Tafuta

Vatican News
Mababa wa Sinodi wamewachagua wajumbe 13 wa Baraza la Ushauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019 Mababa wa Sinodi wamewachagua wajumbe 13 wa Baraza la Ushauri wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019  (Vatican Media)

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Baraza la Washauri

Wahusika wakuu wa Sinodi hii ni familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko wamewachagua wajumbe 13 wa Baraza la Washauri kutoka Ukanda wa Amazonia watakaendeleza utekelezaji wa maazimio na mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kuanzia tarehe 6 -27 Oktoba, 2019 yameongozwa na Kauli mbiu: “Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ekolojia fungamani”. Mababa wa Sinodi wamepitia na kujadili na hatimaye kupitisha Hati ya Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Wahusika wakuu wa Sinodi hii ni familia ya Mungu Ukanda wa Amazonia. Mababa wa Sinodi kwa uwepo na ushiriki mkamilifu wa Baba Mtakatifu Francisko wamewachagua wajumbe 13 wa Baraza la Washauri kutoka Ukanda wa Amazonia watakaendeleza utekelezaji wa maazimio na mapendekezo yaliyotolewa na Mababa wa Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia kwa Mwaka 2019. Kardinali Cláudio Hummes, Mwezeshaji mkuu wa Maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, Ijumaa jioni tarehe 25 Oktoba 2019 amewasilisha Muswada wa Hati ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia, muhtasari wa kazi kubwa iliyotekelezwa na Tume ya Kuhariri Hati ya Sinodi.

Haya ni mawazo, tafakari, changamoto na mchango wa Mababa wa Sinodi kutoka katika Vikundi vidogo vidogo vinavyojulikana kama “Circoli Minori”. Muswada wa Hati hii umefanyiwa marekebisho, ili kuweza kusikiliza na hatimaye, kujibu kwa ufasaha kilio cha “Dunia Mama na Kilio cha Maskini Ukanda wa Amazonia”. Huu ni wakati wa kutenda kwani athari za mabadiliko ya tabianchi zinaendelea kusababisha maafa makubwa kwa watu na mali zao. Sinodi hii inataka kuwasha cheche za matumaini; kwa kujenga na kuimarisha umoja wa Kanisa la Kristo, kwa kuungana na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Jumamosi asubuhi, Mababa wa Sinodi wametumia fursa hii kwa ajili ya kujisomea na kufanya tafakari binafsi juu ya Hati ya Mababa wa Sinodi.

Itakumbukwa kwamba, Sinodi hii imetoa kipaumbele cha pekee kwa mambo makuu manne: Shughuli za Kichungaji, Kitamaduni, Kisiasa na Kiekolojia; mambo yanayo ambatana na kukamilishana. Mababa wa Sinodi wamepembua changamoto hizi kwa kutumia jicho ya Mitume wa Yesu mintarafu: wongofu wa shughuli za kichungaji, kimisionari na kiekolojia. Mababa wa Sinodi wamekazia kuhusu majadiliano ya kidini, kiekumene na kitamaduni kama sehemu muhimu sana ya vinasaba vya maisha na utume wa Kanisa. Kwa njia ya maadhimisho ya Sinodi, Kanisa limekuwa likitembea kwa pamoja, “Kairos”, ili kujipatanisha na Ukanda wa Amazonia sanjari na kuendelea kujikita katika mchakato wa kuziinjilisha tamaduni ili kuitamadunisha Injili; kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi kama sehemu ya mchakato wa ekolojia fungamani.

Sinodi: Washauri

 

26 October 2019, 11:36