Tafuta

Vatican News
Kardinali John Onaiyekan ameng'atuka kutoka madarakani, Askofu mkuu mwandamizi Ignatius Ayau Kaigama ashika hatamu kuongoza Jimbo Kuu la Abuja, Nigeria. Kardinali John Onaiyekan ameng'atuka kutoka madarakani, Askofu mkuu mwandamizi Ignatius Ayau Kaigama ashika hatamu kuongoza Jimbo Kuu la Abuja, Nigeria. 

Kardinali Onaiyekan ang'atuka; Askofu mkuu Kaigama ashika hatamu

Askofu Mkuu Ignatius Ayau Kaigama alizaliwa mwaka 1958, akapewa Daraja takatifu ya Upadre tarehe 6 Juni 1981. Tarehe 3 Februari 1995 akateuliwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Jalingo, Nigeria na kuwekwa wakfu kama Askofu 23 Aprili 1995. Tarehe 14 Aprili 2000, akahamishiwa Jimbo Katoliki la Jos. Tarehe 11 Machi 2019, akateuliwa kuwa Askofu mkuu mwandamizi Jimbo Katoliki la Abuja.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko ameridhia ombi lililowasilishwa kwake na Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Abuja, nchini Nigeria la kung’atuka kutoka madarakani. Wakati huo huo, Baba Mtakatifu amemteua Askofu mkuu mwanadamizi Ignatius Ayau Kaigama kuwa Askofu mkuu mpya wa Jimbo Katoliki la Abuja. Askofu Mkuu Ignatius Ayau Kaigama alizaliwa tarehe 31 Julai 1958 huko Kona, Jimbo Katoliki la Jalingo nchini Nigeria. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, akapewa Daraja Takatifu ya Upadre tarehe 6 Juni 1981 na kuanza kuhudumia Jimbo Katoliki la Yola.

Mtakatifu Yohane Paulo II kunako tarehe 3 Februari 1995 akamteuwa kuwa Askofu wa kwanza wa Jimbo Jalingo, Nigeria na kuwekwa wakfu kama Askofu 23 Aprili 1995. Tarehe 14 Aprili 2000, Mtakatifu Yohane Paulo II akamhamishiwa Jimbo Katoliki la Jos, Nigeria ambako aliendelea kuwahudumia watu wa Mungu kwa kuwafundisha, kuwaongoza na kuwatakatifuza. Ilikuwa ni tarehe 11 Machi 2019, Baba Mtakatifu Francisko akamteuwa Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama kuwa Askofu mkuu mwandamizi wenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Abuja, Nigeria. Na ilipofika tarehe 9 Novemba 2019, Kardinali John Olorunfemi Onaiyekan akang’atuka kutoka madarakani na Askofu mkuu Ignatius Ayau Kaigama akashika usukani kwa ajili ya uongozi wa Jimbo kuu la Abuja, Nigeria.

Jimbo kuu Abuja
09 November 2019, 14:11