Tafuta

Vatican News
Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa amefariki dunia Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 huko Xalapa nchini Mexico Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa amefariki dunia Jumapili tarehe 11 Agosti 2019 huko Xalapa nchini Mexico  (Vatican Media)

Tanzia: Kardinali Sergio Obeso Rivera amefariki dunia!

Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, amefariki dunia, Jumapili, tarehe 11 Agosti 2019. Alizaliwa tarehe 31 oktoba 1931 huko Xalapa nchini Mexico. Tarehe 31 Oktoba 1954 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Mwaka 1971 akateuliwa na kuwekwa wakfu kuwa Askofu. Mwaka 1979 akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Xalapa.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anasema, Kristo Yesu katika maisha na utume wake, aliwaangalisha wafuasi wake kukesha daima, ili waweze kuwa tayari Mwenyezi Mungu anapowapitia katika hija ya maisha yao hapa ulimwenguni, kwa sababu daima anawatembelea waja wake. Yesu anawaonesha mtindo wa maisha wanaopaswa kuufuata yaani, viuno vyao viwe vimefungwa na taa zao ziwe zinawaka. Huu ni mwaliko kwa waamini kujiandalia mazingira ya hija, tayari kutoka na kuanza safari, kwa kutambua kwamba, hapa duniani hawana makazi ya kudumu. Ni kutokana na mwelekeo huu, waamini wanapaswa kujiachilia na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu kama ilivyokuwa kwa Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, aliyefariki dunia, Jumapili jioni, tarehe 11 Agosti 2019.

Itakumbukwa kwamba, alizaliwa tarehe 31 oktoba 1931 huko Xalapa nchini Mexico. Baada ya masomo na majiundo yake ya Kikasisi, kunako tarehe 31 Oktoba 1954 akapewa Daraja Takatifu ya Upadre. Kwa muda wa miaka 17 alitekeleza dhamana na utume wake wa Kipadre kama Jaalimu wa Falsafa na Taalimungu; Mkurugenzi wa maisha ya kiroho na hatimaye kama Gombera. Kunako mwaka 1971 Mtakatifu Paulo VI akamteuwa kuwa Askofu na kuwekwa wakfu tarehe 29 Julai 1971. Tarehe 18 Januari 1974 akateuliwa kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Papantla na Askofu mkuu mwandamizi mwenye haki ya kurithi Jimbo kuu la Xalapa. Akasimikwa rasmi kuwa Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Xalapa tarehe 12 Machi 1979. Tarehe 18 Novemba 1982 akachaguliwa kuwa Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Mexico kwa vipindi vitatu hadi mwaka 1995.

Tarehe 10 Aprili 2007, Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI akaridhia ombi lake la kung’atuka kutoka madarakani. Baba Mtakatifu Francisko kwa kutambua mchango wake katika maisha na utume wa Kanisa nchini Mexico kunako tarehe 28 Juni 2018 akamteuwa na kumsimika kuwa Kardinali. Kardinali Sergio Obeso Rivera, Askofu mkuu Mstaafu wa Jimbo kuu la Xalapa, nchini Mexico, apate rehema kwa Mungu na apumzike kwa amani. Kutokana na kifo cha Kardinali Rivera kwa sasa Baraza la Makardinali linaundwa na Makardinali 216, kati yao wenye haki ya kupiga na kupigia kura wakati wa uchaguzi wa Khalifa wa Mtakatifu Petro ni 119 na waliosalia 97 hawana tena haki ya kupiga wala kupigiwa kura!

Kardinali Rivera

 

12 August 2019, 14:30