Tafuta

Vatican News
Padre Guerrero Alves SJ., ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Mwenyekiti Skretarieti ya Uchumi Vatican. Padre Guerrero Alves SJ., ameteuliwa na Papa Francisko kuwa Mwenyekiti Skretarieti ya Uchumi Vatican.  (Society of Jesus)

Padre Juan Antonio G. Alves: Mwenyekiti wa Sekretarieti Uchumi

Padre Juan Antonio Guerrero Alves, kuanzia mwaka 2017 alikuwa ni Mshauri wa Mkuu wa Shirika, Mratibu na mwakilishi wa Mkuu wa Shirika katika shughuli mbali mbali za Kikanda. Padre Juan Alves, alizaliwa tarehe 20 Aprili 1959 huko Hispania. Kunako mwaka 1979 akajiunga na Shirika la Wayesuit na tarehe 30 Mei 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Amebobea katika uchumi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Mheshimiwa Padre Juan Antonio Guerrero Alves, S.I, kuwa Mwenyekiti wa Sekretarieti ya Uchumi Vatican. Taarifa inaonesha kwamba, ataanza rasmi kazi yake Mwezi Januari 2020. Kabla ya uteuzi huu, Padre Juan Antonio Guerrero Alves, kuanzia mwaka 2017 alikuwa ni Mshauri wa Mkuu wa Shirika la Wayesuit Ulimwenguni, Mratibu na mwakilishi wa Mkuu wa Shirika katika shughuli mbali mbali za Kanda ndani ya Shirika la Wayesuit, (DIR). Itakumbukwa kwamba, Padre Juan Antonio Guerrero Alves, alizaliwa tarehe 20 Aprili 1959 huko Mèrida, Hispania. Kunako mwaka 1979 akajiunga na Shirika la Wayesuit na baada ya majiundo yake ya kitawa, tarehe 30 Mei 1992 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Alijiendeleza kwa masomo mbali mbali nchini Hispania, Brazil, Ufaransa, Marekani na hatimaye akajipatia: Shahada ya uzamivu katika uchumi kunako mwaka 1986; Shahada ya uzamili katika Falsafa mwaka 1993 na Shahada ya uzamili katika Taalimungu mwaka 1994.

Kati ya mwaka 2008-2014 aliteuliwa kuwa Mkuu wa Kanda ya Castiglia nchini Hispania na mwaka 2014-2017 akatumwa nchini Msumbiji kama mchumi akiwa na dhamana ya kusimamia na kuratibu miradi mbali mbali ya Shirika. Itakumbukwa kwamba, Sekretarieti ya Uchumi Vatican inaratibiwa na Baraza la Uchumi la Vatican lililoanzishwa na Baba Mtakatifu Francisko hapo tarehe 24 Februari 2014 kama sehemu ya mchakato wa mageuzi makubwa katika Sekretarieti kuu ya Vatican. Vigezo muhimu vinavyozingatiwa ni: huduma makini, ukweli, uwazi na nidhamu katika masuala ya fedha za Kanisa. Kumekuwepo na mafanikio makubwa katika mchakato wa kuandaa bejeti ya Vatican na taasisi zake. Udhibiti wa matumizi ya fedha za Kanisa utaendelea kufanyika ili kuhakikisha kwamba, kiwango cha bajeti kilichotengwa kinaheshimiwa kama sehemu ya maboresho ya huduma kwa watu wa Mungu kwa kuzingatia nidhamu, tija, weledi na ufanisi bora.

Papa: Uteuzi Uchumi

 

15 November 2019, 10:23