Tafuta

Vatican News
UNESCO: Padre Primo Mazzolari alikuwa ni chombo na shuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa na kimataifa! UNESCO: Padre Primo Mazzolari alikuwa ni chombo na shuhuda wa misingi ya haki, amani na upatanisho wa kitaifa na kimataifa!  (AFP or licensors)

UNIESCO: Padre Primo Mazzolari, chombo na shuhuda wa Injili ya amani duniani!

Kardinali Pietro Parolin anasema, hofu ya Mungu na dhamiri nyofu, viwaongoze wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani kwa kujenga uhusiano mwema kati ya haki msingi za binadamu na haki za jumuiya, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hata wanajeshi wanapaswa kuongozwa na dhamiri nyofu.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Padre Primo Mazzolari, wakati wa maisha yake alihubiri na kuishi Injili inayomwilishwa katika maisha ya kila siku ya mwanadamu kadiri ya changamoto na hali halisi za wakati na mahali. Padre Mazzolari alizaliwa kunako mwaka 1890. Baada ya masomo na majiundo yake ya kikasisi akapadrishwa tarehe 24 Agosti 1912, baada ya sadaka na majitoleo makubwa kama chombo na shuhuda wa Injili ya amani, akafariki dunia, tarehe 12 Aprili 1959. Hivi karibuni, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican ameshiriki katika kongamano la kimataifa lililoandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni, UNESCO kwa kuongozwa na kauli mbiu “Ujumbe na matendo ya amani ya Padre Primo Mazzolari” aliyekumbana na mateso pamoja na mahangaiko ya Vita ya Kwanza ya Dunia, akiwa mstari wa mbele kama Padre mshauri wa maisha ya kiroho kwa wanajeshi. Akashuhudia watu wasiokuwa na hatia wakipoteza maisha au kupata majeraha ya kudumu!

Padre Primo Mazzolari akatafakari kwa kina uwiano uliokuwepo kati ya Injili ya amani na vita iliyokuwa inarindima na hatimaye akasema, haki jamii ndiyo silaha pekee inayoweza kujenga na kudumisha misingi ya amani na utulivu! Padre Mazzolari anasema, amani ni msingi wa umoja na udugu kati ya watu wa Mataifa dhidi ya uvunjifu wa haki msingi za binadamu ambao mara nyingi unafumbatwa katika ubaguzi. Vita ni kielelezo cha ukatili wa binadamu, majanga na maafa ya watu wasiokuwa na hatia! Haya ndiyo matokeo ya Vita Kuu ya Pili ya Dunia pamoja na vita inayoendelea hadi sasa sehemu mbali mbali za dunia. Mkristo mbele ya vita anasema, Padre Mazzolari anapaswa kuwa ni shuhuda wa ukweli, uzuri na mafao ya wengi, tayari kusimama kidete kutetea Injili ya uhai dhidi ya utamaduni wa kifo! Hii ni dhamana ya kimaadili inayofumbatwa katika ujenzi wa Ufalme wa Mungu. Hapa kanuni msingi ni: Imani na Haki.

Kardinali Parolin anakaza kusema, hofu ya Mungu na dhamiri nyofu, viwaongoze wakuu wa Jumuiya ya Kimataifa kujikita katika mchakato wa kutafuta, kulinda na kudumisha amani duniani kwa kujenga uhusiano mwema kati ya haki msingi za binadamu na haki za jumuiya, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Hata askari wa vikosi vya ulinzi na usalama wanapaswa kusaidiwa ili kufanya mang’amuzi ya kweli, kwa kuongozwa na dhamiri nyofu iliyofundwa barabara ili kuweza kuchagua mema na kuachana na mabaya.Kwa Mkristo atambue kwamba, anaitwa na kutumwa kuwa ni shuhuda na chombo cha Injili ya amani duniani, wakati wote anapotekeleza dhamana na wajibu wake katika medani mbali mbali za maisha. Msimamo huu, haukumwacha salama hata kidogo, Padre Primo Mazzolari akajikuta mara kwa mara akitupwa gerezani, ili kushikishwa adabu na wapenda vita duniani!

Lakini katika maisha na utume wake, akaendelea kuwa ni shuhuda na chombo cha ujenzi wa amani hata wakati wa Vita Baridi, dunia ilipogawanywa katika makundi makuu mawili: Ubepari na Ukomunisti na nchi maskini zilizokuwa zinaibukia uhuru zikajikuta ziko njiapanda na ukakasi wa Vita Baridi bado unazipekenyua baadhi ya nchi kwa kuendekeza vita ya wenyewe kwa wenyewe! Kardinali Parolin anaendelea kufafanua kwamba, ujenzi wa amani ni wito wa kweli wa binadamu na wala hakuna vita halali duniani! “Dhana ya vita halali imepitwa na wakati” huu ni muda muafaka wa kujenga kanuni maadili zinazolenga kukuza na kudumisha misingi ya haki na amani, ili kupambana na vita pamoja na mauaji ya kimbari.  Baba Mtakatifu Francisko anasema, huruma ni chemchemi ya furaha, amani na utulivu wa ndani, unaopaswa kukita mizizi yake katika sakafu ya moyo wa mwanadamu; kwa mwelekeo huu, amani inakuwa ni chachu ya upatanisho kati ya watu wa Mataifa.

Amani ni changamoto kubwa katika ulimwengu mamboleo unaoendelea kuogelea katika vita, kinzani na mipasuko mbali mbali ya kijamii! Vita ni chanzo kikuu cha umaskini, magonjwa na majanga katika maisha ya mwanadamu; lakini amani ni utamaduni unaodumisha Injili ya uhai, ustawi na maendeleo ya wengi. Silaha za vita na maangamizi ni kielelezo cha matumizi mabaya ya rasilimali fedha ambayo ingeweza kutumika kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi na badala yake zinakuwa ni chanzo cha maafa. Amani ni amana na wajibu kwa watu wote wenye mapenzi mema kwani vita haina macho wala pazia! Hakuna kinachoweza kupotea kwa njia ya amani, lakini vita ni chanzo cha uharibifu mkubwa wa maisha ya binadamu! Amani ya kweli inapata chimbuko lake kutoka katika sakafu ya maisha ya mwanadamu!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anasema, wajenzi wa amani ya kweli duniani wanaweza kupata changamoto endelevu kutokana na mchango uliotolewa na Padre Primo Mazzolari, aliyesimama kidete kutetea na kudumisha utu na heshima ya binadamu kwa kukataa dhana ya vita katika maisha ya mwanadamu kwa macho meupe pe! Pasi na kupepesa hata kidogo, mfano bora wa kuigwa na viongozi wa Jumuiya ya Kimataifa, kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!

Kardinali Parolin: UNESCO
08 August 2019, 14:21