Tafuta

Vatican News
Familia ya Mungu Barani Asia inapwenda kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili kama mtetezi wa haki, amani, utu na heshima ya binadamu. Familia ya Mungu Barani Asia inapwenda kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kwa mikono miwili kama mtetezi wa haki, amani, utu na heshima ya binadamu.  (AFP or licensors)

Hija ya Papa Francisko Thailand: Nabii wa haki na amani!

Baba Mtakatifu Francisko anaonekana na wengi kuwa ni “Nabii wa nyakati hizi” ambaye katika maisha na utume wake, amekazia zaidi: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kama sehemu ua mchakato wa ujenzi wa haki na amani duniani.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand pamoja na Serikali ya Thailand wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019. Kauli mbiu inayoongoza hija hii ya kitume ni “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”. Hija hii ni sehemu ya maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Siam kuanzia mwaka 1669 hadi mwaka 2019. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Thailand wanaungana na vijana wa kizazi kipya kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, inayobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Waamini wanahimizwa kuzaa matunda ya ushuhuda wa imani yao, kwa kutambua kwamba, wako chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria, Mama wa Kanisa. Kardinali Charles Maung Bo, Askofu mkuu wa Jimbo la Yangon nchini Myanmar ambaye pia ni Rais wa Shirikisho la Mabaraza ya Maaskofu Katoliki Barani Asia, FABC, kwa niaba ya familia ya Mungu Barani Asia, anapenda kuchukua fursa hii, kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko Barani Asia.

Hija hii ya kitume, inafuatia ile iliyofanywa na Baba Mtakatifu Francisko nchini Myanmar na Bangaladesh, watu wa Mungu wakaonja upendo wa Kristo kwa njia ya Papa Francisko. Anamwelezea Baba Mtakatifu kuwa ni “Nabii wa nyakati hizi” ambaye katika maisha na utume wake, amekazia zaidi: Utu, heshima na haki msingi za binadamu; Utunzaji wa mazingira nyumba ya wote pamoja na umuhimu wa Jumuiya ya Kimataifa kukuza na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, kama sehemu ua mchakato wa ujenzi wa amani duniani. Baba Mtakatifu katika vipaumbele vya maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro, anapenda kuendelea kuwaimarisha ndugu zake katika imani kwa Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu. Nchi ya Thailand ina idadi ndogo sana ya Wakristo, ikilinganishwa na sehemu nyingine duniani! Lakini hapa ndipo Baba Mtakatifu ameamua kwa mwaka huu kupatembelea! Lengo ni kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini hata kwa wale ambao wako pembezoni mwa vipaumbele vya walimwengu.

Watu wa Mungu Barani Asia, wanayo kiu ya kutaka kuonana na kuzungumza na Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume nchini Thailand. Ni hujaji wa amani na matumaini na kwamba, uwepo wake ni chachu ya furaha, imani na matumaini ya watu wa Mungu. Hili ni tukio la neema na baraka, ili kuendelea kuwatia shime, kusimama kidete katika mchakato wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote. Hija hii ya kitume, inakuja mara tu baada ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 - 27 Oktoba, 2019 yaliyoongozwa na kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Baada ya kusikiliza kwa makini, sasa ni wakati wa kujikita katika wongofu wa kiekolojia, shughuli za kichungaji, kitamaduni pamoja na wongofu wa kisinodi, ili kutembea kwa kwa pamoja kama familia ya Mungu. Changamoto zote hizi kimsingi zinafumbatwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo, ili kukuza na kudumisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu katika ujumla wao.

Bara la Asia linakabiliwa na changamoto kubwa mbili yaani athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na umaskini. Thailand na Japan ni nchi ambazo zimetikiswa sana na athari za mabadiliko ya tabianchi, lakini zikasimama kidete, ili kupambana na changamnoto hizi. Watu wa Mungu wataweza kusikiliza mafundisho ya Baba Mtakatifu Francisko kuhusu changamoto hizi mintarafu mazingira ya Bara la Asia Kardinali Charles Maung Bo, anasema kwamba, tangu wakati huu, familia ya Mungu Barani Asia inapenda kuchukua fursa hii kumkaribisha kwa mikono miwili: “Nabii wa haki msingi za kiuchumi na utunzaji bora wa mazingira”. Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Baba Mtakatifu Francisko. Barani Asia, ataweza kukutana na kuzungumza na waamini wa dini mbali mbali, ili hatimaye kujenga na kudumisha madaraja yanayowakutanisha watu, kwa ajili ya: haki, amani, maridhiano,  ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amekubali mwaliko kutoka kwa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan pamoja na Serikali ya Japan wa kutembelea nchini humo kuanzia tarehe 23 hadi 26 Novemba 2019. Hija ya Baba Mtakatifu nchini Japan inaongozwa na kauli mbiu “Linda Maisha Yote”. Nembo ya hija hii ni mwali wa moto unaohimiza upendo unaopaswa kumwilishwa katika Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo kwa kulinda maisha. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Japan inapania pamoja na mambo mengine, kutangaza na kushuhudia Injili ya matumaini. Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linasema, maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu, yanayopaswa kulindwa, kutunzwa na kuendelezwa. Maandiko Matakatifu yanabainisha kwamba, Mwenyezi Mungu ndiye aliyeumba dunia na kuifanya, ndiye aliyeifanya imara, hakuimba ukiwa, aliiumba ili ikaliwe na watu. Ili kulinda utu, heshima na haki msingi za binadamu kuna haja wanasema Maaskofu kusimama kidete kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira nyumba ya wote.

Papa: Thailand
14 November 2019, 11:52