Tafuta

Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbainiana kilichoko mjini Roma, hivi karibuni kimemtafakari Mwl. J.K. Nyerere 1922-1999: Fikra na mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa. Chuo Kikuu cha Kipapa cha Urbainiana kilichoko mjini Roma, hivi karibuni kimemtafakari Mwl. J.K. Nyerere 1922-1999: Fikra na mchango wake katika Jumuiya ya Kimataifa. 

Kumbu ya Mwalimu J.K. Nyerere 1922-1999: Mwalimu afunika Roma!

Mh. George K. Madafa, alibainisha kwamba maisha, fikra na mawazo ya Mwl. Nyerere yamefumbatwa na uadilifu, bidii, usawa, mshikamano na uvumilivu. Kama mtumishi wa serikali ya Tanzania, utendaji wake wa kazi ulisadifu kwa dhati fadhila na tunu msingi za maisha ya kikristo yaani; Imani, Matumaini na Mapendo kwa Mungu na unyenyekevu uliotukuka kwa watu aliowawahudumia.

Na Shemasi Karoli Joseph Amani – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anavialika vyuo vikuu na taasisi za elimu zinazosimamiwa na Kanisa Katoliki kukuza majadiliano kama kigezo msingi cha kupanua dhamiri ya mwanadamu katika kuuchunguza ukweli ili kama jumuiya kuufurahia na kubuni namna njema za kuuenzi na kuuishi (Veritatis Gaudium na. 4b). Kwa shime hii, Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana, kilichoko mjini Roma kimejitoma kumtafakari Mwl. Julius Kambarage Nyerere, Muasisi wa Taifa la Tanzania na Mwana majumui wa Afrika (Pan Africanist).  Shabaha yake msingi ni kuchangia kutanabahisha kiongozi huyu mwafrika mkatoliki aliyejibidiisha kusarifu kwamba siasa ni ''tunu faradhi ya upendo kwa sababu lengo lake ni kukuza faida na maendeleo ya wote ''(Evangelii Gaudium na. 205). Chuo kikuu cha kipapa Urbaniana kupitia Kitivo chake cha Taalimungu kikishirikiana na Kitivo cha Misiolojia kilitenga siku ya alhamisi, tarehe 07 novemba 2019 kumtafakari Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, fikra na mchango wake kwa maendeleo endelevu Tanzania, Afrika na uliwenguni kote. Ukumbi mkubwa wa Papa Mstaafu Benedikto wa XVI ulifurika wahadhiri, wageni na wanafunzi kutoka ndani na nje ya chuo hicho kufuatilia kwa makini mada na majadiliano kuhusu mchango wa Mwalimu Nyerere katika kusimamia utu, heshima, haki, ustawi na maendeleo ya watanzania na Afrika katika ujumla wake.

Katika hotuba yake, Balozi wa Tanzania nchini Italia Mh. George Kahema Madafa, alibainisha kwamba maisha, fikra na mawazo ya Mwl. Nyerere yamefumbatwa na uadilifu, bidii, usawa, mshikamano na uvumilivu usio na kipimo. Kama mtumishi wa serikali ya Tanzania, utendaji kazi wa Mwl. Nyerere ulisadifu kwa dhati fadhila na tunu msingi za maisha ya kikristo yaani; Imani, Matumaini na Mapendo kwa Mungu na unyenyekevu uliotukuka kwa watu aliowatumikia. Balozi Madafa alikazia kusema Mwl. Nyerere alikuwa nguzo msingi ya kuwaunganisha watanzania katika hekima, umoja na amani, tunu  faradhi zilizowalea watanzania; kuwaunganisha katika lugha moja ya Kiswahili na kuwawezesha kutambuana na kuishi kama ndugu licha ya wingi wa makabila yanayopatikana nchini Tanzania. Bidii yake katika kuuishi ukristo wake na kuwatumikia watanzania kwa: bidii, weledi na uadilifu mkubwa, vitaendelea kumfanya Mwl. Nyerere kuwa mwalimu maridhawa wa Imani na Siasa Safi kwa watanzania na ulimwengu mzima. Akiamini kuwa amani, maendeleo na salama ya Tanzania inahusiana kwa karibu na ile ya mataifa mengine, Mwl. Nyerere alikuwa daima tayari kusaidia mataifa mengine ya Afrika kujikwamua katika madhila ya harakati za ukombozi, umaskini, misukosuko na hali tete ya kisiasa.

