Tafuta

Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane XXIII, Mwanzo wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican. Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba anaadhimisha Kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane XXIII, Mwanzo wa Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa II wa Vatican. 

Mt. Yohane XXIII: Mtetezi wa haki, amani & Mwana diplomasia makini!

Mtakatifu Yohane wa XXIII katika maisha na utume wake, alikuwa ni mwanadiplomasia aliyejipambanua kwa kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Alikuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Bulgaria na Uturuki ambako alitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican. Kanisa linamkumbuka kila mwaka tarehe 11 Oktoba.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mtakatifu Yohane wa XXIII ambaye hapo mwanzoni alijulikana kama Angelo Giuseppe Roncalli alizaliwa tarehe 25 Novemba 1881 na kufariki dunia kunako tarehe 3 Juni 1963. Alibahatika kuliongoza Kanisa Katoliki kuanzia alikuwa tarehe 28 Oktoba 1958 hadi kifo chake. Alikuwa ni mtu mwema na mwenye mvuto kwa waru! Alitangazwa na Mtakatifu Yohane Paulo II kuwa Mwenyeheri tarehe 3 Septemba 200° wakati wa maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 2000 ya Ukristo. Ni kiongozi aliyethubutu kuitisha Mtaguo Mkuu wa Pili wa Vatican kuanzia mwaka 1962 hadi mwaka 1965, ili kulipyaisha Kanisa la Kristo kwa kusoma alama za nyakati. Mama Kanisa anamkumbuka kila mwaka ifikapo tarehe 11 Oktoba, siku ambapo Kanisa lilizindua rasmi Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican. Katika maisha na utume wake, alikuwa ni mwanadiplomasia aliyejipambanua kwa kulinda na kutetea misingi ya haki, amani, ustawi na maendeleo fungamani ya binadamu. Alikuwa ni chombo cha majadiliano ya kidini na kiekumene nchini Bulgaria na Uturuki ambako alitekeleza utume wake kama Balozi wa Vatican.

Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia, Alhamisi, tarehe 10 oktoba 2019 ameadhimisha Ibada ya Misa Takatifu kama kumbu kumbu ya Mtakatifu Yohane XXIII, Msimamizi na mlinzi wa vikosi vya ulinzi na usalama nchini Italia. Amewakumbusha wanajeshi kwamba, wito wao unawawezesha kuwa ni wafanyakazi wa Serikali, wahudumu wa jirani zao na wasimamizi na walinzi wa amani. Hii ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo. Katika mahubiri yake, amewakumbuka wakimbizi na wahamiaji wanaolazimika kutafuta: hifadhi, usalama na maisha bora zaidi kutokana na vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii. Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama sehemu mbali mbali za dunia, wanao wajibu wa kusimamia haki na amani; utawala wa sheria; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Ni wajibu na dhamana nyeti ya kusimama kidete kulinda na kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo; daima utu na heshima ya binadamu vikipewa kipaumbele cha kwanza.

Askofu mkuu Santo Marcianò anafafanua kwamba, vita, kinzani na migogoro ya kitaifa na kimataifa viwawezeshe kutambua umuhimu wa Serikali kusimamiwa utawala bora unaojikita katika sheria, ili kujenga na kudumisha umoja na udugu wa kibinadamu, mafao ya wengi yakipewa msukumo wa pekee, ili kujenga umoja wa familia ya binadamu. Vikosi vya ulinzi na usalama nchini Italia vinapaswa kujielekeza zaidi kama vyombo vya kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu; umoja, upendo na mshikamano wa dhati ni mambo msingi katika huduma ya Kanisa kwa ajili ya vikosi vya ulinzi na usalama. Papa Yohane wa XXIII na Papa Yohane Paulo II walitangazwa kuwa watakatifu, wakati Mama Kanisa alipokuwa anaadhimisha Jubilee ya Miaka 50 ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican sanjari na Mwaka wa Imani uliotangazwa na kuzinduliwa na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI na kufungwa rasmi na Papa Francisko.

Papa Roncali ni kiongozi ambaye hakuwa na wasi wasi katika hija ya maisha ya imani, daima alionesha amani na utulivu wa ndani. Akiwa Padre kijana kabisa aliwahi kusema kwamba, amana kubwa ambayo anaihifadhi katika undani wa moyo wake ni imani, aliyorithi kutoka kwa wazazi wake! Hii ndiyo imani ambayo alisimama kidete kuilinda, kuitetea na kuwamegea wengine katika maisha yake kama Padre, Askofu na Khalifa wa Mtakatifu Petro. Ni imani iliyomuunganisha na Kristo Yesu pamoja na Kanisa lake, kiasi cha kumsukuma kuwashirikisha wengine, tangu alipokuwa mtumishi wa Altareni Parokiani mwake, mchakato ambao ameuendeleza kwa ari na moyo mkuu kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Hii ndiyo imani iliyomsukuma kuwa na ujasiri wa kutangaza na hatimaye, kuadhimisha Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, hapo tarehe 11 Oktoba 1962. Hapa Familia ya Mungu ikasimama na kuungama imani kwa Kanisa moja, takatifu, katoliki na la mitume!

