Tafuta

Vatican News
Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na mambo mengine wamechangia kuhusu dhambi za kiekolojia, utakatifu wa maisha na ushuhuda wa furaha ya Injili. Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia pamoja na mambo mengine wamechangia kuhusu dhambi za kiekolojia, utakatifu wa maisha na ushuhuda wa furaha ya Injili.  (AFP or licensors)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Dhambi za Kiekolojia!

Mada zilizojadiliwa: Umaskini wa hali na kipato; dhambi za kiekolojia; changamoto ya utakatifu wa maisha na wito wa kipadre; Uwajibikaji wa pamoja; haki msingi za binadamu; Mashemasi wa kudumu na umuhimu wa kuwahamasisha vijana kuwa watakatifu hata katika ujana wao. Mababa wa Sinodi wamemkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Serafim Fernandes de Araujo.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6-27 Oktoba, 2019 yanaongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Hii ni Sinodi inayoadhimishwa kwa kuzingatia mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana kwa sababu ni sehemu muhimu ya ekolojia fungamani. Mababa wa Sinodi wameendelea kuchangia hoja mbali mbali kama zilivyobainishwa kwenye Hati ya Kutendea Kazi, “Instrumentum Laboris”. Siku ya Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019, mada zilizojadiliwa ni pamoja na: Umaskini wa hali na kipato; dhambi za kiekolojia; changamoto ya utakatifu wa maisha na wito wa kipadre; Uwajibikaji wa pamoja; haki msingi za binadamu; Mashemasi wa kudumu Ukanda wa Amazonia pamoja na umuhimu wa kuwahamasisha vijana kuwa watakatifu hata katika ujana wao. Mababa wa Sinodi wamemkumbuka na kumwombea Marehemu Kardinali Serafim Fernandes de Araujo, Askofu mkuu mstaafu wa Jimbo Kuu la Belo Horizonte nchini Brazil, aliyefariki dunia Jumanne, tarehe 8 Oktoba 2019 akiwa na umri wa miaka 95.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kushiriki vikao hivi kwa kusikiliza maoni, ushauri na mang’amuzi yanayotolewa na Mababa wa Sinodi Umaskini wa hali na kipato wanasema Mababa wa Sinodi unaendelea kupekenya hata maisha ya kiroho ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Uhaba mkubwa wa Mapadre unaendelea kuwatumbukiza waamini katika umaskini wa maisha ya kiroho, kwa kukosa Neno la Mungu na Sakramenti za Kanisa, lakini zaidi Sakramenti ya Ekaristi Takatifu inayoboresha maisha ya waamini na kuwasukuma kuwa ni sadaka kwa ajili ya jirani zao, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kuna mapadre 45 katika Ukanda mzima wa Amazonia wanaohudumia wastani wa waamini 25, 000 kwa kila Padre. Mababa wa Sinodi wanaendelea kuwahamasisha waamini kusali kwa ajili ya kuombea miito mitakatifu pamoja na kuwataka vijana kujisadaka kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia furaha ya Injili.

Lakini, ikumbukwe kwamba, uhaba wa mapadre ni changamoto kwa Kanisa zima na wala si tu Ukanda wa Amazonia. Kanisa linawahitaji Mapadre watakatifu, wachapakazi na waadilifu wanaothubutu kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Kutopea kwa maisha ya kipadre na kitawa; ukosefu wa ushuhuda wa utakatifu wa maisha ni kati ya vikwazo vinavyoendelea kusababisha uhaba mkubwa wa mapadre na watawa ndani ya Kanisa. Hapa kuna haja ya kuwa na wongofu wa kichungaji na kimisionari, ili kufikiri na kutenda kama Kristo Mchungaji mwema. Vijana wavutwe kwa ushuhuda na harufu nzuri ya utakatifu wa maisha na wito wa Kipadre. Mababa wa Sinodi wamegusia pia umuhimu wa kuwaandaa Mashemasi wa kudumu, watakaosaidia kupyaisha maisha na utume wa Kanisa Ukanda wa Amazonia. Kumbe, hapa kuna haja ya kuunganisha nguvu, ili kupandikiza mbegu na ari ya kimisionari miongoni mwa watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia.

