Tafuta

Caritas Romana kwa mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwake na Don Luigi Di Liegro kunako mwaka 1979. Caritas Romana kwa mwaka 2019 inaadhimisha Kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwake na Don Luigi Di Liegro kunako mwaka 1979. 

Caritas Romana: Miaka 40 ya Utume kwa Maskini wa Roma!

Jimbo kuu la Roma linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Msaada la Caritas Romana na Don Luigi di Liegro kunako mwaka 1979 na baada ya huduma kwa maskini, akafariki dunia tarehe 12 Oktoba 1997. Katika maisha yake, alisimama kidete kuomba nafasi na haki kwa maskini waliokuwa wanyanyasika utu na heshima yao mjini Roma. Injili ya upendo!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, maskini ni amana na utajiri wa Kanisa. Hawa ni walengwa wa kwanza wa mchakato mzima wa uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili. Umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika utangazaji na ushuhuda wa Injili ya upendo kwa watu wa Mataifa. Mambo yanayopaswa kuzingatiwa ni: Ufahamu wa Neno la Mungu; umuhimu wa toba na wongofu wa ndani sanjari na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo ya huruma: kiroho na kimwili. Kanisa linapaswa kuwa ni kielelezo cha utandawazi wa mshikamano na katika maisha ya kiroho dhidi ya sera na mikakati ya kiuchumi inayowatenga na kuwanyanyasa maskini; na kwamba, kwa sasa tofauti kati ya watu inakuwa ni chanzo cha kinzani, uhasama na vita. Lakini, ikumbukwe kwamba, dunia inahitaji wajenzi wa madaraja ya kuwakutanisha watu, kwa kujikita katika majadiliano yanayofumbatwa katika ukweli na uwazi.

Huu ni mwaliko wa toba na wongofu wa ndani, ili kuwa na Uso wa huruma; wajenzi na vyombo vya amani duniani; manabii wa huruma na wasamaria wema wanaothubutu kuwahudumia maskini kwa ari na moyo mkuu, kwa kutambua kwamba, Kanisa ni Sakramenti ya umoja wa binadamu, kati ya watu wa mataifa, familia na tamaduni zao. Ni katika muktadha huu, Jimbo kuu la Roma linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu kuanzishwa kwa Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Roma, Caritas Romana na Don Luigi di Liegro kunako mwaka 1979 na baada ya huduma kwa maskini, akafariki dunia tarehe 12 Oktoba 1997. Katika maisha yake, alisimama kidete kuomba nafasi na haki kwa maskini waliokuwa wanyanyasika utu na heshima yao mjini Roma. Kardinali Angelo De Donatis, Makamu Askofu Jimbo kuu la Roma hivi karibuni ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Yohane wa Lateran, kama sehemu ya kumbu kumbu ya Miaka 40 tangu Caritas Romana ilipoanzishwa.

Kardinali Angelo De Donatis amelitaka Jimbo kuu la Roma kutoa kipaumbele cha kwanza kwa maskini, kwa kuwasikiliza na kuwashirikisha katika maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa. Hii ni changamoto kwa waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuendelea kugundua mifumo mipya umaskini katika ulimwengu mamboleo. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kuwa ni chumvi ya dunia na mwanga wa Mataifa. Chachu ya huduma ya upendo ipate chimbuko lake ndani ya: familia na Jumuiya za Kikristo. Hakuna huduma mbadala ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Kwa upande wake, Padre Benoni Ambarus, Mkurugenzi mkuu wa Shirika la Msaada la Kanisa Katoliki Jimbo Kuu la Roma, Caritas Romana amewashukuru watu wa kujitolea pamoja na Parokia 337 zinazoendelea kutoka huduma kwa maskini na wahitaji zaidi. Kuna hosteli 52 zinazotoa huduma ya chakula na malazi kwa maskini; wakimbizi na wahamiaji; wagonjwa na watu wasiokuwa na makazi maalum.

Kuna watu wanaoelemewa na upweke hasi, kumbe, kwanza kabisa wanapaswa kusikilizwa kwa makini; kupewa chakula, malazi na huduma ya afya. Wazee na wagonjwa wa muda mrefu wanapaswa kuhudumia kikamilifu. Caritas Romana inataka kuendelea kujizatiti katika huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, kwa sababu wao ni shule makini ya huruma na upendo wa Mungu. Baba Mtakatifu Francisko anawaalika Wakristo pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kujifunza kutoka kwenye shuleni ya maskini na watu wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. Hawa ni watu wa kawaida wanaopaswa kuonjeshwa upendo na kuthamini utu wao. Kati ya maskini na watu wasiokuwa na makazi maalum, humu humo kuna watakatifu na watu ambao wanaweza kuwafundisha wengine tunu msingi za maisha ya kijamii, kiutu na kiroho. Wasanii wasaidie kuhamaisha tunu msingi za maisha  kama vile: upendo kwa Mungu na jirani; umoja na mshikamano wa kidugu.

Baba Mtakatifu anapenda kuwahakikishia maskini na wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii kwamba, wao “si mzigo wa kutwishwa Wanyamwezi” bali ni shule makini kwa vijana wa kizazi kipya kuhusu umuhimu wa kusimama kidete kulinda na kutetea ustawi na mafao ya wengi. Maskini ni kielelezo cha Kristo kati ya watu wake. Jimbo kuu la Roma limekuwa ni kielelezo cha upendo na mshikamano kati ya watu. Hapa Kanisa linajivunia kuwa na viongozi ambao wamejisadaka kwa ajili ya huduma kwa maskini, daima wakitenda kama Wasamaria wema kama ilivyokuwa kwa Mtakatifu Laurenti, Shemasi na shahidi pamoja na Padre Luigi Di Liegro, muasisi wa Shirika la msaada  Roma, Caritas Romana bila kuwasahau watu wanaoendelea kujisadaka kwa ajili ya kuwahudumia maskini ndani na nje ya Roma. Katika shule ya upendo, watu wanatafuta faraja, mahusiano, utu na  heshima ya binadamu na kwa njia hii, waamini wanaweza kujifunza kutoka kwa maskini kwa kuwakaribisha, kuwasikiliza, kuwakirimia na kuwahudumia kwa upendo na nidhamu ya hali ya juu.

Caritas Romana
22 October 2019, 14:46