Tafuta

Vatican News
Siku ya Vijana Kimataifa: Mladifest 2019 huko Bosnia na Erzegovina: Kauli mbiu "Njoo Unifuate". Siku ya Vijana Kimataifa: Mladifest 2019 huko Bosnia na Erzegovina: Kauli mbiu "Njoo Unifuate". 

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa: Vijana na Imani!

Maadhimisho ya Siku ya Vijana Kimataifa, Mladifest 2019: Kimekuwa ni kipindi cha shuhuda mbali mbali za maisha na utume wa vijana katika kukabiliana na changamoto mamboleo na hatimaye, wameadhimisha pia Ibada ya Njia ya Msalaba, kwa kuwakumbusha vijana kubeba vyema Misalaba yao na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Changamoto kubwa iliyoko mbele ya vijana wengi ni utupu unaojionesha katika tamaduni kutokana na mawazo hafifu pamoja na kutopea kwa imani, kunakowafanya watu kushindwa kuzamisha maisha yao katika mambo msingi, kiasi cha imani kuonekana kuwa si mali kitu kwa vijana wa kizazi kipya. Baba Mtakatifu Francisko anasikitika kusema, hitimisho la namna hii ni kosa kubwa, kwani leo hii kuna vijana wanaochakarika kutafuta maana ya maisha; vijana wanaojisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya mambo makuu ya maisha. Kuna vijana wanaompenda na wanataka kuambatana na Kristo Yesu; hawa ni vijana wenye upendo mkubwa kwa binadamu. Kuna vijana wanaotafuta furaha, upendo wa kweli, mafanikio na hata utimilifu wa maisha ya ujana wao! Yote haya ni matamanio halali ya vijana wa kizazi kipya, ambayo yanapaswa kuratibiwa kama alivyofanya Mwenyezi Mungu katika kazi ya uumbaji.

Kanisa halina budi kuwasaidia vijana kuratibu na kudhibiti matamanio yao pamoja na kuwawezesha kuwa ni wadau,  kwa kuwapatia nafasi, ili kweli waweze kuchachua matamanio yao! Ulimwengu wa vijana umegawanyika katika sehemu mbali mbali! Kumbe, kunahitajika: ubunifu unaofumbatwa katika wongofu wa kichungaji, ili kuwaonesha mapendekezo ya Kiinjili yanayoweza kuwasaidia kufanya mang’amuzi ya miito yao ndani ya Kanisa. Hati ya Mababa wa Sinodi ya Maaskofu kwa ajili ya Vijana, 2018 pamoja na Wosia wa Kitume: ”Christus vivit” yaani “Kristo anaishi” ni nyaraka muhimu sana zinazoweza kuyasaidia Makanisa mahalia katika sera na mbinu mkakati wa malezi na makuzi ya vijana wa kizazi kipya, ili waweze kujenga umoja na mshikamano na Kristo Yesu, kama mwenza wa safari ya maisha yao!

Maadhimisho ya Siku ya 30 ya Vijana Kimataifa huko Medjugorje nchini Bosnia na Erzegovina kuanzia tarehe 31 Julai hadi tarehe 6 Agosti 2019, Sherehe ya Kung’ara Bwana, yameongozwa na kauli mbiu “Mladifest 2019”: “Njoo unifuate” (Mk. 10:21). Maadhimisho haya yamepambwa kwa Ibada ya Misa Takatifu zilizoongozwa na viongozi mbali mbali wa Kanisa; Katekesi makini kama sehemu ya majiundo endelevu ya vijana wa kizazi kipya, sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Mababa wa Sinodi kuhusu utume wa vijana. Kimekuwa ni kipindi cha shuhuda mbali mbali za maisha na utume wa vijana katika kukabiliana na changamoto mamboleo na hatimaye, wameadhimisha pia Ibada ya Njia ya Msalaba, kwa kuwakumbusha vijana kubeba vyema Misalaba yao na kuanza kumfuasa Kristo Yesu katika maisha ya huduma ya upendo kwa Mungu na jirani!

Askofu mkuu Luigi Pezzuto, Balozi wa Vatican nchini Bosnia na Erzegovina katika mahubiri yake kwa umati wa vijana kutoka sehemu mbali mbali za Bara  la Ulaya alikazia kwa namna ya pekee wito wa Kristo Yesu alioutoa kwa Mitume wake wa kwanza na hatimaye, katika pita pita zake, akakutana na Mathayo Mtoza ushuru, akamwangalia, akampenda na kumchagua kuwa ni kati ya Wafuasi wake wa karibu, tayari kuzama katika mchakato wa kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu. Lakini, ikumbukwe kwamba, Mwenyezi Mungu kadiri ya wema na upendo wake wa daima uliofunuliwa katika historia ya wokovu, alimwita Bikira Maria, akamshirikisha mpango wa ukombozi na Bikira Maria akakubali na kuitikia “Ndiyo” Mimi ni mtumishi wa Bwana na iwe kwangu kama ulivyonena.

