Tafuta

Vatican News
Padre Raniero Cantalamessa: Utenzi wa Bikira Maria ni mtazamo mpya kuhusu Mungu na Ulimwengu katika ujumla wake! Padre Raniero Cantalamessa: Utenzi wa Bikira Maria ni mtazamo mpya kuhusu Mungu na Ulimwengu katika ujumla wake!  (© Catherine Leblanc - byzance-photos.fr)

Utenzi wa Bikira Maria: Magnificat: Mtazamo wa Mungu & Ulimwengu

Padre Raniero Cantalamessa kwamba, Utenzi wa Bikira Maria ni mwelekeo kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu katika ujumla wake; ni shule ya toba, wongofu wa ndani; utakatifu wa maisha na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Bikira Maria aliyekingizwa dhambi ya asili, akapalizwa mbinguni, amevikwa taji la Umalkia. Ni mwombezi wa wote..

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Jimbo kuu la Aquila nchini Italia linaadhimisha kumbu kumbu ya Miaka 725 tangu Papa Celestini V katika Waraka wake wa Kitume wa “Inter Sanctorum Solemnia” wa tarehe 29 Septemba 1294 alipochapisha kuhusu “Msamaha wa Celestini” na tangu wakati huo, Jimbo kuu la Aquila likawa ni chemchemi ya msamaha na huruma ya Mungu kwa waja wake. Kardinali Giuseppe Petrocchi ametangaza na kuzindua maadhimisho ya Jubilei ya Miaka 200 ya huruma na msamaha, yatakayofikia kilele chake hapo tarehe 28 Agosti 2019 katika mkesha wa Sherehe ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji kukatwa kichwa inayoadhimishwa na Mama Kanisa kila mwaka ifikapo tarehe 29 Agosti. Tukio hili litaadhimishwa na Kardinali Giuseppe Bertello, Rais wa Tume na uongozi wa mji wa Vatican. Kuanzia tarehe 24-29 Agosti 2019, waamini wanayo fursa ya kuadhimisha Mafumbo ya Kanisa; kwa njia ya Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, Sakramenti ya Upatanisho kati ya Mungu na jirani; Mazungumzo na ushauri wa kiroho utakaotolewa na wakleri pamoja na watawa ambao wako katika eneo hili kama mashuhuda na vyombo vya Injili ya huruma, msamaha, upendo na matumaini kwa watu waliokata tamaa baada ya tetemeko la ardhi lililotokea katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita kuleta athari za kubwa sana katika maisha ya watu wa Mungu Jimbo kuu la Aquilla.

Hiki ni kipindi ambacho Mama Kanisa anatoa rehema kwa waamini watakaotimiza masharti yaliyowekwa! Rehema ni msamaha mbele ya Mwenyezi Mungu ambao kosa lake lilikwishwafutwa, msamaha ambao Mkristo mwamini, aliyejiandaa vyema huupata  kutoka katika hazina ya malipizi ya Kristo Yesu na ya Watakatifu. Rehema inaweza kuwa ya muda mfupi au Kamili. Rehema ya muda huondoa sehemu ya adhabu za dhambi na rehema kamili huondoa adhabu zote (Rej. KKK, namba1472). Mkristo huweza kupata rehema kamili kwa ajili yake yeye mwenyewe au kwa ajili ya marehemu kama atatimiza masharti yafuatayo: Mosi, awe na nia thabiti ya kupata rehema katika kipindi kilichopangwa, pili apokee Sakramenti ya Upatanisho, tatu, apokee Sakramenti ya Ekaristi Takatifu siku hiyo ya kutolewa rehema kamili, nne; asali kwa ajili ya nia za Baba Mtakatifu na tano atembelee Kanisa au Kituo maalumu kilichotengwa kwa ajili ya kupatiwa rehema Kamili.

