Tafuta

Vatican News
2019.09.15 Beatificazione Riccardo Henkes, Limburg 2019.09.15 Beatificazione Riccardo Henkes, Limburg 

Mwenyeheri Riccardo Henkes shuhuda wa ukweli katika imani

Kardinali Koch amekazia kuhusu: Msalaba wa Kristo Yesu, kama ushuhuda wa upendo wa Mungu; kifodini ni kielelezo cha hali ya juu sana cha upendo; ushuhuda wa imani unapaswa kububujika kutoka katika imani inayomwilishwa kwenye matendo. Aiwezekani kuwepo kwa upendo bila kuwa na sadaka. Mwenyeheri Riccardo Henkes aliishi kifungoni kwa muda wa miaka 17 huko Dachau.

Na Padre Angelo Shikombe, - Vatican.

Kardinali Kurt Koch, Rais wa Baraza la Kipapa la Kuhamasisha Umoja wa Wakristo kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko, Jumapili, tarehe 15 Septemba 2019, huko Limburg, nchini Ujerumani, amemtangaza Mtumishi wa Mungu Padre Riccardo Henkes wa Shirika la Wapallottini, kuwa Mwenyeheri. Baba Mtakatifu Francisko anasema, Padre Henkes aliuwawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani huko Dachau kunako mwaka 1945. Hii ni mifano hai ya mashuhuda na wafuasi wa Kristo, wanaoendeleza kuwategemeza hata waamini wengine katika safari yao kuelekea kwenye utakatifu wa maisha. Kardinali Kurt Koch katika mahubiri yake, amekazia kuhusu Msalaba wa Kristo Yesu, kama ushuhuda wa upendo wa Mungu; kifodini ni kielelezo cha hali ya juu sana cha upendo; ushuhuda wa imani unapaswa kububujika kutoka katika imani inayomwilishwa kwenye matendo. Anakaza kusema, haiwezekani kuwepo kwa upendo bila kuwa na sadaka. Mwenyeheri Riccardo Henkes aliishi kifungoni kwa muda wa miaka 17 huko Dachau akibeba msalaba wake na kumshuhudia Yesu katika upendo wa Mungu.

Riccardo Henkes ametangazwa kuwa Mwenyeheri katika maadhimisho ya Siku kuu ya kutukuka kwa Msalaba, tarehe 14 Septemba 2019 ili aendelee kuwa shuhuda wa Msalaba wa Yesu na wa upendo wa Mungu. Msalaba wa Yesu unasimama kama alama ya upendo wa kweli kwa Mungu na haipingani na hadhi ya mwana wa Mungu. Ni alama inayoashiria ukombozi wa wanadamu. Msalaba ni ushuhuda unaofundisha kuwa hakuna upendo usiokuwa na sadaka na mateso. Mwenyeheri Padre Henkes hakukitafuta kifo dini kwa namna yeyote ile bali alibaki mwaminifu katika imani yake. Kwa maana kifo dini kwa mkristo hakina tabia ya mtu kutafuata kifo na kuyapuuza maisha bali kinatokana na mapenzi ya Mungu. Kardinali Kurt Koch amesema, kifodini ni matokeo ya ushuhuda wa kiimani kama alivyoishi mwenyeheri Padre Richard Henkes kwa kupinga upagani mamboleo wa kinazi na hivyo serikali kujenga chuki dhidi yake iliyopelekea kufungwa kwake na kuuwawa kikatili. Mwenyeheri Padre Riccardo Henkes alitoa ushuhuda wa kitume hata alipokuwa gerezani na kuna ushuhuda wa chuki iliyosababisha kifo chake. Aidha, Kardinali Kurt Koch amesema, ufiadini ni upendo wa kiwango cha juu kabisa kama ulivyooneshwa na Mwenyeheri kwa mithili ya Kristo ambaye hakuyatafuta mateso na msalaba bali aliyapokea kama matashi ya Mungu kwa ajili ya wokovu.

Hata baada ya kifo chake, watu walianza kumwomba na kufanikiwa katika sala zao, wakataka kuufukua mwili wake ili wajichukulie masalia lakini mwili wake ulihamishiwa Limburg ambako umehifadhiwa.  Baada ya kuwa na uhakika wa sadaka ya maisha yake, ametangazwa kuwa Mwenyeheri ili aendelee kuwa mfano hai wa ushuhuda na  ufuasi wa Kristo, unaoendeleza kuwategemeza hata waamini wengine katika safari yao kuelekea kwenye utakatifu wa maisha yao. Mwenyeheri Padre Riccardo Henkes, alizaliwa  mjini Limburg, nchini Ujerumani tarehe 26 Mei 1900. Aliweka nadhiri zake za daima 25 Septemba 1924. Akapewa Daraja takatifu ya upadre 6 Juni 1925. Akafariki dunia tarhe  22 Februari 1945. Katika maisha yake, alikuwa ni Padre na Jalimu aliyepinga kwa nguvu zote utawala wa kinazi na mauaji ya watu wanyonge na hatimaye kuuawa kikatili kutokana na chuki dhidi ya imani huko Dachau kunako mwaka 1945.

Mwenyeheri Riccardo
18 September 2019, 15:05