Juhudi hizi hazina budi kwenda sanjari na malezi pamoja na majiundo makini ya waamini walei, ili waweze kuwa ni chumvi ya dunia na nuru ya ulimwengu, tayari kuyatakatifuza malimwengu kwa uwepo na ushiriki wao mkamilifu katika maisha na utume wa Kanisa. Mababa wa Sinodi wamekazia pia umuhimu wa kuwawezesha wanawake ili waweze kuchangia kikamilifu katika utume wa Kanisa kwenye Ukanda wa Amazonia. Tafakari ya Neno la Mungu katika familia ni jambo ambalo limekaziwa na Mababa wa Sinodi. Haki msingi za binadamu; utu na heshima yake ni changamoto pevu kwa familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia. Viongozi na wale wote waliojitokeza kwa ajili ya kutetea haki msingi za binadamu Ukanda wa Amazonia, wengi wao wameuwawa kikatili, ili kuzima sauti na kilio cha maskini na wanyonge. Ulinzi na usalama wa raia na mali zao ni changamoto kubwa kwa wananchi wengi. Kuna baadhi ya viongozi wamekuwa wababe sana na hivyo kuendelea kuongoza kwa kutumia “mkono wa chuma”.

Katika muktadha huu, Kanisa haina budi kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu. Kanisa lazima liwe na ujasiri wa kupinga miradi mikubwa inayohatarisha, utu, heshima, ustawi na maendeleo ya wengi. Kanisa liendelee kuhamasisha mshikamano pamoja na kujizatiti katika utekelezaji wa haki jamii. Idadi ya wazalendo waliouwawa kwa sababu ya kutetea haki msingi, utu na heshima ya binadamu kuanzia mwaka 2003 hadi mwaka 2017 ni takribani watu 1, 119 katika Ukanda mzima wa Amazonia. Zaidi ya watu milioni moja, ambao ni asilimia 36% wameathirika vibaya kutokana na uchafuzi wa vyanzo vya maji pamoja na kugombania ardhi ya wazawa inayokwapuliwa na Makampuni makubwa makubwa. Idadi hii inaendelea kuongezeka kila kukicha. Haya ni matokeo ya ubinafsi, uchoyo, uchu wa mali na utajiri wa haraka haraka unaofumbatwa katika utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine.

Kuna haja wanasema Mababa wa Sinodi, kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu, Ukanda wa Amazonia. Mama Kanisa anapenda kushiriki kikamilifu katika mchakato wa maendeleo fungamani ya binadamu kama chachu na kikolezo cha maendeleo na wala si kama mtazamaji tu. Kanisa linataka kusoma alama za nyakati kwa kujikita katika hali halisi, ili kusikiliza na hatimaye, kujibu kilio cha Dunia Mama na kilio cha maskini; yaani “akina yakhe pangu pakavu tafadhali tia mchuzi”. Mababa wa Sinodi wanaendelea kuhimiza demokrasia na uchumi shirikishi, dhidi ya utamaduni wa kifo na utandawazi usiojali mahangaiko ya watu. Mababa wa Sinodi wameendelea kukazia umuhimu wa utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kwa sababu majanga ya moto, ufyekaji wa misitu na matumizi makubwa ya mazao ya msitu wa Amazonia ni hatari kwa ustawi na mafao ya wengi. Rasilimali na utajiri wa Ukanda wa Amazonia hauna budi kuendelezwa kwa ajili ya mafao ya wengi.

Katika mchakato wa kulinda, kutunza na kutetea haki msingi za wananchi wazawa, wamisionari wengi wamejikuta wakiuwawa kikatili. Hizi zote ni dhambi za kiekolojia zinazowataka watu kutubu na kuongokea ekolojia fungamani. Uharibifu mkubwa wa mazingira na ukosefu wa fursa za ajira ni chanzo kikuu cha wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji Ukanda wa Amazonia. Hili ni eneo ambalo: biashara na matumizi ya dawa za kulevya ni jambo la kawaida. Biashara ya binadamu na utumwa mamboleo ni mambo yanayopaswa kuvaliwa njuga kwa kuwashirikisha vijana katika maisha na utume wa Kanisa. Vijana waandaliwe ili waweze kushiriki pia katika masuala ya kisiasa, kiuchumi na kijamii. Ukanda wa Amazonia umebarikiwa kuwa na mifano bora ya watakatifu, wafiadini na waungama imani, changamoto na mwaliko wa wongofu wa kiekolojia, ili kuambata utakatifu wa maisha. Hii ni nguvu yenye mvuto mkubwa kwa vijana wa kizazi kipya, ambao kimsingi wamechoka na maneno tupu, sasa wanataka kuona vitendo.

Hawa ndio wale vijana wanaopambana pia biashara na matumizi haramu ya dawa za kulevya; utumwa mamboleo, vurugu na ghasia. Ushuhuda wa imani kwa Kristo na Kanisa lake ni muhimu sana kwa vijana wa kizazi kipya!

Sinodi: Majadiliano
09 October 2019, 16:00