Tafuta

Vatican News
Diplomasia ya Vatican na Papa Francisko inasimikwa katika: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Diplomasia ya Vatican na Papa Francisko inasimikwa katika: Utu, heshima, haki msingi za binadamu; Ustawi, maendeleo na mafao ya wengi!  (AFP or licensors)

Kardinali Parolin: Diplomasia ya Vatican & Papa Francisko

Diplomasia ya Baba Mtakatifu Francisko inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali ya dunia inafumbatwa katika: Utu, heshima na haki msingi za binadamu. Lengo ni kukuza na kudumisha mapambano dhidi ya umaskini, uharibifu wa mazingira nyumba ya wote pamoja na kuimarisha misingi ya amani, mshikamano na maridhiano kati ya watu, kwa wanategemeana na kukamilishana.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dhana ya diplomasia ya Vatican inafumbatwa katika amani, kwa kusimama kidete kupambana na baa la njaa na umaskini duniani; kwa kulinda na kutunza mazingira bora nyumba ya wote kwani kuna mamilioni ya watu wanaoathirika kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na ukosefu wa fursa za ajira na maendeleo fungamani! Baba Mtakatifu Francisko anawataka waamini pamoja na watu wote wenye mapenzi mema kuwa ni mashuhuda na wajenzi wa misingi ya haki, amani, upendo na mshikamano wa kidugu, ili kuweza kukabiliana na changamoto katika ulimwengu mamboleo. Mataifa yatambue kwamba, yanategemeana na kukamilishana na kwamba, binadamu ni kiumbe jamii. Kwa njia, hii, Jumuiya ya Kimataifa inaweza kuwa ni alama ya matumaini kwa wale waliokata tamaa ya maisha kutokana na sababu mbali mbali.

Baba Mtakatifu Francisko katika mchakato wa kidiplomasia na uhusiano wa mambo ya nchi za nje na ushirikiano wa kimataifa anakazia kwa namna ya pekee: Mosi, umuhimu wa kushirikiana na kushikamana katika mapambano dhidi ya umaskini unaodhalilisha utu na heshima ya binadamu sehemu mbali mbali za dunia. Jambo la pili, ni uhamasishaji wa familia ya binadamu kujenga na kudumisha madaraja ya watu kukutana na kusaidiana, ili kujenga na kuimarisha: haki, umoja na udugu wa kibinadamu ili kuondokana na utandawazi usiojali wala kuguswa na mahangaiko ya wengine. Vatican inakazia: ujenzi wa utamaduni wa majadiliano katika ukweli na uwazi, ili kutatua migogoro ya kivita, mipasuko, kinzani na changamoto mbali mbali zinazoendelea kujitokeza katika uso wa dunia!

Lengo la diplomasia ya Vatican ni kukuza na kudumisha mchakato wa ujenzi wa utamaduni wa amani duniani. Katika sehemu hii, Vatican imekuwa ni sauti ya kinabii na hasa zaidi sauti ya watu wasiokuwa na sauti! Jumuiya ya Kimataifa inahamasishwa kusimama kidete kulinda, kutetea na kudumisha haki msingi za binadamu, uhuru wa kuabudu, utu na heshima ya binadamu wote bila ubaguzi. Ikiwa kama Jumuiya ya Kimataifa inataka kupata maendeleo ya kweli na endelevu, basi binadamu anapaswa kupewa kipaumbele cha kwanza katika sera na mikakati ya maendeleo fungamani! Kanisa linapenda kudumisha mchakato wa haki, amani, utulivu na maridhiano kwa kuzimisha moto wa machafuko, kinzani na vita kwa maji ya baraka, majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kuzingatia ustawi, maendeleo na mafao ya wengi.

Ni mchakato wa majadiliano ya kidiplomasia unaojikita katika kubainisha mbinu mkakati wa mawasiliano, vikwazo na vizingiziti vinavyoweza kujitokeza pamoja na kuunda mazingira ya kuaminiana na kuthaminiana, ili kuendeleza majadiliano. Diplomasia inayotekelezwa na Vatican sehemu mbali mbali za dunia inajikita kwa namna ya pekee, katika msingi wa haki, amani na maridhiano kati ya watu! Ni diplomasia inayojipambanua kwa kusimama kidete: kulinda, kutetea na kudumisha utu, heshima, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi! Ni katika muktadha huu, Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican, hivi karibuni, katika mahojiano maalum kama sehemu ya maadhimisho ya Siku kuu ya “Avvenire, huko Matera” nchini Italia amekazia kuhusu mambo msingi yanayozingatiwa na Diplomasia ya Vatican pamoja na Baba Mtakatifu Francisko.

