Tafuta

Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti, Mkurugenzi Mkuu Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti, Mkurugenzi Mkuu Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. 

Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti, Kamanda wa Usalama Vatican!

Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti alizaliwa mwaka 1973 huko Gubbio, Perugia, nchini Italia. Ana shahada ya uzamivu katika sekta ya uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha “La Sapienza”, Roma. Alijiunga na Vatican kunako mwaka 1995. Tangu wakati huo, akapewa dhamana ya kuanzisha mfumo wa ulinzi na usalama kwa njia ya teknolojia pamoja na kujikita katika masuala ya usalama wa kimtandao.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko amemteua Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti kuwa Mkurugenzi mkuu wa Huduma ya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Wakati huo huo atakuwa ni Kamanda Mkuu wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican, hadi kuteuliwa kwake, alikuwa ni Kaimu Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican. Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti alizaliwa tarehe 3 Juni 1973 huko Gubbio, Perugia, nchini Italia. Katika masomo yake, akafanikiwa kujipatia shahada ya uzamivu katika sekta ya uhandisi kutoka Chuo Kikuu cha “La Sapienza” kilichoko mjini Roma Ameoa na kubahatika kupata watoto wawili. Alijiunga na Vikosi vya Ulinzi na Usalama vya Vatican kunako mwaka 1995. Tangu wakati huo, akapewa dhamana ya kuanzisha mfumo wa ulinzi na usalama kwa njia ya teknolojia pamoja na kujikita katika masuala ya usalama wa kimtandao. Kunako mwaka 2010 akahamishiwa kwenye Kituo Kikuu cha Usalama. Hatua kwa hatua, akapewa dhamana na majukumu hadi kufikia mwaka 2017 akawapandishwa cheo na kuwa ni Kaimu Mkurugenzi Mkuu na hatimaye kunako mwaka 2018 kuwa Kaimu Kamanda wa Vikosi vya Ulinzi na Usalama mjini Vatican.

Katika maisha na utume wake, ameendelea kujipambanua kuwa ni kiongozi mwaminifu na mwadilifu; mwenye uwezo wa kujenga na kudumisha mahusiano na mafungamano na Sekretarieti mbali mbali zinazomsaidia Baba Mtakatifu kutekeleza dhamana na utume wake. Dr. Gianluca Gauzzi Broccoletti ana mahusiano mazuri na Sekretarieti kuu pamoja na uongozi mzima wa mjini wa Vatican. Ni kiongozi anayetekeleza dhamana na wajibu wake kwa weledi, uadilifu na nidhamu ya hali ya juu kabisa. Amekuwa bega kwa bega na Baba Mtakatifu Francisko katika hija zake za kitume kimataifa pamoja na safari za kichungaji ndani ya Italia. Ni kiongozi aliyekuwa anaratibu ulinzi na usalama wa Mtakatifu Yohane Paulo II na Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI, kwenye Ikulu Ndogo ya Castel Gandolfu kwa wakati huo, kwa sasa imegeuzwa kuwa ni Jumba la Makumbusho.

Ni kiongozi aliyesimamia na kuratibu ulinzi na usalama wakati wa maadhimisho ya Baraza la Makardinali katika kipindi cha uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro kwa Mwaka 2005 na Mwaka 2013. Kimsingi ni kiongozi anayeifahamu vyema kazi yake kutokana na uzoefu wa muda mrefu pamoja na kuiwakilisha Vatican kwa matukio makuu yanayohusisha moja kwa moja uwepo wa Baba Mtakatifu. Katika kipindi cha miaka hii yote, ameendelea kujinoa kwa masuala ya ulinzi na usalama ndani na nje ya Italia, sasa amepewa dhamana nyeti na Baba Mtakatifu Francisko!

Kamanda
16 October 2019, 15:02