Tafuta

Vatican News
Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kuanzia tarehe 1-4 Oktoba 2019 ni mwenyezi wa mkutano wa Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinachopambana na utumwa mamboleo duniani. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, kuanzia tarehe 1-4 Oktoba 2019 ni mwenyezi wa mkutano wa Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinachopambana na utumwa mamboleo duniani. 

Mkutano dhidi ya Utumwa Mamboleo waanza, Nairobi, Kenya!

Awamu ya pili ya mkutano huu huko Nairobi nchini Kenya, unatarajiwa kuwa ni jukwaa litakalotoa fursa kwa washiriki kushirikishana: ujuzi, maarifa na mbinu mkakati wa kupambana na biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa wataalam na maofisa wanaopambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo wanashiriki.

Na Rose Achiego, Nairobi & Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. - Vatican.

Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo kilichozinduliwa na Baba Mtakatifu Francisko kunako mwaka 2014, ili kupambana na donda hili la kijamii, linalodhalilisha utu na heshima ya binadamu kwa kuwatumbukiza watoto, wasichana na wanawake katika utumwa mamboleo. Biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni uhalifu mkubwa dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu; mambo ambayo wakati mwingine yanafumbiwa macho na jamii, lakini umefika wakati kwa Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kwamba, inatokomeza kabisa biashara ya binadamu na athari zake. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha, kinaongozwa na Kardinali Vincent Nichols, Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Uingereza na Wales, kwa kushirikiana na wakuu wa Majeshi ya Polisi na Maaskofu kutoka sehemu mbali mbali za dunia. Kikundi hiki kinaendelea kufanya kazi kwa pamoja ili kung'oa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake; utumwa mamboleo pamoja na kutoa huduma za kichungaji na kijamii kwa wahanga wa vitendo hivi vya kinyama dhidi ya utu, heshima na haki msingi za binadamu.

Kikundi hiki kwa sasa kinatekeleza dhamana na wajibu wake katika nchi 30 duniani.  Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha, kinapania pamoja na mambo mengine, kuibua mbinu mkakati wa kuzuia vitendo hivi vya kinyama vinavyodhalilisha utu na heshima ya binadamu pamoja na kuendelea kutoa huduma za kichungaji. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinataka pia kushirikiana na Jumuiya ya Kimataifa katika mapambano dhidi ya biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo, donda ndugu katika ulimwegu mamboleo. Baraza la Maaskofu Katoliki Kenya, K.C.C.B., kuanzia tarehe 1-4 Oktoba 2019, litakuwa ni mwenyeji wa Mkutano wa Pili wa Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha. Itakumbukwa kwamba, kunako mwaka 2018, Mkutano wa kwanza ulifanyika Barani Afrika huko Abuja, nchini Nigeria. Mkutano huu ulihudhuriwa na viongozi wa Kanisa, watunga sera na sheria; vyombo vya ulinzi na usalama kwa kuongozwa na kauli mbiu“Kanisa na Serikali kushirikiana kwa pamoja ili kurejesha utu wa wale waliotumbukizwa kwenye biashara ya binadamu”.

Awamu ya pili ya mkutano huu huko Nairobi nchini Kenya, unatarajiwa kuwa ni jukwaa litakalotoa fursa kwa washiriki kushirikishana: ujuzi, maarifa na mbinu mkakati wa kupambana na biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo. Mtandao wa wataalam na maofisa wanaopambana na biashara ya binadamu na utumwa mamboleo, watashirikisha uzoefu na mang’amuzi yao katika mapambano ya biashara hii Barani Afrika, ambako kuna waathirika wengi zaidi. Padre Mark Odion, Mratibu wa Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha Barani Afrika, hivi karibuni, akizungumza na Kamati ya Maandalizi Barani Afrika alisikika akisema kwamba, hata wakimbizi na wahamiaji wanahitaji kupewa huduma za kichungaji na maisha ya kiroho. Kuna haja kwa Bara la Afrika kujizatiti katika kutoa huduma kwa waathirika wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na mifumo mbali mbali ya utumwa mamboleo, kwa kushirikiana na taasisi mbali mbali Barani Afrika.