Huu ni urithi mkubwa ambao Papa Yohane wa XXIII ameliachia Kanisa la Kristo. Hii ndiyo imani inayowaimarisha waamini hata kujitosa kimaso maso kupambana na changamoto za maisha kwa ujasiri na umakini mkubwa! Alisikika daima akisema kwamba, mtu mwenye imani thabiti kamwe hawezi kutetereka! Nabii Isaya anasema, kwa ajili ya hayo Bwana, Mungu, asema hivi, ”Tazama, naweka jiwe katika Sayuni, liwe msingi, jiwe linalojaribiwa, jiwe la pembeni lenye thamani, msingi ulio imara: yeye aaminiye hatafanya haraka. Isaya 28: 16. Mtakatifu Yohane wa XXIII alikuwa ni kiongozi mwenye unyenyekevu mkubwa, fadhila ambayo iliongoza maisha na huduma yake kwa Kanisa kama Khalifa wa Mtakatifu Petro. Maadhimisho ya Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican ni kumbu kumbu endelevu ya unyenyekevu na huduma makini iliyotolewa na Papa Yohane wa XXIII katika maisha na utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Askofu mkuu Santo Marcianò, wa Jimbo la Kijeshi nchini Italia, hivi karibuni alitabaruku Kanisa la Shama, huko nchini Lebanon na kuliweka chini ya ulinzi na tunza ya Mtakatifu Yohane XXIII na Mtakatifu Decor Carmel. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko katika ujumbe ulioandikwa kwa niaba yake na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, aliwashukuru wale wote waliojitoa na kujisadaka bila ya kujibakiza ili kukamilisha ujenzi wa Kanisa hili, mahali pa Ibada na Sala panapowawezesha waamini kukutana na Mwenyezi Mungu katika undani wa maisha yao. Baba Mtakatifu alisema ni kwa njia ya ushuhuda wa maisha yenye mvuto na mashiko, wanaweza pia kuwa kweli ni mashuhuda wa amani na udugu. Baba Mtakatifu amewahakikishia uwepo wake wa karibu kwa njia ya sala na sadaka yake pamoja na kuwapatia baraka zake za kitume! Kwa upande wake, Askofu mkuu Santo Marcianò, alisema, hili ni Kanisa litakalotumiwa na wanajeshi Wakatoliki kwa ajili ya sala na ibada wanapotekeleza utume wao wa kulinda na kudumisha amani huko Lebanon, lakini pia litaweza kutumiwa na watu wote wenye mapenzi mema.

Hapa ni mahali pa kukuza na kudumisha umoja na udugu unaofumbatwa katika majadiliano ya kidini na kiekumene; kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu nchini Lebanon. Wanajeshi wa vikosi vya ulinzi na usalama kutoka sehemu mbali mbali za dunia, watapata nafasi ya kusali, ili kuendelea na utume wao wa kulinda: usalama, amani na maridhiano kati ya watu. Mtakatifu Yohane XXIII katika Waraka wake wa kitume, “Pacem in terris” yaani “Amani Duniani” ulioachapishwa kunako tarehe 11 Aprili 1963 anakazaia: ukweli, haki, upendo na uhuru wa watu wa Mungu. Huu ndio wajibu unaopaswa kutekelezwa na vikosi vya ulinzi na usalama huko Mashariki ya Kati. Changamoto zinazoendelea kujitokeza katika ulimwengu mamboleo kiasi cha kutishia: haki, amani na maridhiano kati ya watu ni pamoja na: vitendo vya kigaidi, ukosefu wa haki msingi za binadamu; uhuru wa kuabudu, uhalifu pamoja na misimamo mikali ya kidini inayopandikiza hofu na utamaduni wa kifo! Mtakatifu Yohane XXIII, katika maisha na utume wake, aliwahi kuwa Padre wa maisha ya kiroho kwa wanajeshi pamoja na kuwa ni Balozi wa Vatican huko Mashariki ya Kati. Hii ni changamoto ya kujenga na kudumisha msingi ya haki, amani na upatanisho kati ya watu wa Mataifa.

Mt. Yohane XXIII

 

11 October 2019, 15:27