Tafuta

Vatican News
Baraza la Makardinali Washauri linaendelea kuboresha muswada wa katiba ya Kitume: "Predicate evangelium" yaani "Tangazeni Injili" kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa. Baraza la Makardinali Washauri linaendelea kuboresha muswada wa katiba ya Kitume: "Predicate evangelium" yaani "Tangazeni Injili" kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.  (Vatican Media)

Mkutano wa XXXII wa Baraza la Makardinali Washauri: Mapendekezo!

Muswada wa Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Tangazeni Injili”: Mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican” kuanzia tarehe 13 Aprili, 2013 - 10 Aprili 2018, Unaendelea kufanyiwa maboresho kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa: Uhusiano kati ya Sekretarieti kuu ya Vatican na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki pamoja na uwepo na ushiriki wa walei ni muhimu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Makardinali Washauri, Jumatano tarehe 4 Desemba 2019 limehitimisha mkutano wake wa XXXII uliohudhuriwa na kuongozwa na Baba Mtakatifu Francisko. Makardinali wote washauri wamehudhuria. Dr.  Matteo Bruni, Msemaji mkuu wa Vatican wakati “akichonga” na waandishi wa Habari mjini Vatican mara baada ya mkutano wa Baraza la Makardinali Washauri amesema, Muswada wa Katiba Mpya ya Kitume “Predicate evangelium” yaani “Tangazeni Injili”: Mchakato wa mageuzi ya Sekretarieti kuu ya Vatican” kuanzia tarehe 13 Aprili, 2013 - 10 Aprili 2018, Unaendelea kufanyiwa maboresho zaidi kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa.

Muswada huu unadadavua hatua muhimu ambazo zimechukuliwa na kutekelezwa na Baba Mtakatifu Francisko katika kipindi cha miaka mitano ya uongozi wake, kuhusu uongozi wa Kanisa la Kiulimwengu sanjari na tema muhimu zinazogusa kwa namna ya pekee kabisa Katiba ya Kitume ya “Pastor bonus” yaani “Mchungaji mwema”. Maboresho haya yanafafanua kuhusu uhusiano kati ya Sekretarieti kuu ya Vatican na Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia; uwepo na ushiriki wa waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa; dhamana na wajibu wa maamuzi yanayotolewa na Ofisi mbali mbali kutoka Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na taasisi mbali mbali za Kanisa. Yote haya yamepembuliwa na mabingwa mintarafu mwelekeo wa kitaalimungu na shughuli za kichungaji.

Kardinali Michael Czerny, Katibu mkuu msaidizi, Idara ya Wahamiaji na Wakimbizi, Baraza ya Kipapa la Huduma ya Maendeleo Endelevu na Fungamani ya Binadamu ambaye alikuwa ni kati ya Makatibu Maalum wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia amewasilisha mbele ya Baraza la Makardinali washauri muhtasari wa maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Wamesikiliza ushauri kutoka kwa Kardinali Seàn Patrick O’Malley kuhusu namna ya kushughulikia Wosia wa Kitume baada ya maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Kardinali Reinhard Marx kwa upande wake, amedadavua Safari ya Sinodi ya Maaskofu Nchini Ujerumani na tema ambazo zitafanyiwa kazi. Tangu mwezi Septemba hadi siku chache tu zilizopita, kumekuwepo na mapendekezo zaidi kuhusu maboresho Muswada wa Katiba Mpya ya Kitume: “Predicate evangelium” yaani “Tangazeni Injili” mapendekezo ambayo yatashughulikiwa katika mkutano wa XXXIII wa Baraza la Makardinali Washauri ambao umepangwa kufanyika mwezi Februari 2020.

Baraza la Makardinali

 

05 December 2019, 15:05