Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, "Propaganda Fide" Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle kuwa Mwenyekiti mpya wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, "Propaganda Fide" 

Kardinali Luis Antonio Tagle: Mwenyekiti mpya wa Propaganda Fide: Uinjilishaji wa watu!

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kabla ya uteuzi huu, Kardinali Luis A. G. Tagle alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini. Alizaliwa Mwaka 1957 huko Manila na Mwaka 1982 akapewa Daraja takatifu. Tarehe 22 Oktoba 2001 akateuliwa na kuwekwa wakfu mwaka 2001

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali Edwin Frederick O’Brien la kutaka kung’atuka kutoka madarakani kama Mkuu wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalem “Order of the Holy Sepulchre of Jerusalem”. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu ameteua Kardinali Fernando Filoni kuwa mkuu mpya wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalem. Kabla ya uteuzi huu, Kardinali Filoni alikuwa ni Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu.  Katika muktadha huu wa mabadiliko makubwa katika Sekretarieti ya Vatican, Baba Mtakatifu Francisko amemteua Kardinali Luis Antonio Gokim Tagle, kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu. Kabla ya uteuzi huu, Kardinali Luis Antonio Tagle alikuwa ni Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Manila nchini Ufilippini. Itakumbukwa kwamba, Kardinali Tagle alizaliwa tarehe 21 juni 1957 huko mjini Manila, nchini Ufilippini. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, tarehe 27 Februari 1982 akapewa Daraja takatifu ya Upadre.

Ilikuwa ni tarehe 22 Oktoba 2001, Mtakatifu Yohane Paulo II alipomteuwa kuwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Imus na kuwekwa wakfu tarehe 12 Desemba 2001. Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akamteuwa kuwa Askofu mkuu tarehe 13 Oktoba 2011. Na hatimaye, tarehe 24 Novemba 2012, akateuliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI kuwa Kardinali. Kuanzia tarehe 14 Mei 2015 amekuwa ni Rais wa Shirikisho la Mashirika ya Misaada ya Kanisa Katoliki Kimataifa pia ni Rais wa Shirikisho la Vyama vya Biblia vya Kanisa Katoliki  Caritas Internationalis. Na tarehe 8 Desemba 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Propaganda Fide. Kardinali Tagle anafahamika sana kwa sadaka na majitoleo yake katika utume miongoni mwa vijana wa kizazi kipya

Kardinali Edwin Frederick O’Brien amemshukuru na kumpongeza Baba Mtakatifu Francisko kwa kumteuwa Kardinali Fernando Filoni kuwa mkuu mpya wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalem, kwa sababu ni kiongozi ambaye ana uzoefu mkubwa katika masuala ya shughuli za kichungaji na uongozi kwa Kanisa la kiulimwengu! Baba Mtakatifu anawashukuru na kuwapongeza wanachama wa Shirika la Ulinzi wa Kaburi Takatifu Yerusalem “Order of the Holy Sepulchre of Jerusalem”,  kwa kuendelea kujisadaka katika huduma ya elimu, afya, ustawi na maendeleo pasi na ubaguzi wa kidini, kielelezo makini cha ushuhuda wa tunu msingi za maisha ya Kikristo zinazomwilishwa katika huduma; majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama binadamu walioumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Katika mkutano wao, wamejikita zaidi katika dhamana na nafasi ya wafanyakazi mahalia, wanaotekeleza dhamana na utume wao katika nchi zaidi ya 30, ushuhuda wa upyaisho wa huduma inayotolewa na Shirika.

Baba Mtakatifu amewataka kukuza na kudumisha maisha ya kiroho ya wanachama wake, ili kudumisha uhusiano na mafungamano na Kristo Yesu kwa njia ya: Sala, Tafakari ya Neno la Mungu pamoja na uelewa makini wa Mafundisho Jamii ya Kanisa. Viongozi wakuu wa Shirika wawe ni mfano bora wa kuigwa kwa maneno na matendo yao, ili kuonesha kwamba, kweli uongozi ni huduma inayofumbatwa katika unyenyekevu! Huduma ya upendo inayotolewa na Shirika hili haina budi kujikita katika Injili ya upendo unaobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake; ushuhuda wa wema na upendo wa Mungu anayewapenda wote pasi na ubaguzi. Shirika hili ambalo linawashirikisha hata wakleri ni kielelezo cha huduma ya kichungaji inayowawajibisha kujenga maisha ya sala za kijumuiya, liturujua inayoadhimishwa katika ngazi mbali mbali, ili kumtukuza Mwenyezi Mungu na mwanadamu kukombolewa; mazoezi ya maisha ya kiroho na katekesi endelevu ni muhimu sana katika majiundo ya maisha na ukuaji wa wanachama wao.

Baba Mtakatifu anasikitika kusema kwamba, idadi ya Wakristo wanaouwawa kila siku inaongezeka maradufu. Mashuhuda wa imani ni wale ambao pia wananyimwa uhuru wa kidini na kuabudu hata katika nchi zile ambazo zinajidai kwamba, zina demokrasia ya kweli. Baba Mtakatifu anasema, yuko pamoja nao kwa njia ya sala na wasichoke kumwomba Bikira Maria wa Palestina, msaada wa Wakristo, ili awaombee nguvu na faraja wakati wa mateso na mahangaiko yao. Bikira Maria aendelee kuwaombea wale wote ambao uhuru wa kidini uko mashakani na daima wanatembea katika hofu ya kifo.

Propaganda Fide
08 December 2019, 16:53