Padre Raniero Cantalamessa, Mhubiri wa Nyumba ya Kipapa ndiye aliyepewa dhamana ya kuwaandaa watu wa Mungu, Jimbo kuu la Aquilla katika hija ya maisha ya kiroho, kuelekea kwenye kisima cha huruma na msamaha wa Celestini kwa njia ya tafakari kuhusu utenzi wa Bikira Maria “Magnificat”, mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu katika ujumla wake. Hii ni fursa ya kutafakari huruma ya Mungu inayodumu kwa vizazi vyote, kwa kumwachia nafasi Bikira Maria kwa niaba ya Kanisa aweze kuzungumza na watu wa Mungu hadi miisho ya dunia. Katika tafakari yake, Padre Cantalamessa anasema, Utenzi wa Bikira Maria, ni mtazamo mpya kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu. Ni utenzi wa toba na wongofu wa ndani unaowahimiza waamini kujenga na kudumisha utamaduni unaomwilisha huruma na upendo wa Mungu katika uhalisia wa maisha. Utenzi wa “Magnificat” una mwelekea Mwenyezi Mungu,  ambaye ni mkuu, mwingi wa huruma na mapendo, mtakatifu na enzi zote ni zake na kwamba, huruma yake kwa watu wanaomcha hudumu kizazi hata kizazi.

Hiki ni kielelezo cha huruma na upendo wa Mungu unaobubujika kutoka katika Fumbo la Utatu Mtakatifu. Huruma inakita mizizi yake katika msamaha wa kweli kama unavyojidhihirisha katika historia nzima ya ukombozi wa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti. Huu ni utenzi unaoshuhudia: upendo, neema na hekima inayofumbatwa katika maisha ya Bikira Maria. Utenzi wa Bikira Maria unaonesha mwelekeo mpya kuhusu ulimwengu. Amefanya mambo makuu kwa mkono wake, amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao; Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema, matajiri amewaacha waende mikono mitupu. Ukuu wa Bikira Maria unafumbatwa katika mateso, kwa kukimbilia Misri ili kuokoa maisha ya Mtoto Yesu yaliyokuwa hatarini. Maskini ni amana na utajiri wa Kanisa; watu ambao wako tayari kupokea na kuambata tunu msingi za Kiinjili kwa moyo wa upendo na ukarimu, changamoto kwa waamini kuwa kweli ni matajiri wa imani, tayari kushiriki katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu hapa duniani.

Padre Cantalamessa anaendelea kufafanua kwamba, utenzi wa Bikira Maria unalikumbusha Kanisa wajibu wake wa kinabii wa kutangaza na kushuhudia imani inayomwilishwa katika matendo, kielelezo cha imani tendaji. Utajiri na karama mbali mbali walizokirimiwa waamini zitumike kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu. Ni mwaliko wa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu, kwa kujikita katika Amri ya Upendo kwa Mungu na jirani kama njia ya kujenga udugu wa kibinadamu. Ni changamoto ya watu wa Mungu kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini, njaa na magonjwa duniani; mambo yanayoathiri utu, heshima na haki msingi za binadamu. Kimsingi, “Magnificat” ni muhtasari wa Mafundisho Jamii ya Kanisa, chachu makini ya mchakato wa kuyatakatifuza malimwengu. Kanisa halina budi kuwa na ujasiri wa kinabii ili kusimama kidete kulinda, kutetea utu, heshima na haki msingi za binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Rasilimali na utajiri wa dunia hii vinapaswa kutumiwa kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu katika ujumla wake.

Utenzi wa “Magnificat” anasema Padre Cantalamessa ni shule ya toba na wongofu wa ndani, tayari kuambata na kukumbatia utakatifu wa maisha. Hii ni sala inayopaswa kumwilishwa katika maisha ya kila siku katika hali ya unyenyekevu, sadaka na majitoleo kwa ajili ya huduma kwa Mungu na jirani. Utenzi huu ni chemchemi ya hekima na busara ya Kiinjili; kioo cha toba na wongofu endelevu, ili kuambata huruma na upendo wa Mungu katika maisha. Huruma ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomwajibisha pia mwamini kuwa ni chombo na shuhuda wa huruma na upendo wa Mungu. Haya ni mambo mazito ambayo Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kuyapatia kipaumbele cha pekee katika maisha na utume wa Kanisa, kwani Heri za Mlimani kwa hakika na muhtasari wa Mafundisho ya Kristo Yesu kwa wafuasi wake. Waamini wanahimizwa kuwa na huruma kama Baba yao wa mbinguni alivyo na huruma! Matendo ya huruma: kiroho na kimwili ni ushuhuda wa imani tendaji. Changamoto kwa waamini ni kusoma alama za nyakati ili kutambua aina mpya ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili.

