Tafuta

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia ni tukio muhimu sana katika maisha na utume wa Kanisa Amerika ya Kusini. 

Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia: Tukio muhimu la maisha na utume wa Kanisa

Papa Francisko anasema, ukoloni mamboleo unaendelea kujikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Sinodi ya Maaskofu ni tukio la Kikanisa ili kupembua changamoto zote hizi!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko wakati wa hija yake ya kitume huko Amerika ya Kusini hivi karibuni alisikita kusema kwamba: Ukoloni mamboleo unaendelea kujikita katika nguvu ya kiuchumi: kwa uchimbaji wa mafuta na gesi asilia; kilimo cha mashamba makubwa ili kukidhi mahitaji ya mali ghafi ya viwanda; ni mambo yanayotishia usalama, maisha, ustawi na maendeleo ya watu wa Mungu Ukanda wa Amazonia. Baba Mtakatifu anawataka Maaskofu kuwa karibu zaidi na wakleri wao; kukuza na kudumisha tunu msingi za maisha ya Kiinjili na kiutu, ili kupambana na: saratani ya rushwa, ufisadi na kumong'onyoka kwa haki msingi, utu na heshima ya binadamu na kwamba, Maaskofu wathamini majadiliano katika ukweli na uwazi. Lengo la Sinodi hii itakayoadhimishwa mjini Vatican kuanzia tarehe 6-27 Oktoba 2019, ni kuibua mbinu mkakati wa shughuli za kichungaji, zitakazokidhi mchakato wa uinjilishaji wa kina, unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kanisa linataka kuendeleza mchakato wa utamadunisho kwa kuhakikisha kwamba, tunu msingi za kiinjili zinamwilishwa katika tamaduni, mila na desturi njema za watu wa Ukanda wa Amazonia pamoja na kuzisafisha zile zinazosigana na kupingana na tunu msingi za Kiinjili! Ni Sinodi itakayojikita katika mchakato wa kukuza na kudumisha haki msingi za binadamu kama njia ya kuenzi utu na heshima ya binadamu! Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu, wakati wa Semina ya Maandalizi ya Sinodi ya Amazonia iliyohitimishwa hivi karibuni alikaza kusema, hili ni tukio la kikanisa na wala si kusanyiko la kisiasa! Sinodi hii inaongozwa na kauli mbiu "Amazonia: njia mpya ya Kanisa na kwa ajili ya ekolojia fungamani". Hati ya maandalizi ya Sinodi ya Amazonia inakazia umuhimu wa: kuona, kung'amua na kutenda! Ni Sinodi itakayopembua tema mbali mbali:kuhusu: haki jamii, malezi, katekesi, liturujia na utambulisho wa Kanisa katika Ukanda wa Amazonia.

Maadhimisho ya Sinodi za Maaskofu yamedadavuliwa kwa kina na mapana katika Katiba ya Kitume ya Papa Francisko “Episcopalis Communio” yaani “Kuhusu Sinodi za Maaskofu” iliyochapishwa kunako mwezi Septemba 2018. Hiki ni chombo cha uinjilishaji kinachopania kukuza na kudumisha ari na mwamko wa kimisionari dhamana na wajibu wa Kanisa. Maaskofu wanahimizwa kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu “sensum fidei” katika maisha na utume wa Kanisa! Ni katika mantiki hii, Kanisa linataka kusikiliza na kujibu kilio cha watu wa Mungu kutoka Ukanda wa Amazonia mintarafu utunzaji bora wa mazingira nyumba ya wote kama sehemu ya mbinu mkakati wa uinjilishaji wa kina. Baba Mtakatifu Francisko anakazia umuhimu wa kulinda, kutunza na kuendeleza mazingira kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.  Hii ni changamoto kubwa na endelevu katika Ukanda wa Amazonia. Ikumbukwe kwamba, Kanisa daima linataka kujipambanua katika huduma ya kiroho na kimwili kwa ajili ya watu wa Mungu anasema, Kardinali Lorenzo Baldisseri.

Kanisa linataka kukuza na kudumisha miito ya kipadre na kitawa kutoka kwa watu mahalia wa Ukanda wa Amazonia. Utamadunisho, maendeleo endelevu na fungamani ya binadamu; umoja na mshikamano ni kati ya mambo ambayo yanapewa uzito wa pekee kama sehemu ya maandalizi na hatimaye, maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia. Mama Kanisa anataka kuchota amana na utajiri; hekima na busara kutoka kwenye familia ya Mungu, Ukanda wa Amazonia kuhusu mila, desturi na tamaduni njema za watu wa Mungu. Lengo ni kuliwezesha Kanisa kuendelea kusoma alama za nyakati kwa kupambana na maafa makubwa yanayosababishwa na uharibifu wa mazingira nyumba ya wote kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi. Kuna mmong’onyoko mkubwa wa maadili na utu wema kutokana na maendeleo makubwa ya sayansi na teknolojia ya mawasiliano; athari za myumbo wa uchumi, kifedha na hata katika masuala ya kijamii.

Zote hizi ni changamoto zinazopaswa kuangaliwa kwa jicho la Kiinjili, bila kusahau wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji wanaotafuta: usalama, hifadhi na maisha bora zaidi ughaibuni. Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia anasema Kardinali Lorenzo Baldisseri, Katibu mkuu wa Sinodi za Maaskofu ni Kanisa kutaka kutambua na kuthamini mchango wa familia ya Mungu katika maisha na utume wa Kanisa la Kiulimwengu na dunia katika ujumla wake. Ekolojia na Kanisa ni sawa na chanda na pete, kwani Mama Kanisa anataka kulinda na kudumisha kazi ya uumbaji. Kanisa linataka kuzama katika hali halisi ya watu wa Ukanda wa Amazonia ili kutambua: Shida, changamoto na fursa zilizopo, ili kwa msaada wa wataalam na mabingwa mbali mbali, ziweze kupewa ufumbuzi wa kudumu mintarafu mwanga wa Injili kwa kuzingatia majadiliano katika ukweli na uwazi!

Maadhimisho ya Sinodi ni mchakato wa Kanisa kutembea kwa pamoja kama sehemu ya utekelezaji wa utume na dhamana ya uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili; mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee na Baba Mtakatifu Francisko.Itakuwa ni nafasi ya kuwahimiza waamini walei kujikita zaidi na zaidi katika mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu, kwa kuthamini mchango unaotolewa na wanawake katika maisha na utume wa Kanisa!

Amazonia 2019
01 August 2019, 11:55