Mkutano huu, utaibua mbinu mkakati utakaotumika kwa ajili ya Bara la Afrika, kwa kuhakikisha kwamba, rasilimali watu, fedha na vitu vinavyotumika ni kutoka Barani Afrika. Hii ni pamoja na kujenga uhusiano bora zaidi kati ya viongozi wa Kanisa na vyombo vya ulinzi na usalama, ili kuwatambua wadau wa biashara hii na waathirika, ili sheria iweze kuchukua mkondo wake. Kikundi cha Kimataifa cha Mtakatifu Martha kinabainisha kwamba, kwa njia ya ushirikiano kati ya Kanisa na vyombo vya ulinzi na usalama, kumekuwepo na ufanisi mkubwa huko Argentina, Lithuania, Ujerumani na Nigeria kwa upande wa Bara la Afrika. Wahanga wa biashara ya binadamu na viungo vyake pamoja na wale wote wanaotumbukizwa kwenye mifumo ya utumwa mamboleo, wameanza kutambuliwa na taarifa kuhusu matukio haya zinaendelea kuongezeka kwenye vituo vya Polisi sanjari na kampeni ya kuragibisha uwepo na madhara ya biashara ya binadamu duniani.

Baba Mtakatifu Francisko daima anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, kufungua macho na nyoyo zao, ili kuweza kusikiliza na kujibu kilio cha mateso na mahangaiko ya waathirika wa biashara haramu ya binadamu na viungo vyake. Anawataka kusimama kidete, kupambana kufa na kupona, ili kuvunjilia mbali mtandao wa biashara haramu ya binadamu duniani na utumwa mamboleo ili hatimaye, kuleta faraja, uponyaji wa ndani na huduma kwa wahanga wa nyanyaso kwa utu, heshima na haki msingi za binadamu. Katika maadhimisho ya Kumbu kumbu ya Mtakatifu Josefina Bakhita, kunako mwaka 2015, Kanisa lilianzisha Siku ya Kimataifa ya Kupambana na Biashara Haramu ya Binadamu na utumwa mamboleo, unaoendelea kudhalilisha: utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Takwimu za Jumuiya ya Kimataifa zinaonesha kwamba, zaidi ya asilimia 70% ya wahanga wa biashara haramu ya binadamu na utumwa mamboleo ni wanawake na wasichana, kati yao theluthi moja ni watoto wadogo.

Hii  ni hali ya unyonyaji, unyanyasaji, na mateso ya wanyonge hawa kimwili, kiakili na kisaiokolojia na ni aibu na kashfa kubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa inayoonekana hata kutojali kabisa uvunjwaji wa utu, heshima na haki msingi za watu hawa! Baba Mtakatifu Francisko anamwomba Mtakatifu Josefina Bhakita, Msimamizi wa waathirika wa biashara haramu ya binadamu, kuwaombea watu wote waliotumbukizwa kwenye utumwa mamboleo, ili kwa neema na msaada wa Mwenyezi Mungu waweze kuokolewa na hatimaye, kusaidiwa kuganga na kuponya madonda ya nyanyaso dhidi ya utu na heshima yao. Askofu mkuu Bernardito Auza Mwakilishi wa kudumu wa Vatican kwenye Umoja wa Mataifa anasema, Mpango wa Maendeleo Endelevu na Fungamani wa mwaka 2015 hadi mwaka 2030, Jumuiya ya Kimataifa inapania kufutilia mbali mifumo yote ya: biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na unyonyaji; pamoja na nyanyaso dhidi ya watoto wadogo ifikapo mwaka 2030.

Ili kuweza kufikia maamuzi haya kuna haja kwa Jumuiya ya Kimataifa: kuaminiana, kutekeleza sera na mikakati iliyokwisha kuibuliwa pamoja na kuwajibika kwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu. Kikundi cha Mtakatifu Martha ni taasisi ya kimataifa inayopaswa kuigwa katika mapambano dhidi ya biashara ya binadamu, utumwa mamboleo na mifumo yote ya unyonyaji, ili kuwahudumia waathirika, kwa kulinda na kuheshimu utu wao pamoja na kuwarejeshewa uhuru ambao walikuwa wamepokwa na watesi wao kwa kuwageuza kuwa watumwa. Ni taasisi ambayo imeweza kwa mwanga wa Injili kufunua kashfa na madonda yanayodhalilisha utu wa binadamu; ili kuanza kuyaganga na kuyaponya, tayari kuandika historia mpya ya maisha katika utu na heshima ya binadamu!

Kikundi St. Martha

 

30 September 2019, 12:43