Kwa upande wake, Padre Juvenalis Baitu Rwelamira Mhadhiri wa Chuo cha Kumbukumbu ya Kardinali Rugambwa Bukoba - Tanzania, akiwasilisha mada 'Nyerere, mkatoliki katika siasa', alimtaja Mwl. Nyerere kuwa mtu wa kujisadaka na kujitolea kwa ajili ya wanyonge. Daima alitilia mkazo maisha ya sala na kushiriki Sakramenti za Kanisa, hususan Ekaristi Takatifu. Alihudhuria Misa Takatifu kila siku na mara kwa mara alipokea Sakramenti ya Kitubio. Mwalimu alitumia ujuzi wake wa lugha za Kilatini na Kigiriki kutafsiri Maandiko Matakatifu na Katekisimu kwa lugha ya Kizanaki na Kikwaya kwa ajili ya kuwasaidia Wamisionari katika shughuli za uinjilishaji katika jamii ya wazanaki. Kimsingi huo pia ulikuwa ni mwanzo wa mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili. Alitambulika kwa ukarimu na majitoleo yake pamoja na kuwashirikisha wengine mazao ya kazi ya mikono yake. Akisukumwa na upendo kwa taifa lake na faida ya wananchi wote, alidiriki hata kuusadaka mshahara wake binafsi wa kazi ya ualimu, ili utumike katika shughuli za chama cha TANU kilichoongoza harakazi za kuikomboa Tanganyika iliyopata uhuru wake mnamo tarehe 09 Desemba 1961.

Mwl. Nyerere hakutoa nafasi wala kuendekeza upendeleo binafsi kwake wala kwa familia yake, bali alihimiza "kufyekelea" mbali matabaka ya kiuchumi, kikabila au kikanda. Alitilia mkazo watu wote kueshimiana licha ya tofauti zao kidini, kinasaba au kikabila. Aidha, Mwl. Nyerere alikuwa mpole kupokea marekebisho pale alipokosolewa na zaidi sana alitoa msamaha kwa wale walimkosea kwani kwake kukosa na kukosoana ni sehemu ya maisha ya binadamu. Ni kiongozi aliyeheshimu na kuthamini majadiliano ya kidini na kiekumene. Alisaidia waamini wa dini ya Kiislam kijijini Butiama kupata fedha za kujengea Msikiti. Rafiki zake kutoka Canada, wakamsaidia kujenga Kanisa ambalo leo hii ndilo Kanisa la Parokia ya Butiama, Jimbo Katoliki la Musoma. Mwl. Nyerere akang’atuka kutoka madarakani mwaka 1985 na kurejea Kijijini Butiama kuendelea na maisha kama raia na mkulima wa kawaida. Akimzungumzia Mwl. Nyerere katika mchakato wa ujenzi wa taifa la Tanzania, Prof. Antoine Pooda, Mhadhiri kutoka katika Kitivo cha Misiolojia Urbaniana, alimwita Mwl. Nyerere kuwa ni 'Mbuyu' akitafsiri dhana kwamba Mwl. Nyerere ni mtu muhimu aliyetoa mchango wake mkubwa katika harakati za kuwaelimisha watanzania na Afrika kiujumla kutumia akili zao wenyewe kubuni mifumo ya kujitegemeza na kujikwamua katika wimbi la umaskini, ujinga na maradhi; maadui nambari moja.

Prof. Antoine Pooda alisema Mwl. Nyerere hakutaka  hata  kidogo Tanzania kuwa nakala ya taifa lingine lolote bali, taifa "original", lililo huru na linalojitawala katika maamuzi na utendaji wake kuwahudumia watu wake. Katika hili, elimu ni ufunguo muhimu ili kufahamu mahitaji halisi ya taifa na kutengeneza mifumo stahiki kwa wakati na nafasi iliyopo. Prof, Pooda alisema Mwalimu Nyerere ni changamoto kwa watanzania na waafrika wote kwamba maendeleo ya Tanzania na Afrika kiujumla ni matunda ya maarifa na juhudi za watanzania na waafrika wenyewe kabla ya watu wengine. Sanjari na juhudi hizo, Mwal. Nyerere ni kielelezo na mfano wa matumizi ya elimu na weledi binafsi kupyaisha mifumo asili ya maendeleo ili kusadifu mahitaji ya watu katika zama wanazoishi. Aidha, alisisitiza hamasa ya Mwl. Nyerere kuwasaidia watanzania kutambua kwamba elimu na uongozi bora ni daraja linalovusha maendeleo kuwafikia watu na kuboresha maisha yao na wala siyo mfereji wa kujijazia fedha mifukoni.

