Tafuta

Vatican News
Kuna tofauti sana kwa wenye uwezo mkubwa na wasio na uwezo,kati ya wenye nafasi nzuri katika jamii na waliotengwa na jamii,kati ya matajiri na maskini. Kuna tofauti sana kwa wenye uwezo mkubwa na wasio na uwezo,kati ya wenye nafasi nzuri katika jamii na waliotengwa na jamii,kati ya matajiri na maskini. 

Ondoeni tofauti kati ya watu wenye uwezo mkubwa na wasio kuwa nao!

Mwakilishi wa kudumu wa Vatican katika Ofisi za Umoja wa Mataifa ameutaka umoja wa Mataifa kuondoa tofauti iliyopo kati ya watu wenye uwezo mkubwa na wasio na uwezo,kati ya wenye nafasi nzuri katika jamii na waliotengwa na jamii,kati ya matajiri na maskini na hivyo Umoja wa Mataifa wanapaswa kuwajali maskini,walemavu,wazee, katika masuala ya kiuchumi,kijamii,kisiasa,kiutamaduni.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican

Askofu mkuu Bernadito Auza Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kati ofisi za Umoja wa matiafa jijini New York, katika mkutano wa 74 wa Umoja wa Mataifa uliofanyika hivi karibuni mwishoni mwa mwezi Septemba, ameutaka umoja wa Mataifa kuondoa tofauti iliyopo kati ya watu wenye uwezo mkubwa na wasio na uwezo, kati ya wenye nafasi nzuri katika jamii na waliotengwa na jamii,  kati ya matajiri na maskini, na hivyo Umoja wa Mataifa wanapaswa  kuwajali maskini, walemavu, wazee,  katika masuala ya kiuchumi, kijamii, kisiasa, kiutamaduni.

Askofu mkuu Bernardito ameyasema hayo katika mkutano wa maendeleo ya jamii akibaini changamoto zilizopo zinazohitaji utatuzi wa haraka. Katika kufafanua mada hiyo amesema, pamoja na kubuni fursa mpya za elimu na ajira, bado maendeleo mamboleo hayatoi fursa sawa kwa wote. Kumekuwepo na mitazamo ya kuwajali watu kutokana na walichochangia kwenye jamii. Hii inaminya fursa kwa wazee na vijana ambao hawakupata fursa ya ajira na hivyo kuwa na mchango kidogo katika jamii. 

Maendeleo ya kweli ni yale yanayozingatia heshima na utu yakifungamanisha vipaji hata vya watu wa hali ndogo ya kiuchumi vinavyohuishwa katika utekelezaji wake na makampuni mbalimbali ulimwenguni. Nafasi za elimu na ajira zinapaswa kutolewa wakipewa upendeleo mkubwa watu walio na ulemavu badala ya kutengwa. Bado vitengo vingi vinavyohusika na ulinzi wa wasiojiweza havijafanikiwa kuwapatia haki zao. Sehemu nyingi zenye ukosefu wa ajira vijana wanalazimika kuingia jeshini au kukimbia nchi zao wakitafuta ajira. Kama elimu itatolewa kwa vijana wanaoishi katika mazingira hatarishi kuna uwezekano wa kuondoa tofauti zilizopo na kuhamasisha uchumi endelevu unaowashirikisha vijana na familia.

Katika kuhitimisha Askofu mkuu Bernardito Auza, ameutaka umoja wa mataifa kuhamasisha maendeleo fungamani katika jamii. Tena kuwekeza katika familia na kuweka sera nzuri za ulinzi wa jamii kutaongeza kasi ya ukuaji wa uchumi. Kwa hiyo maendeleo ya jamii yatokane maendeleo msingi ya kifamilia yenye kutoa nafasi za kuwapenda na kuwatunza wazee, wasio na uwezo, maskini na vijana. Huu ndiyo msingi wa maendeleo ya kweli ya jamii ya leo na vizazi vijavyo.

26 September 2019, 09:19