Tafuta

Vatican News
Waamini wanahimizwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari kama sehemu ya mbinu mkakati wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. Waamini wanahimizwa kukuza na kudumisha ari na moyo wa kimisionari kama sehemu ya mbinu mkakati wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani. 

Waamini kuzeni ari na mwamko wa kimisionari ndani ya Kanisa!

Askofu mkuu Agostino Marchetto, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Mèrida-Badajoz, huko nchini Hispania, na kilele chake kikawa ni hapo tarehe 11 Oktoba 2019 amekazia kuhusu “ukatoliki na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo” kama ulivyopembuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika nyaraka zake!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican katika Hati ya Fumbo la Kanisa, “Lumen Gentium” wanasema, Kristo Yesu ndiye Mwanga wa Mataifa “Lumen Gentium” na katika hati hii, wanafafanua maana ya Fumbo la Kanisa; Umuhimu wa Taifa la Mungu; Muundo wa Kanisa; nafasi na dhamana ya waamini walei katika maisha na utume wa Kanisa na kwamba, wito wa watu wote katika Kanisa ni kuwa watakatifu. Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican wanachambua pia nafasi ya watawa; umoja wa Kanisa linalosafiri na umoja wa Kanisa lililo mbinguni. Mababa wa Mtaguso walibainisha pia nafasi ya Bikira Maria, Mama wa Mungu katika Fumbo la Kristo Yesu na Kanisa lake.

Ni katika muktadha huu, Askofu mkuu Agostino Marchetto, katika maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 25 tangu kuanzishwa kwa Jimbo kuu la Mèrida-Badajoz, huko nchini Hispania, na kilele chake kikawa ni hapo tarehe 11 Oktoba 2019 amekazia kuhusu “ukatoliki na utume wa Kanisa katika ulimwengu mamboleo” kama ulivyopembuliwa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican, akikazia umoja, upendo na mshikamano katika kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari, kama sehemu ya utekelezaji wa kazi ya ukombozi ambayo Kristo Yesu ameliachia Kanisa lake. Watu wote wa Mungu ni warithi  wa uzima wa milele na kwamba, Roho Mtakatifu ni Bwana na Mleta uzima.

Hii ni changamoto na mwaliko kwa waamini kujikita katika mchakato wa ujenzi wa Ufalme wa Mungu unaofumbatwa katika umoja na udugu wa watu wa Mungu. Umoja huu unapaswa kujidhihirisha katika Liturujia ya Kanisa, Malezi na majiundo ya watu wa Mungu pamoja na Majadiliano ya kidini na kiekumene. Umoja wa Kanisa unashuhudiwa katika urika wa Maaskofu mahalia, wakiwa wameungana na Khalifa Mtakatifu Petro katika umoja na amani kwa kukazia ari na mwamko wa kimisionari. Lengo ni kwenda ulimwenguni kote ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Kumbe, uinjilishaji ni dhamana inayopaswa kuvaliwa njuga na Wakristo wote hasa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko, ili ulimwengu mzima, uweze kujisikia kuwa ni sehemu muhimu sana ya watu wa Mungu.

Waamini watambue kwamba, wao ni Hekalu la Roho Mtakatifu na hivyo wanapaswa kumtolea Mwenyezi Mungu utenzi wa utukufu, sifa na shukrani kwa Mwenyezi Mungu, Muumbaji. Askofu mkuu Agostino Marchetto, ambaye aliwahi kuwa ni Katibu mkuu wa Baraza la Kipapa la Shughuli za Kichungaji kwa wakimbizi, wahamiaji na watu wasiokuwa na makazi maalum anaendelea kufafanua kwamba, Hati za Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican: “Dei Verbum” yaani “Ufunuo wa Kimungu” pamoja na “Gaudium et spes yaani “Juu ya Kanisa na Ulimwengu” zinakita ujumbe wake katika ari na mwamko wa kimisionari. Zinakazia majadiliano katika ukweli na uwazi na ushirikiano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu.

Majadiliano na utume wa Kanisa ni mambo msingi katika mchakato mzima wa uinjilishaji sanjari na upyaisho wa maisha na utume wa Kanisa. Uhuru wa kuabudu na uhuru wa kidini ni muhimu sana kwa waamini kuweza kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo adili na matakatifu. Majadiliano ya kidini na kiekumene, ni sehemu muhimu sana ya vinasaba vya uinjilishaji, yawasaidie waamini kutafuta na hatimaye, kuuambata ukweli. Wajenge umoja na mshikamano wa dhati kwa kutambua na kuheshimu pia tofauti zao msingi.

Lumen Gentium

 

 

 

 

12 October 2019, 15:08