Leo hii kuna wazee wanaoelemewa na upweke hasi, hawa wanahitaji kuona huruma na upendo; kuna watoto na vijana ambao wamekengeuka na kutopea katika malimwengu, hawa pia wanapaswa kuelimishwa, dhamana na wajibu wa kwanza unao paswa kutolewa na wazazi pamoja na walezi. Inasikitisha kuona kwamba, malezi na makuzi ya watoto na vijana, yametelekezwa na kutupiwa kwenye televisheni na kwenye mitandao ya kijamii na matokeo yake ndio hayo yanayoendelea kuwashangaza wazazi na walezi, wanapowaona na kuwasikia watoto wao wakishtumiwa kwa kufanya “mambo ya ovyo ovyo”. Baba Mtakatifu Francisko katika Waraka wake wa Kitume “Misericordia et misera” yaani "Huruma na amani” anasema, hiki ni kipindi cha huruma ya Mungu kinachopania kuwaonjesha maskini na wale wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii: huruma na upendo wa Mungu usiokuwa na mipaka na kwamba, kila mtu anaalikwa kukimbilia na kuambata huruma ya Mungu katika maisha yake. Ni kipindi cha huruma ya Mungu, ili maskini na wanyonge waweze kuangaliwa kwa heshima pamoja na kujali utu na mahitaji yao msingi kwa kuzingatia mambo msingi katika maisha badala ya kugubikwa na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya jirani. Ni muda wa huruma ya Mungu, ili wadhambi waweze kutubu na kumwongokea Mungu.

Ni kipindi cha kujenga na kudumisha utamaduni wa mshikamano, udugu na upendo unaowashirikisha wote bila ubaguzi! Kristo Yesu ni ufunuo wa huruma na upendo wa Mungu unaojidhihirisha kwa binadamu mdhambi kama ilivyokuwa kwa yule mwanamke mzinzi, anayeonesha dhambi na udhaifu wa binadamu. Huruma ni chemchemi ya wokovu wa mwanadamu katika ulimwengu mamboleo. Huruma inakita mizizi yake katika uvumilivu, upole, upendo, kuwajali na kuwathamini wengine. Huruma na upendo ni chachu ya udumifu wa maisha ya ndoa na familia ili kuondokana na kishawishi cha utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Kukosa na kukosehana ni sehemu ya ubinadamu; kusamehe na kusahau ni mwanzo wa utakatifu wa maisha, ndivyo wanavyofundishwa wazee wenye hekima na busara zao. Huruma, upendo na msamaha vipate chimbuko na hitimisho lake kwanza kabisa katika maisha ya ndoa na familia; katika jumuiya za mapadre na watawa; ili tunu hizi msingi ziweze kumwilishwa kwa njia ya ushuhuda wenye mvuto na mashiko katika jamii na familia ya Mungu katika ujumla wake.

Utamaduni wa huruma na upendo unakita mizizi yake katika maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu sanjari na maadhimisho ya mafumbo la Kanisa yanayomwilishwa katika uhalisia wa maisha, kielelezo cha imani tendaji! Kwa ufupi kabisa anasema Padre Raniero Cantalamessa kwamba, Utenzi wa Bikira Maria ni mwelekeo kuhusu Mwenyezi Mungu na ulimwengu katika ujumla wake; ni shule ya toba, wongofu wa ndani; utakatifu wa maisha na uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika katika ushuhuda wenye mvuto na mashiko. Bikira Maria aliyekingizwa dhambi ya asili, akapalizwa mbinguni mwili na roho na hatimaye, kuvikwa taji kama Malkia wa mbingu, anaendelea kuwaombea watoto wake wanaosafiri hapa bondeni kwenye machozi. “Magnificat” ni utenzi wa sifa, ukuu na utukufu wa Fumbo la Utatu Mtakatifu.

UTENZI WA MAMA BIKIRA MARIA: “Magnificat”

Moyo wangu wamtukuza Bwana,

Roho yangu inafurahi*

Kwa sababu ya Mungu mwokozi wangu

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma,

Mtumishi wake mdogo,*

Hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*

Jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*

Hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake*

Amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*

Akawakweza wanyenyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*

Matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israel mtumishi wake,*

Akikumbuka huruma yake,

Kama alivyowaahidia wazee wetu,*

Abrahamu na uzao wake hata milele.

Cantalamessa: Magnificat

 

 

27 August 2019, 10:11