Prof. Angelo Romano, Mhadhiri kutoka Kitivo cha Taalimungu na mzoefu aliebobea wa masuala ya usuluhishi Barani Afrika, alidadavua  mchango wa Mwl. Nyerere tangu enzi za hakati ya kutafuta Uhuru sanjari na ujenzi wa Umoja wa Afrika. Alisema Mwl. Nyerere alikuwa na busara kujiepusha na hila za mataifa ya kigeni mintarafu amani, umoja na maendeleo fungamani ya Tanzania na Afrika katika ujumla wake. Kama kiongozi makini Mwl. Nyerere alisimama kidete kuunda umoja miongoni mwa waafrika. Azma na bidii ya Mwl. Nyerere na viongozi wenzake wengine pia ilikuwa ni kuiunganisha Afrika nzima kuwa moja kwa kuunda Umoja wa Afrika. Hili lilikuwa jambo muhimu lakini lenye changamoto kubwa na tete sana kwa sababu ya utofauti mkubwa wa lugha, tamaduni, dini, makabila na kadhalika. Mwalimu alikazia Afrika kuungana hatua kwa hatua; lakini kwanza kuungana kikanda ili polepole nchi majirani zijilee na kuzoea kuungana kabla Afrika yote kiujumla haijaungana.

Ni katika muktadha huu, Mwl. Nyerere na viongozi wengine walifanya makubaliano na kujitanibu kuunda jumuiya mbalimbali za kikanda Barani Afrika, kama vile Jumuiya ya nchi za Afrika Mashariki (EAC), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na Jumuiya ya Kiuchumi ya Nchi za Afrika Magharibi (ECOWAS). Prof. Romano alikazia kwamba Mwal. Nyerere alikuwa nguzo muhimu katika juhudi za usuluhishi katika migogoro mbalimbali barani Afrika. Umahiri wake kaama mwalimu, uling'aa katika mioyo na macho ya wengi. Aliwakutanisha waliotofautiana na kutumia muda kuwaelekeza na kuzungumza nao kwa busara, upole na utulivu wa hali ya juu. Alisisitiza kwamba watu wasiokubaliana na kutoelewana wanapaswa kujifunza kukubali na kuwa tayari kuishi pamoja, licha ya tofauti zao. Kabla ya kupendekeza suluhisho Mwl. Nyerere alizoea daima kuanza kwanza kutanabahisha kanuni msingi za maisha ya mwanadamu, kufafanua miongozo na taratibu na mwishoni aliweka mapendekezo suluhishi aliyoona yangefaa kuondoa migogoro. Mchango wa Mwl. Nyerere katika kusuluhisha migogoro utabaki kuwa shule tosha ya demokrasia kwa ulimwengu mzima.

Mwl. Nyerere ni kani iliyosukuma watanzania na Afrika katika umoja, ukombozi, mikakati ya kujitawala, kujitegemea na kukuza maendeleo fungamani ya watu. Dhana ya ubaguzi wa aina yoyote ile ilileta kichefuchefu kwa Mwl. Nyerere. Alishirikiana na watu mbali mbali katika maisha, wito na utume wake kama kiongozi na mwamini Mkatoliki. Aliheshimu zawadi ya maisha dhidi ya utamaduni wa kifo. Hakupenda kufungamana na upande wowote kwa ajili ya masilahi mapana ya Tanzania na Afrika kwa ujumla. Mkuu wa Chuo cha Urbaniana Prof. Leonardo Sileo alimshukuru Balozi wa Tanzania nchini Italia, viongozi wawakilishi wa mataifa mbalimbali, watoa mada, wanafunzi na washiriki wote kuitikia wito na kuja kwa wingi katika tukio hili muhimu katika malezi ya wanafunzi, ambao ni tegemeo la Kanisa na Ulimwengu kiujumla. Alitumia wasaa huo pia kumkabidhi Balozi wa Tanzania nchini Italia George Kahema Madafa medali maalumu ya Chuo Kikuu cha Kipapa Urbaniana. Hiyo ni ishara ya kutambua mchango na ushuhuda wa Mwl. Julius Kambarage Nyerere katika kukuza maendeleo fungamani ya Watanzania, waafrika na ulimwengu mzima. Alimwita Mwl. Nyerere 'mwalimu wa upendo'.

Mwl. J.K. Nyerere 1922-1999
09 November 2019, 16:15