Na kwa utii wa Bikira Maria, akawa ni Mama wa Mungu na Kanisa. Akajifunza kutoka kwa Kristo Yesu na kuwa ni mwanafunzi wa kwanza wa Neno wa Mungu aliyefanyika mwili. Kristo Yesu katika maisha na utume wake, alitoa mwaliko kwa baadhi ya wafuasi wake kuwa ni wanafunzi wake wa karibu zaidi, kielelezo cha upendo wa dhati unaooneshwa na kudhihirishwa na Mwana wa Mungu. Bikira Maria katika maisha yake, akajazwa neema na Roho Mtakatifu, tayari kutekeleza mapenzi ya Mungu katika maisha yake. Bikira Maria ni mfano na kielelezo makini cha kufuata kwa kukubali kushiriki katika kazi ya ukombozi. Huu ni mfano pia wa watakatifu wengi sehemu mbali mbali za dunia, ambao, walikubali na kuruhusu mpango wa Mungu katika hija ya maisha yao, kwa kutambua kwamba, Mwenyezi Mungu amewaonesha upendo wa pekee kabisa katika hija ya maisha yao, kwani amewaona na kuwapenda kwa dhati.

Kukubali mpango wa Mungu ni kukubali kuambata upendo wa Mungu katika maisha. Hii ndiyo changamoto inayotolewa na Kristo Yesu kwa kila mwamini hadi leo hii. Askofu mkuu Luigi Pezzuto anasema wito wa kwanza ni utakatifu wa maisha unaomwilishwa katika hija ya maisha ya kila siku kwa njia ya toba na wongofu wa ndani; kwa kufuata kanuni maadili na utu wema; kwa kuonesha huruma na upendo kwa Mungu na jirani. Haya ni mambo ambayo hata vijana wa kizazi kipya wanapaswa kuyamwilisha katika uhalisia wa maisha yao ya kila siku kwani mchakato wa utakatifu ni mapambano endelevu katika maisha. Vijana “wasione sooo” wanapoitwa na Kristo Yesu, kujisadaka kwa ajili ya maisha na utume wa Kanisa, kwani hizi ni dalili kwamba, kwa hakika wanapendwa na kuthaminiwa na Mwenyezi Mungu anayetaka kuwashirikisha katika mpango wa ukombozi.

Wito wa kujisadaka katika maisha ya kitawa na kipadre, iwe ni fursa ya shukrani, furaha na matumaini kwa Mwenyezi Mungu anayeendelea kuwatembelea watu wake na hivyo kuwashirikisha mpango wake wa ukombozi. Hivi ndivyo ilivyokuwa kwa Bikira Maria. Ndiyo ya Bikira Maria ikawa ni chemchemi ya furaha ya walimwengu kwa kuzaliwa kwa Mwana wa Mungu. Vijana wanapaswa kuwa ni mashuhuda na vyombo vya imani kwa watu wanaowazunguka. Ili kufanikisha azma hii, vijana wanapaswa kufundwa barabara katika misingi ya: Imani, Sakramenti za Kanisa, Kanuni na maisha adili pamoja na ujenzi wa utamaduni wa maisha ya sala na tafakari. Kwa kufanya hivi, kwa hakika vijana watakuwa ni chemchemi ya furaha miongoni mwa watu wanaowazunguka.

Bikira Maria ni mfano wa mwamini aliyesheheni furaha kama inavyojionesha katika utenzi wake, “Magnificat”. Ikumbukwe kwamba, imani ni zawadi kutoka kwa Mwenyezi Mungu inayomtaka mwamini kujiaminisha chini ya ulinzi na tunza ya Baba wa milele! Bila imani na kujiaminisha kwa Mungu ni kazi bure kuzungumzia tunu ya imani. Mwenyezi Mungu ni chemchemi ya furaha ya kweli katika maisha ya ujana! Bila tunu msingi za maisha ya kiutu na kimaadili, ujana si mali kitu! Huu ni mwanzo wa kuchuma majanga kwa familia. Mwenyezi Mungu anapenda kuwashirikisha vijana furaha na hatimaye, maisha ya uzima wa milele.

Askofu mkuu Luigi Pezzuto, Balozi wa Vatican nchini Bosnia na Erzegovina, amewapongeza vijana wote waliokuwa wanashiriki katika maadhimisho haya na kuwataka kuendelea kumjifunza Kristo Yesu kwa njia ya shule ya Bikira Maria. Wakuze ibada kwa Bikira Maria Mama wa Mungu na Kanisa na wawasaidie vijana wenzao kukimbilia ulinzi na tunza ya Bikira Maria katika hija ya maisha yao hapa duniani, ili mwishoni, waweze kufika mbinguni. Vijana wawe kweli ni vyombo vya huruma na upendo wa Mungu, ili watu wengi zaidi waweze kupata furaha, uhuru wa kweli na nguvu ya kupambana na changamoto mbali mbali zinazowakabili katika maisha!

Vijana Bosnia 2019

 

08 August 2019, 16:19