Tafuta

Kardinali Mauro Piacenza: Sherehe ya Watakatifu wote na Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu ni Kipindi cha kujichotea rehema kutoka katika hazina ya Mama Kanisa. Kardinali Mauro Piacenza: Sherehe ya Watakatifu wote na Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu ni Kipindi cha kujichotea rehema kutoka katika hazina ya Mama Kanisa. 

Sherehe ya Watakatifu na Marehemu Wote: Kipindi cha Rehema!

Waamini wanaalikwa kuzama zaidi katika ushirika wa: Imani, Sakramenti, Karama na Mapendo mambo ambayo ndilo chimbuko la rehema inayotolewa na Kanisa. Ushirika huu ushuhudiwe katika maadhimisho ya Ekaristi Takatifu, katika Sala, Toba na Wongofu na unaonekana katika sadaka na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha wokovu ulioletwa na Kristo Yesu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Sherehe ya Watakatifu wote inawaunganisha waamini na watakatifu wote walioandikwa kwenye orodha ya watakatifu wa Kanisa na wale ambao bado hawajaandikwa. Hawa ni wale wenye haki. Hawa ni jirani, ndugu na jamaa zao, ambao kimsingi wanaunda umati mkubwa wa watu wanaomtukuza na kumsifu Mwenyezi Mungu. Ni katika mukatadha huu, anasema Baba Mtakatifu Francisko hii ni Sherehe ya Familia. Watakatifu ni watu ambao wako karibu nao na ni ndugu zao wa kweli; wanaowafahamu na kuwapenda; wanaotambua mahitaji yao msingi; wanaowasaidia na kuwasubiri kwa mikono miwili; huku wakiwa na furaha ya kutaka kukutana nao huko Paradiso! Baba Mtakatifu anawaalika waamini na watu wote wenye mapenzi mema kuambata “Heri za Mlimani”: Muhtasari wa Mafundisho makuu ya Kristo Yesu, chemchemi ya umaskini wa roho, rehema na moyo safi. Njia ya Heri za Mlimani na Hija ya Utakatifu wa maisha, zinaonekana kana kwamba, hazina nguvu tena “eti zimepitwa na wakati” kwani watu wamekengeuka na wanapenda kutopea katika dhambi!

Lakini, Neno la Mungu linakaza kusema, watakatifu wamevikwa mavazi meupe na wana matawi ya mitende mikononi mwao, alama ya ushindi dhidi ya malimwengu, kwani wameamua kumchagua Mungu ambaye ni Mtakatifu na utakatifu ni mwaliko wa kwanza kwa watu wote! Siku kuu hii iamshe ndani ya waamini ari na mwamko wa kutaka kuchuchumilia na kuambata utakatifu wa maisha unaofumbatwa katika toba na wongofu wa ndani. Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote pamoja na Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu wote, inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 2 Novemba, anawaalika waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kulitafakari kwa kina Fumbo la Kanisa na ni nani Kanisa? Kanisa lina asilia ya Kimungu kwa sababu limeanzishwa na Kristo Yesu, Nafsi ya Pili ya Fumbo la Utatu Mtakatifu na kwa jinsi hii linakita mizizi yake katika Fumbo la Utatu Mtakatifu “Ecclesia de Trinitate”.

Kristo Yesu ndiye kichwa cha mwili wa Fumbo wa Kristo yaani Kanisa linalowafumbata na kuwakumbatia wale ambao bado wako safarini hapa duniani na wale ambao wamekwisha kutangulia mbele ya haki, wakiwa na tumaini la maisha na uzima wa milele. Maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu wote, katika sala, tafakari binafsi na maadhimisho ya Ibada ya Misa Takatifu, waamini wanaalikwa kuzama zaidi katika ushirika wa: Imani, Sakramenti, Karama na Mapendo mambo ambayo ndilo chimbuko la rehema inayotolewa na Mama Kanisa. Ushirika huu unapaswa kujionesha katika ushiriki mkamilifu wa maadhimisho ya Fumbo la Ekaristi Takatifu, katika Sala, Toba na Wongofu wa ndani unaomwilishwa katika sadaka sanjari na matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama kielelezo makini cha wokovu ulioletwa na Kristo Yesu. Huu ni mwaliko kwa waamini kukumbatia neema inayokita mizizi yake katika uhuru binafsi, kazi ya Fumbo la Utatu Mtakatifu inayojidhihirisha katika kazi ya uumbaji iliyotekelezwa na Mungu Baba, Kazi ya Ukombozi iliyofanywa na Kristo Yesu na Roho Mtakatifu anaendelea kulitakatifuza Kanisa. Wote wanahimizwa kujenga ushirika na Kristo Yesu.

