Tafuta

Vatican News
Kardinali Fernando Filoni anasema, vipaumbele vya Papa Francisko katika maisha na utume wa Kanisa ni: Uinjilishaji, Utunzaji bora wa mazingira, Maskini, Haki na Amani Duniani. Kardinali Fernando Filoni anasema, vipaumbele vya Papa Francisko katika maisha na utume wa Kanisa ni: Uinjilishaji, Utunzaji bora wa mazingira, Maskini, Haki na Amani Duniani.  (Vatican Media)

Vipaumbele vya maisha na utume wa Papa Francisko kwa Kanisa!

Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa mataifa yanayofumbatwa katika majadiliano.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Fernando Filoni, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa Watu, hivi karibuni, katika hotuba yake elekezi wakati wa ufunguzi wa Siku ya Masomo Kitivo cha Sheria za Kanisa Chuo Kikuu cha San Damaso, kwa kushirikiana na Jimbo kuu la Madrid, Mahakama ya Jimbo kuu la Madrid pamoja na Shule ya Sheria, amekazia ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa wafuasi wa Kristo. Amesema, Baba Mtakatifu Francisko katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, amejipambanua kwa kusimama kidete katika mchakato mzima wa uinjilishaji na utamadunisho; utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote na mapambano dhidi ya umaskini ili kulinda na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Siku hii maalum imeongozwa na kauli mbiu: “The Portico of the Church of Pope Francis” yaani “Vipaumbele vya Kanisa la Papa Francisko”. Baba Mtakatifu anaendelea kuwasaidia wamini kubadilisha misimamo na mitazamo yao ya kitamaduni, kwa kusoma alama za nyakati, ili kuliwezesha Kanisa kuachana na mazoea ya kujitafuta lenyewe kwa kujifungia Sakristia, na hivyo kuwa tayari kutoka kifua mbele kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa ari na moyo mkuu.

Changamoto hii inapaswa kumwilishwa katika maisha na utume wa Kanisa na hususan katika shughuli za: Mahakama za Kikanisa, Taalimungu, Sera na Mikakati ya Shughuli za Kichungaji; yote haya ni mambo yanayohitaji wongofu wa shughuli za kimisionari. Kardinali Fernando Filoni anasema, huu ni mwaliko kwa Kanisa kujenga na kudumisha majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaopania kuleta upyaisho katika maisha ya watu na kama njia muafaka ya kutamadunisha Injili ili kuinjilisha tamaduni miongoni mwa watu wa Mataifa. Kanisa halina budi kufungua malango ya maisha yake kwa kuzingatia mambo msingi yaliyobainishwa na Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Evangelii gaudium” yaani “Furaha ya Injili”. Baba Mtakatifu katika mlango huu wa kwanza anatoa kipaumbele cha pekee kwa furaha ya Injili, kwa kuwaalika waamini kushirikisha furaha yao inayopata chimbuko lake kutoka katika huruma na upendo wa Mungu kwa wanadamu.

Katika mwono huu, Kristo Yesu ni kiini cha furaha ya Injili na kwamba, Kanisa linaalikwa kufanya mageuzi makubwa kama sehemu ya uinjilishaji mpya unaokita mizizi yake katika ushuhuda. Waraka huu ni ramani inayotoa dira na mwongozo thabiti wa shughuli za kichungaji zinazopaswa kutekelezwa na Mama Kanisa kwa sasa na kwa siku za mbeleni kwa kuwa na mwono wa kinabii na mwelekeo chanya, licha ya vikwazo na changamoto zinazoendelea kujitokeza katika maisha na utume wa Kanisa, ili Kristo Mfufuka aendelee kupeperusha bendera ya ushindi. Waraka huu wa kitume unachota utajiri wake katika mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi juu ya Uinjilishaji Mpya kama njia ya kutangaza na kushuhudia Imani ya Kikristo katika ulimwengu mamboleo. Mlango wa pili katika vipaumbele vya Baba Mtakatifu Francisko unapatikana katika Waraka wa “Laudato Si”  yaani “Sifa iwe kwako” juu ya utunzaji wa nyumba ya wote”, anapembua kwa na kina mapana jinsi ambavyo uharibifu wa mazingira unavyohitaji kuwa na wongofu wa kiekolojia; kwa kuwa na mageuzi makubwa katika maisha, ili kweli mwanadamu aweze kuwajibika katika utunzaji wa nyumba ya wote.

Hii ni dhamana ya kijamii inayopania pia kung’oa umaskini, kwa kuwajali maskini pamoja na kuhakikisha kwamba, rasilimali ya dunia inatumika sawa na kwa ajili ya ustawi, maendeleo mafao ya watu wote duniani. Waraka huu unagusa maisha na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo. Mlango wa tatu katika vipaumbele vya Baba Mtakatifu ni majadiliano ya kidini kama yanavyofafanuliwa kwa kina na mapana katika Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu. Huu ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu wa kibinadamu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho.

Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Kardinali Fernando Filoni amedadavua na kupembua kwa kina na mapana umuhimu wa hati hii: kihistoria, kimaadili, kitamaduni na kijamii, kwa sababu ni hati ambayo imewashikirisha viongozi wakuu wa dini mbali mbali duniani, ambao wanaendelea kuhimiza umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita zaidi katika majadiliano ya kidini, ili kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja licha ya tofauti msingi zinazojitokeza kati yao. Lengo ni kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

kardinali Filoni
28 November 2019, 17:28