Tafuta

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Thailand inapania kuamsha ari na mwamko wa kimisionari kati ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo! Hija ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Thailand inapania kuamsha ari na mwamko wa kimisionari kati ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini humo! 

Hija ya Papa Francisko nchini Thailand: Moto wa kimisionari!

Hija hii, itasaidiaa kukoleza maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika: kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma kama kielelezo makini cha imani tendaji. Ni mwaliko wa kupyaisha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa wafu! Papa anataka kuwasha moto wa utume wa kimisionari Thailand.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko kuanzia tarehe 19-23 Novemba 2019 anafanya hija ya 32 ya kitume nchini Thailand inayoongozwa na kauli mbiu: “Mitume wa Kristo, Wamisionari Mitume”, kama sehemu ya  maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kwa utume wa Vikarieti ya Siam, kunako mwaka 1669. Baba Mtakatifu anatambua na kukiri utajiri mkubwa unaounda taifa la Thailand, ambalo limejishughulisha kikamilifu ili kuhakikisha kwamba, linajenga na kudumisha amani na utulivu, si tu kwa ajili ya wananchi wake, bali hata kwa Ukanda mzima wa Kusini Mashariki wa Bara la Asia. Anataka kuungana na waamini wa Kanisa Katoliki, ili kuwaimarisha katika imani, matumaini na mapendo sanjari na kuwatia shime, ili waendelee kuchangia katika ustawi, maendeleo na mafao ya jamii nzima. Ni matumaini yake kuwa, ataweza kuimarisha majadiliano ya kidini na kiekumene kwa kujikita katika ujenzi wa jamii himilivu na yenye utulivu utambulisho makini wa familia ya Mungu nchini Thailand.

Kwa upande wake, Askofu mkuu Paul Tshang In-nam, Balozi wa Vatican nchini Thailand, Birmania, Cambodia na Mwakilishi wa Kitume nchini Laos anasema,  hija hii ya kitume ni kielelezo makini cha mchakato wa uinjilishaji wa tamaduni na utamadunisho wa Injili, unaopania kuamsha, kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari miongoni mwa waamini wa Kanisa Katoliki nchini Thailand. Hija hii, itasaidiaa kukoleza maisha na utume wa Kanisa unaofumbatwa katika: kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu, Maisha ya Kisakramenti na Matendo ya huruma kama kielelezo makini cha imani tendaji. Ni mwaliko wa kupyaisha ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu aliyeteseka, akafa na kufufuka kwa wafu! Kwa muda mrefu tangu Mtakatifu Yohane Paulo II alipotembelea Thailand kunako mwaka 1984, Baraza la Maaskofu Katoliki Thailand, lilionesha tena nia kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro kutembelea tena nchini humo.

Askofu mkuu Paul Tshang In-nam anasema, mwanzoni mwa mwaka 2019, maandalizi ya awali yakaanza “kutimua vumbi” na sasa ndoto hii imetimia masikioni mwa watu wa Mungu nchini Thailand, matendo makuu ya Mungu. Familia ya Mungu katika ujumla wake nchini Thailand iko tayari kumpokea na kumkaribisha Baba Mtakatifu Francisko nchini mwao, kama kiongozi mkuu wa Kanisa Katoliki, rafiki wa maskini na wanyonge; mpenda haki, amani na mtetezi wa mazingira nyumba wote. Familia ya Mungu nchini Thailand inamwona Baba Mtakatifu Francisko kuwa ni mjumbe wa amani na matumaini kwa wale waliokata tamaa; chombo na shuhuda wa huruma ya Mungu. Waamini wa Kanisa Katoliki nchini Thailand ni 390, 000 sawa na asilimia 00.58% ya idadi ya wananchi wote wa Thailand. Mwaka 2019, Kanisa nchini Thailand linaadhimisha Jubilei ya Miaka 350 tangu kuanzishwa kisheria kwa Vikarieti ya Siam kunako mwaka 1669.

Hili ni tukio ambalo imeacha chapa ya kudumu katika historia na maisha ya Kanisa Katoliki nchini Thailand, ndiyo maana hata kauli mbiu ya hija ya Baba Mtakatifu Francisko inaongozwa na tukio hili adhimu. Jumuiya ya waamini wa Kanisa Katoliki nchini Thailand inaishi, inatangaza na kushuhudia imani yake katika Fumbo la Pasaka kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji unaokita mizizi yake katika ushuhuda. Kaskazini mwa Thailand, Kanisa bado linachechemea sana katika mchakato wa uinjilishaji unaopaswa kujielekeza zaidi katika majadiliano ya kidini; toba na wongofu wa ndani. Mjini Bankok, Kanisa linaendelea kustawi na kushamiri kama “mtende wa Lebanon”. Hiki ni kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa majadiliano ili kuwakutanisha watu, ili waweze kuheshimiana, kusaidiana na kufanya kazi katika umoja, upendo na mshikamano licha ya tofauti zao msingi. Thailand ni nchi ambayo ina ukarimu mkubwa na ni bandari salama kwa wananchi wanaotoka: China, Vietnam na Birmania na wengi wao ni waamini wa dini ya Kibudha.

Askofu mkuu Paul Tshang In-nam anaendelea kufafanua kwamba, Majimbo ya Chiang Rai na Chiang Mai ni moto wa kuotea mbali katika maisha na utume wa Kanisa. Waamini wa Majimbo haya wanatambua na kuthamini wito na utume wao kama waamini wa Kanisa Katoliki, wanaotumwa kwenda kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu, kama sehemu ya utambulisho wao wa Kikatoliki. Ni waamini ambao wanaendelea kuinjilisha tamaduni na kutamadunisha Injili kwa njia ya majadiliano ya kidini na kitamaduni; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja. Itakumbukwa kwamba, kunako tarehe 16 Mei 2018, Baba Mtakatifu Francisko alipata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wajumbe wa dini ya Kibudha kutoka Thailand. Kumbe, hija ya kitume ya Baba Mtakatifu Francisko nchini Thailand itaendeleza mchakato wa majadiliano ya kidini, ili kujenga na kudumisha jamii inayosimikwa katika tunu msingi za kiutu. Ni nafasi ya kuwaimarisha Wakristo katika imani, matumaini na mapendo, ili waweze kuwa tayari kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kumtangaza na kumshuhudia Kristo Yesu aliyeteswa, akafa na kufufuka kwa wafu.

Balozi: Thailand
19 November 2019, 14:19