Tafuta

Vatican News
Watanzania wanahimizwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, urithi walioachiwa na Baba wa Taifa Mwl. J.K. Nyerere. Watanzania wanahimizwa kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kitaifa, urithi walioachiwa na Baba wa Taifa Mwl. J.K. Nyerere. 

Watanzania dumisheni amani, umoja na mshikamano wa kitaifa!

Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu anasema na Askofu mkuu Rugambwa. AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hekima, umoja na amani ni ngao muhimu za watanzania mahali popote pale walipo ili kuweza kudumisha uhuru na umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, licha ya tofauti msingi zinazoweza kujitokeza. Haki, umoja na amani ni nyenzo msingi katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu. Kinzani, migogoro, vita na mipasuko ya kijamii inayojionesha sehemu mbali mbali za dunia ni changamoto kwa watanzania kusimama kidete kulinda na kudumisha umoja wa kitaifa na amani ambayo kimsingi ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu. Hayo yamebainishwa na Askofu mkuu Protase Rugambwa, Katibu wa Baraza la Kipapa la Uinjilishaji wa watu, Jumamosi, tarehe 16 Novemba 2019 wakati wa kuwakaribisha watanzania wapya waliofika mjini Roma kwa ajili ya masomo na utume wao katika kipindi cha mwaka 2019-2020. Askofu mkuu Protase Rugambwa, amewahimiza watanzania wanaoishi na kusoma Roma, kujenga na kudumisha: umoja, upendo na mshikamano wa kitaifa, mambo msingi yanayowatambulisha watanzania, licha ya tofauti zao msingi.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa unaotarajiwa kufanyika tarehe 24 Novemba 2019, usiwe ni sababu ya kuvuruga umoja na mshikamano wa kitaifa, lakini zaidi amani ambayo ni chachu ya maendeleo fungamani ya binadamu. Amani ikitoweka hata kile kidogo ambacho watanzania wamekihangaikia na kukitolea jasho, kitatoweka kama “ndoto ya mchana” haya ndiyo yanayojitokeza sehemu mbali mbali za dunia! Katika kipindi hiki tete, watanzania wawe makini zaidi, kwa kujikita katika umoja na mshikamano wa kitaifa, uzalendo, nidhamu pamoja na kutetea haki jamii, ili kujenga jamii inayoheshimu: utu wa binadamu, heshima, haki msingi, amani na maridhiano. Askofu mkuu Protase Rugambwa amewaambia watanzania wanaosoma na kufanya utume wao mjini Roma kwamba, kati ya mambo wanayopaswa kuzingatia ni wajibu, dhamana na majukumu waliyotumwa kuyatekeleza. Pili, wahakikishe kwamba, wanajitahidi kujenga na kudumisha umoja na mafungamano ya watanzania, ili kukabiliana na changamoto za kuishi na kusoma ughaibuni. Watekeleze wajibu huu kwa juhudi, maarifa na weledi, daima wakijiweka chini ya ulinzi na tunza ya Mwenyezi Mungu.

Kwa upande wake, Padre Walter Milandu, C.PP.S. ambaye ndiye aliyeongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kuwakaribisha watanzania wapya waliofika mjini Roma kwa kipindi hiki cha mwaka 2019-2020, aliwataka watanzania kujibidiisha zaidi katika kutafuta elimu na maarifa, ili waweze kuwa tayari kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu nchini Tanzania. Wajitahidi kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa Kanisa la Tanzania linaloendelea kujiimarisha na kukomaa, tayari kujibu changamoto mbali mbali zinazojitokeza katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu, ili kuwatangazia watanzania Injili ya matumaini. Kanisa la Tanzania halina budi kukazia ubora unaojikita katika ushuhuda wa imani kwa Kristo Yesu, aliyeteswa, akafa na kufufuka. Ni ushuhuda unaosimikwa katika tunu msingi za Kiinjili ili kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa liwe tayari kutangaza na kusimamia: utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Mwalimu Julius Kambarage Nyerere anakumbukwa na kuheshimiwa ndani na nje ya Tanzania kwa sababu alikazia: umoja wa kitaifa, utu, heshima na haki msingi za binadamu; akaijenga Tanzania yenye amani na kimbilio kwa nchi jirani. Huu ni wakati wa kujenga na kuimarisha imani, matumaini na mapendo miongoni mwa familia ya Mungu nchini Tanzania. Watanzania wafahamiane, waheshimiane na kusaidiana kama sehemu ya mchakato wa kukamilishana kwani hakuna mtu ambaye anaweza kujitosheleza kwa kila jambo. Zote hizi ziwe ni juhudi za ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Watanzania waipende na wawe wazalendo kwa nchi yao dhidi ya maadui wa ndani na nje ya nchi! Padre Walter Milandu, C.PP.S amemaliza utume aliokabidhiwa na Shirika la Wamisionari wa Damu Azizi ya Yesu kama Mshauri wa mkuu wa Shirika kwa kipindi cha Miaka sita na Padre mlezi wa maisha ya kiroho katika Seminari kuu ya Shirika, Kanda ya Italia.

Watanzania Roma
18 November 2019, 15:52