Ikumbukwe kwamba, Rehema ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu ambao kosa lake lilikwishwafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini aliyejiweka vizuri huupata  kutoka katika hazina ya malipizi ya Kristo na ya Watakatifu. Rehema inaweza kuwa ya Muda au Kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (Rej. KKK, 1472). Mkristo huweza kupata rehema kamili kwa ajili yake yeye mwenyewe au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza yafuatayo. Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa, pili apokee Sakramenti ya Upatanisho (Kitubio), tatu, Apokee Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili, nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu na tano atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa Rehema Kamili. Kardinali Mauro Piacenza anawaalika waamini kujichotea rehema na neema kutoka katika hazina ya huruma na upendo wa Kanisa, kwa kuomba rehema kwa ajili yao binafsi na kwa ajili ya waamini marehemu, waliotangulia mbele za haki, wakiwa na imani na tumaini la ufufuko na uzima wa milele.

Huu ni mwaliko kwa waamini kupyaisha maisha yao ya kiroho kwa kujipatanisha na Mungu pamoja na jirani zao kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho sanjari na kutekeleza masharti kwa ajili ya kupata Rehema Kamili. Kwa njia ya matendo haya adilifu na matakatifu, mwamini anaweza kujichotea neema na baraka zinazotolewa na Mama Kanisa katika hazina yake ya maisha ya kiroho. Katika hali ya unyenyekevu na moyo wa Ibada, hata yale matendo ya kibinadamu, yanasaidia kupyaisha na kuimarisha imani. Kupiga magoti, kuchunguza dhamiri, kuungama na hatimaye kulipiza malipizi ni matendo yanayo imarisha imani na uhuru wa ndani. Katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote na Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu Wote, iwe ni fursa ya kukimbilia huruma na upendo wa Mungu kwa njia ya Sakramenti ya Upatanisho. Katika kipindi hiki cha sala, toba na wongofu wa ndani, waamini wajenge na kudumisha moyo wa upendo na ukarimu kwa maskini na wahitaji zaidi, ili kuimarisha ushirika wa upendo na wale wote waliotangulia mbele ya haki!

Kardinali Piacenza anaendelea kukazia umuhimu wa ushirika wa mapendo “Sanctorum communio”, kwani katika ushirika wa watakatifu hakuna mtu aishiye kwa nafsi yake, wala afaye kwa nafsi yake. Matendo yanayotekelezwa kwa upendo yana maana kubwa sana katika maisha ya waamini. Upendo hautafuti mambo yake, kila tendo ambalo limefanywa katika upendo, huleta faida kwa wote katika mshikamano huu na watu wote walio hai au waliokufa, ambao una msingi wake katika ushirika wa watakatifu. Mapadre waungamishaji katika kipindi hiki ambacho waamini wanajichotea neema na rehema, wajenge ari na moyo wa kusikiliza kwa makini, bila kuwa na papara; wawasaidie waamini kwa ushauri na malipizi ya dhambi zao, ili kusaidia mchakato wa kupyaisha maisha ya kiroho, ili rehema na neema zinazobubujika kutoka katika hazina ya Mama Kanisa ziweze kuwafikia watoto wake! Sakramenti ya Upatanisho iwe ni chemchemi ya faraja, ari na moyo wa kusonga mbele kwa bidii. Ni mahali pa kufuta machozi kwa njia ya: upendo, huruma na msamaha wa dhambi.

Waamini watambue kwamba, hapa duniani ni wapita njia tu, matendo ya huruma: kiroho na kimwili yawasaidie kujiwekea hazina mbinguni. Mapadre waungamishaji wakite huduma hii katika kusikiliza, kufariji na hatimaye, kuwaongoza watu wa Mungu katika hija ya utakatifu wa maisha kwa njia ya msamaha wa dhambi! Mwezi Novemba, uwe ni chemchemi ya upyaisho wa maisha ya kiroho, kwa kugundua tena hazina ya imani inayomwilishwa katika matendo ya kila siku, ili kupokea neema ya Roho Mtakatifu inayotolewa na Mama Kanisa katika kipindi hiki. Kwa hakika matendo ya huruma: kiroho na kimwili, yatazaa matunda mengi katika maisha na utume wa Kanisa; kwa mtu binafsi na hasa kwa ajili ya ustawi na mafao ya watu wote wa Mungu.

Kardinali Mauro Piacenza, Mhudumu mkuu wa Toba ya Kitume anahitimisha ujumbe wake katika maadhimisho ya Sherehe ya Watakatifu wote pamoja na Kumbu kumbu ya Waamini Marehemu wote kwa kuwaweka waamini na watu wote wenye mapenzi mema chini ya ulinzi na tunza ya Bikira Maria Malkia wa Watakatifu wote, Mlango wa mbingu, msaada wa wale wanaoteseka. Bikira Maria chombo cha neema na mwombezi wa wale wanaokimbilia huruma ya Mungu, awaombee na kuwasindikiza wale wote ambao wako njiani kuelekea mbinguni, ili furaha yao, iweze kuwa pia ni furaha ya waamini ambao bado wako huku bondeni kwenye machozi!

Watakatifu Wote
31 October 2019, 11:11