazo kuna ugumu, kwa kuwa kuna matumaini ya familia bora ya wanadamu kwa siku za mbeleni. Shughuli za kidiplomasia ni nyenzo katika kufuatilia, kushiriki, na kutoa ushawishi katika Jumuiya ya Kimataifa. Utume wa Kanisa ni kuhangaikia kwa matumaini na kushuhudia ile hamu ya haki, amani, ustawi na mafao ya wengi.

Diplomasia ya Kanisa sio upendeleo kwa Kanisa, bali ni haki ya msingi ambayo Kanisa inayo, na hivyo katika Jumuiya ya Kimataifa, Kanisa lina haki sawa kama vyombo na Jumuiya zingine wanachama. Kwa zama hizi, ni wajibu wa Kanisa kutafuta mahusiano ya amani kati ya Mataifa, wakati likizingatia lengo la mwisho, yaani wokovu wa roho za watu. Katika ulimwengu mamboleo kuna matatizo na changamoto mbali mbali zinazohitaji kushughulikiwa kwa kutumia kanuni ya kidiplomasia. Leo hii kuna tabia ya ukuaji wa utaifa usiokuwa na mvuto wala mashiko kiasi cha baadhi ya mataifa kujimwambafai, na hivyo kuhatarisha diplomasia ya kimataifa. Kimsingi, matatizo na changamoto mbali mbali zinapaswa kujadiliwa kwa kuzingatia msingi ya ukweli na uwazi; kuibua mbinu mkakati na hatimaye, sera za utekelezaji wake. Changamoto kubwa kwa wakati huu ni amani. Kuna baadhi ya mataifa yanatishia kufumbia macho mafao ya wengi, hali ambayo inayatumbukiza mataifa yenye mwelekeo kama huo katika uchoyo na ubinafsi. Mafanikio ya taifa lolote liwe yanapata chimbuko lake katika elimu na tafiti makini.

Kwa upande wake, Prof. Franco Anelli, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore”, Milano katika hotuba yake elekezi amesema kwamba, Chuo hiki kwa sasa kimeanza maandalizi ya Maadhimisho ya Jubilei ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake. Amekazia umuhimu wa majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama sehemu ya ujenzi wa misingi ya haki na amani duniani. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni kati ya vipaumbele vinavyopaswa kufanyiwa kazi na Jumuiya ya Kimataifa. Chuo Kikuu kinapaswa kuwa ni mahali pa majiundo makini ya akili na sehemu ambayo itawawezesha wanafunzi kuwa na matumaini kwa leo na kesho iliyo bora zaidi. Chuo kiwasaidie wanafunzi kupata mawazo mapana kwa ajili ya: ujenzi wa udugu wa kibinadamu, ustawi na maendeleo ya mwanadamu pamoja na kuwa na matumizi sahihi ya teknolojia, kwa kuzingatia utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Elimu iwasaidie wanafunzi kudumisha ekolojia ya maendeleo fungamani, upendo na mshikamano kwa kuzingatia tunu msingi za maisha ya binadamu, tamaduni na mapokeo yao. Kuwepo na uwiano mzuri kati ya imani na uwezo wa mwanadamu kufikiri na kutenda, bila kusahau utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Majaalimu na wakufunzi wa vyuo vikuu wanapaswa kujiendeleza zaidi, ili kuwasaidia wanafunzi wao kuwa na uwezo wa kusoma alama za nyakati. Prof. Franco Anelli, Mkuu wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha “Sacro Cuore, Milano amesema, Chuo hiki kinaendelea kukuza utamaduni wa ukarimu kwa kuwapatia waalimu na wanafunzi fursa ya kufanya tafiti za kisayansi katika medani mbali mbali za maisha ya binadamu. Ukarimu unakiwezesha Chuo kuwajengea watu uwezo wa kiuchumi na kifedha pamoja na kuhakikisha kwamba, wanachuo wanahitimu vyema masomo yao na hivyo kuwajengea leo na kesho yenye matumaini zaidi.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Mario Enrico Delpini wa Jimbo kuu la Milano, Italia ambaye pia ni Rais wa Taasisi ya Giuseppe Toniolo amekaza kusema hiki ni kipindi muhimu cha kukazia utambulisho wake  kwa kuwa na mwono unaowashirikisha watu wengi zaidi pamoja na kuendelea kuwajibika kwa ajili ya familia ya Mungu nchini Italia sanjari na kuendeleza tafiti mbali mbali za kisayansi.

Kardinali Parolin: Elimu

 

 

03 December 2019, 16:32