Tafuta

Vatican News
Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni Mlango wa Majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu. Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni Mlango wa Majadiliano ya kidini ili kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mungu.  (AFP or licensors)

Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni Mlango wa Majadiliano ya Kidini!

Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii. AMANI!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu, iliyotiwa saini kati ya Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, ulioko mjini Kairo, nchini Misri, tarehe 4 Februari  2019 huko Abu Dhabi, Umoja wa Falme za Kiarabu, ni mwaliko na changamoto kwa waamini wa dini mbali mbali duniani, kuungana na kushikamana, ili kufanya kazi katika umoja na udugu, ili kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Hati hii ni nguzo msingi ya haki, amani na upatanisho. Hati inakazia pamoja na mambo mengine kwamba: binadamu wote wameumbwa kwa sura na mfano wa Mwenyezi Mungu; wanatakiwa kusimama kidete kulinda, kutunza na kudumisha: uhai wa binadamu, mazingira nyumba ya wote, sanjari na kushikamana na maskini pamoja na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inapata chimbuko lake katika mikutano elekezi iliyowasaidia waamini wa dini hizi mbili kushirikishana: furaha, majonzi, matamanio yao halali pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kumwandama mwanadamu!  Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot, Rais wa Baraza la Kipapa la Majadiliano ya Kidini, katika hotuba yake elekezi, hapo Alhamisi, tarehe 17 Oktoba 2019, katika mkutano ulioandaliwa na Chuo Kikuu cha LUMSA, kilichoko mjini Roma kama sehemu ya tafakari ya Hati hii muhimu inayoendelea kufanyiwa kazi katika ngazi mbali mbali za Jumuiya ya Kimataifa anasema, kwa hakika Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni “dirisha wazi kwa ajili ya mchakato wa majadiliano ya kidini” miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali duniani.

Ni hati inayowahamasisha waamini kushikamana na kutembea bega kwa bega katika udugu wa kibinadamu; kwa kujikita katika misingi ya haki na amani; utulivu na maridhiano. Mkutano huu, umehudhuriwa na viongozi wa Chuo Kikuu cha LUMSA, wanafunzi pamoja na wataalam wa majadiliano ya kidini kati ya Kanisa Katoliki na Waamini wa Dini ya Kiislam. Baadhi ya wanafunzi wanaotoka katika nchi za Kiislam wanaosoma mjini Roma, wameshirikisha pia ushuhuda wa mchakato wa ujenzi wa udugu wa kibinadamu, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot amefafanua zaidi kwa kusema kwamba, Hati ya Udugu wa Kibinadamu ni changamoto na mwelekeo mpya katika masuala ya kijamii. Ni mchakato ambao umeanzishwa na kwa sasa unaishirikisha familia kubwa ya binadamu.

Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawaalika: Viongozi wa kidini; viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa; Watunga sera; Wachumi wa Kitaifa na Kimataifa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kushirikiana na kushikamana katika ujenzi wa utamaduni wa maridhiano, haki na amani, ili hatimaye, kusitisha vita, kinzani na umwagaji wa damu ya watu wasiokuwa na hatia. Baba Mtakatifu Francisko tangu mwanzo wa utume wake kama Khalifa wa Mtakatifu Petro ameendelea kujipambanua katika majadiliano ya kidini kwa kukazia: ukweli na uwazi; utu, heshima na haki msingi za binadamu, ili kukuza na kudumisha urafiki. Umefika wakati wa kugundua tena tunu msingi zinazofumbatwa katika amani, haki, wema, uzuri, udugu wa kibinadamu, upendo na mshikamano. Huu ni mwamba salama wa wokovu kwa watu wote; mambo yanayopaswa kumwilishwa katika uhalisia wa maisha ya watu.

Kardinali Miguel Angel Ayuso Guixot anahitimisha kwa kusema, mchakato wa kujenga na kudumisha udugu wa kibinadamu ni hatua muhimu sana ya ujenzi wa misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu wa Mataifa na ni kikolezo kikubwa cha maendeleo fungamani ya binadamu!

Majadiliano ya Kidini

 

23 October 2019, 16:30