Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Japana linamwomba Baba Mtakatifu kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani ili kuondokana na hofu ya silaha za maangamizi duniani. Baraza la Maaskofu Katoliki Japana linamwomba Baba Mtakatifu kusaidia mchakato wa ujenzi wa amani ili kuondokana na hofu ya silaha za maangamizi duniani.  (Vatican Media)

Hija ya Kitume ya Papa Francisko nchini Japan: Maaskofu Japan

Wanamwomba Papa Francisko asimame kidete kuiasa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu madhara ya silaha za maangamizi. Pamoja na hayo yote, mwaka 2019 Japan inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Balozi wa kwanza wa Vatican alipotumwa nchini Japan. Maaskofu Katoliki Japan wanamwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie watu wa Mungu nchini Japan kuthamini Ukristo na Kanisa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kanisa Katoliki nchini Japan, mwaka 2019 linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 470 tangu alipowasili nchini humo, Mtakatifu Francisko Xavier pamoja na wenzake na huo ukawa ni mwanzo wa kuenea kwa Ukristo nchini Japan. Kunako mwaka 1614 madhulumu dhidi ya Wakristo yakafumuka na kupamba moto kwa takribani miaka 260 na waamini wengi wakauwawa kikatili kwa ajili ya imani yao kwa Kristo Yesu na Kanisa lake. Katika kipindi cha madhulumu, Wakristo waliokuwa wanaishi kwenye Mkoa wa Nagasaki waliendelea kupyaisha imani yao na kufanikiwa kuwarithisha wengine amana na utajiri huu kwa njia ya ushuhuda wa imani tendaji, sala na katekesi ya kina.

Hayo yamesemwa na Askofu mkuu Joseph Mitsuaki Takami, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, CBCJ, Jumamosi tarehe 23 Novemba 2019, wakati wa hotuba yake ya utangulizi kwa ajili ya kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko kutembelea nchini Japan. Watu wa Mungu nchini Japan ni wapenda amani, utulivu na watunzaji bora wa mazingira. Lakini kuna matatizo chungu nzima kuhusu maisha yanayokwamisha mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Ni matumaini ya Baraza la Maaskofu Katoliki Japan kwamba, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu nchini mwao itasaidia kutoa ujumbe kuhusu utu, maana ya maisha na jinsi ya kuumwilisha. Japan imeendelea kujielekeza katika ujenzi wa misingi ya amani na jirani zake. Japan ni nchi pekee ambayo wakati wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia iliweza kushambuliwa kwa mabomu ya atomiki.

Baraza la Maaskofu Katoliki Japan linaomba kwamba, kusiwepo tena duniani nchi ambayo inaweza inaweza kushambuliwa kwa makombora ya atomiki. Haya ni matamanio halali ya Baraza la Maaskofu Katoliki Japan, kuona kwamba, ulimwengu unaondokana na vitisho vya mashambulizi ya silaha za maangamizi. Wanamwomba Baba Mtakatifu Francisko asimame kidete kuiasa Jumuiya ya Kimataifa kuhusu madhara ya silaha za maangamizi. Pamoja na hayo yote, mwaka 2019 Japan inaadhimisha Jubilei ya Miaka 100 tangu Balozi wa kwanza wa Vatican alipotumwa rasmi nchini Japan. Maaskofu Katoliki Japan wanamwomba Mwenyezi Mungu ili awasaidie watu wa Mungu nchini Japan kuthamini Ukristo na Kanisa Katoliki, ili mahusiano na mafungamano baina ya pande hizi mbili, yasaidie kuchochea mchakato wa maendeleo fungamani kwa ajili ya Jumuiya ya Kimataifa.

Askofu Mkuu Takami
23 November 2019, 16:50