Tafuta

Vatican News
Maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha mchakato wa amani na upatanisho miongoni mwa watu wa Mungu. Maadhimisho ya Sinodi ya Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine ni muda muafaka wa kukuza na kudumisha mchakato wa amani na upatanisho miongoni mwa watu wa Mungu. 

Sinodi Kanisa Katoliki la Kigiriki Ukraine: Amani & Upatanisho

kardinali Leonardo Sandri katika tafakari yake amekazia zaidi umuhimu wa kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa Mungu nchini Ukraine; maana na umuhimu wa kulinda zawadi ya maisha na imani kwa njia ya wongofu endelevu unaofumbatwa katika hali ya uvumilivu, dhidi ya ukanimungu na upagani mamboleo unaoendelea kujitokeza kwa kasi kubwa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Leonardo Sandri, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki, Jumapili, tarehe 1 Septemba 2019 amezindua rasmi maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, itakayohitimishwa hapo tarehe 10 Septemba 2019 kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ushirikiano na umoja katika ushuhuda wa Kanisa la Ukraine wakati huu”. Ibada hii ya Misa Takatifu imekwanda sanjari na maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 50 tangu Kanisa kuu la Mtakatifu Sofia lililoko mjini Roma lilipotabarukiwa hapo tarehe 28 Septemba 1969. Ibada hii imeongozwa na Askofu mkuu Sviatoslav Shevchuk, Mkuu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine.

Kardinali Leonardo Sandri ametoa tamko la maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu wa Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine. Katika tafakari yake amekazia zaidi umuhimu wa kutafuta, kujenga na kudumisha misingi ya haki, amani na upatanisho wa Mungu nchini Ukraine; maana na umuhimu wa kulinda zawadi ya maisha na imani kwa njia ya wongofu endelevu unaofumbatwa katika hali ya uvumilivu, dhidi ya ukanimungu na upagani mamboleo unaoendelea kujitokeza kwa kasi kubwa. Matatizo na changamoto mbali mbali za maisha ya watu wa Mungu nchini Ukraine zinafahamika sana kwa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Imekuwa ni fursa pia ya kumkumbuka na kumwombea Hayati Kardinali Achille Silvestrini, aliyefariki dunia tarehe 29 Agosti 2019 ambaye, enzi za uhai wake, amewahi kuliongoza Baraza la Kipapa kwa Makanisa ya Mashariki kuanzia mwaka 1991 hadi mwaka 2000. Huyu ni kiongozi ambaye alitoa kipaumbele cha pekee kwa maisha na utume wa Kanisa nchini Ukraine. Mwenyezi Mungu, mwingi wa huruma na mapendo ambaye ameliongoza Kanisa Katoliki la Kigiriki nchini Ukraine, asaidie mchakato wa toba na wongofu wa ndani; asafishe, agange na kuponya kinzani na mipasuko mbali mbali inayojitokeza nchini humo pamoja na kuwakirimia neema ya msamaha na upatanisho.

Mwishoni, Kardinali Leonardo Sandri amemwomba Mwenyezi Mungu ili awajalie watu wa Mungu nchini Ukraine kupata uhuru wa ndani; haki, amani na upatanisho wa kitaifa. Wakiwa wanaunganishwa na Sakramenti ya Ubatizo, watambue kwamba, wameifia dhambi na utu wa kale na kwamba, kwa sasa wote wanashiriki: ukuhani, unabii na ufalme wa watu wa Mungu. Wajumbe wa Sinodi hii wametembelea na kusali kwenye Makaburi ya Watakatifu Yosefat na Petro Mtume.

Sinodi Ukraine
03 September 2019, 18:25