Tafuta

Vatican News
Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu "Mpanzi wa amani na matumaini" Hija ya Papa Francisko nchini Madagascar inaongozwa na kauli mbiu "Mpanzi wa amani na matumaini"  (AFP or licensors)

Hija ya Baba Mtakatifu Francisko Madagascar: Mpanzi wa amani na matumaini!

Papa Francisko kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 anafanya hija ya kitume Barani Afrika kwa kutembelea: Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anatarajiwa kufanya hija ya kitume Barani Afrika kuanzia tarehe 4-10 Septemba 2019 kwa kutembelea Msumbiji, Madagascar pamoja na Mauritius. Kauli mbiu inayoongoza hija ya Baba Mtakatifu nchini Msumbiji ni: matumaini, amani na upatanisho. Upande wa Madagascar ni “Mpanzi wa amani na matumaini na kauli mbiu ya familia ya Mungu nchini Mauritius ni “Hujaji wa amani”. Bara la Afrika kwa sasa lina kiu kubwa ya: haki, amani, upatanisho na matumaini ya kuweza kuanza upya na kusonga mbele kwa imani na matumaini thabiti pasi na kukata tamaa hasa baada ya matukio ya vita, ghasia, kinzani na majanga asilia ambayo yamelikumba Bara la Afrika kwa siku za hivi karibuni!

Kardinali Juan Josè Omella, Askofu mkuu wa Jimbo kuu la Barcelona, Hispania, hivi karibuni alipata fursa ya kutembelea na kutoa mafungo ya kiroho kwa wakleri wa Jimbo Katoliki la Ambanja linaloongozwa na Askofu Rosario Saro Vella, mmisionari kutoka Italia, ambaye ameyasadaka maisha yake kwa takribani miaka thelathini ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa wananchi wa Madagascar. Katika safari hii ya kichungaji ameshuhudia mateso, mahangaiko ya watu wa Mungu; furaha na matumaini yanayobubujika kutoka kwa Kristo na Kanisa lake. Licha ya umaskini wa hali na kipato, lakini bado wananchi wa Madagascar wanapendeza na ni watu wenye furaha inayotanda mbele ya nyuso zao, kama “umande wa asubuhi”.

Kardinali Juan Josè Omella amepata nafasi ya kukutana na kuzungumza na wananchi wa Madagascar ambayo kimsingi ina utajiri mkubwa wa rasilimali na maliasili, lakini bado utajiri huu unaendelea kuwanufaisha watu wachache katika jamii. Kuna kundi kubwa la wananchi bado linaogelea katika umaskini wa hali na kipato! Madagascar imebahatika kuzungukwa na eneo kubwa la maji na misitu asilia; changamoto kwa wananchi wa Madagascar kuendelea kulinda na kutunza mazingira nyumba ya wote, ili watu wengi zaidi waweze kufaidika na kazi hii ya uumbaji! Haya ni mazingira ambamo mtu anaweza kupata amani na utulivu wa ndani kutokana na ukimya wake, hasa kwa watu ambao wanatoka kwenye maeneo yenye kelele, vurugu na patashika nguo kuchanika kutokana uchafuzi wa mazingira na kelele za mijini.

Kardinali Omella amefurahishwa na ukarimu na upendo unaooneshwa na wananchi wa Madagascar, kielelezo cha maadili na utu wema na kwamba, binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu anapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa. Wenyeji walipoona kundi la wakleri limesimama barabarani, walifika kuulizia kama walikuwa wanahitaji msaada wowote kutoka kwao, jambo ambalo limemfurahisha sana Kardinali Juan Josè Omella kuona jinsi watu wa Magascar wanavyojaliana hata katika umaskini wao. Ameguswa kwa namna ya pekee kabisa, na ushuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, kwa kuheshimu maadhimisho ya Mafumbo ya Kanisa; kwa kuwa na ushiriki mkamilifu, changamoto iliyotolewa na Mababa wa Mtaguso Mkuu wa Pili wa Vatican.

Majadiliano ya kidini na kiekumene ni sehemu ya vinasaba vya maisha yao na chachu ya kukuza na kukoleza mafungamano ya kijamii. Ameshunudia Injili ya upendo inavyomwilishwa katika huduma kwa wagonjwa na wazee; watoto yatima na wale wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, kielelezo cha imani tendaji. Ametembelea na kuwaona watawa wanavyojisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake, kama sehemu ya mchakato wa uinjilishaji mpya unaofumbatwa katika ushuhuda wa maisha! Licha ya rushwa na ufisadi; umaskini na ukosefu wa fursa za ajira kwa vijana wengi, waamini wengi wameendelea kuwa ni chachu ya matumaini hata katika mazingira magumu na tete kiasi hiki, ili kuwarejeshea watu: utu na heshima yao kwa njia ya huduma ya elimu, afya na ustawi wa jamii. Wamisionari wanahitaji kuoneshwa na kuonjeshwa moyo wa ushirikiano na mshikamano kwa ajili ya ustawi, maendeleo na mafao ya watu wa Mungu wanaowahudumia.

Ushirikiano huu, unaweza kufumbwa kwa namna ya pekee katika mambo makuu matatu: ushirikiano katika maisha ya kiroho kwa njia ya sala na sadaka, ili kweli kazi ya uinjilishaji iweze kuzaa matunda ya toba na wongofu wa ndani, ili ulimwengu uweze kuwa ni mahali pazuri zaidi pa kuishi. Pili, ni ushirikiano kwa njia ya rasilimali watu. Huu ni mwaliko kwa vijana wanaojisikia kuwa na wito wa kipadre na kitawa, wasisite kuacha yote na kumfuasa Kristo ili kutangaza na kushuhudia Habari Njema ya Wokovu kwa watu wa mataifa! Vijana watambue kwamba, kuna furaha na heri kubwa sana kutoa kuliko kupokea! Vijana wanahamasishwa kuthubutu kujisadaka kwa ajili ya Kristo na Kanisa lake. Tatu, ni ushirikiano wa rasilimali fedha na vitu, kama mchakato wa maboresho ya huduma za jamii na mapambano dhidi ya umaskini wa hali na kipato, kielelezo makini cha uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji ya mtu mzima: kiroho na kimwili.

Kardinali Juan Josè Omella anakaza kusema, Kanisa lipo kwa ajili ya kuinjilisha pamoja na kupambana na ukosefu wa haki jamii, ili kweli rasilimali na utajiri wa Madagascar na Afrika katika ujumla wake, uweze kusaidia mchakato wa maboresho ya maisha ya familia ya Mungu Barani Afrika, kuliko mtindo wa sasa wa Makampuni na Mashirika makubwa ya Kimataifa kuendelea kukwapua rasilimali na utajiri wa Bara la Afrika. Kuna haja ya kuwekeza katika sekta ya uchumi, elimu na afya, ili kupambana na umaskini, ujinga na maradhi. Ushirikiano na mshikamano kati ya Madagascar na watu wenye mapenzi mema, usaidie utunzaji bora wa mazingira ili kupambana na athari za mabadiliko ya tabianchi yanayoendelea kuwatumbukiza watu wengi katika maafa makubwa.

Uinjilishaji Madagascar
08 August 2019, 15:29