Baba Mtakatifu ni kiongozi anayependa kuona kwamba, diplomasia inagusa watu wa kawaida: maskini, wagonjwa, wazee, watoto, wakimbizi na wahamiaji; watu ambao hawana sauti hata kidogo katika ulimwengu wa utandawazi na maendeleo ya sayansi na teknolojia. Utu, heshima na haki msingi za binadamu ni mambo ambayo yanapaswa kupewa uzito unaostahili. Diplomasia ya Vatican inakita mizizi yake katika tunu msingi za Kiinjili, kama chombo muhimu cha kutekeleza maisha na utume wa Kanisa katika Jumuiya ya Kimataifa. Kardinali Parolin anakaza kusema, licha ya nia njema, ustawi, maendeleo na mafao ya wengi yanayokusudiwa katika sera na mikakati mbali mbali inayotekelezwa kuanzia na Baba Mtakatifu mwenyewe pamoja na Vatican, kumekuwepo pia na shutuma dhidi ya Vatican, kwa mfano, utekelezaji wa maagizo ya Baraza la Makardinali kuhusu umuhimu wa kupyaisha Sekretarieti kuu ya Vatican; na Uhusiano wa Vatican na China kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia!

Lakini yote haya yanaonesha uhuru wa watu kutoa maoni yao kama kielelezo cha tofauti msingi katika maisha ya binadamu, lakini kwa mambo makubwa na mazito, umoja na mshikamano unahitajika sana! Kuhusu uteuzi wa Maaskofu mahalia nchini China anasema Baba Mtakatifu Francisko ni safari inayohitaji uvumilivu na subira, kama ilivyokuwa hivi karibini, Maaskofu wawili kutoka China walishiriki maadhimisho ya Sinodi ya Maaskofu kuhusu vijana, iliyofanyika mjini Vatican, Mwezi Oktoba 2018. Kanisa linaendelea kufanya upembuzi yakinifu ili kupata majina ya Wakleri watakaoweza kuteuliwa kuziba nafasi za Maaskofu katika majimbo ambayo yako wazi kwa sasa. Bado kuna matatizo na changamoto pevu, ndiyo maana hivi karibuni Vatican imechapisha Mwongozo wa Shughuli za Kichungaji nchini China, utakaowawezesha waamini kuwa ni raia wema na wachamungu; kwa kuheshimu sheria za nchi pamoja na kuhakikisha kwamba, wanakuwa ni mashuhuda wa imani inayomwilishwa katika matendo, daima wakiwa wameunganika na Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Kwa maneno mengine, Kanisa linaomba fursa ya kuweza kutekeleza dhamana yake ya kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu bila kuingiliwa na Serikali. Makubaliano kuhusu uteuzi wa Maaskofu ni hatua kubwa katika kujenga mahusiano ya kidiplomasia na China. Rais Vladimir Putin wa Urussi, Alhamis,  tarehe 4 Julai 2019 anakutana na Baba Mtakatifu Francisko kwa mara ya tatu. Ni kiongozi mchamungu anayetambua karama, utume na dhamana ya Khalifa wa Mtakatifu Petro katika mchakato wa kukuza na kudumisha misingi ya haki, amani na maridhiano kati ya watu. Vita, kinzani na mipasuko huko Mashariki ya Kati pamoja na kumong’onyoka kwa kanuni maadili na utu wema hususan Barani Ulaya ni mambo ambayo yanaweza kuzungumziwa na viongozi wa pande hizi mbili.

Ziara ya Rais Putin wa Urussi ni muda muafaka kwa Vatican kuweza kujadiliana naye kuhusu mambo msingi yanayopewa kipaumbele cha pekee kwenye Diplomasia ya Vatican, kwa mfano hali ya Syria na vita huko nchini Ukraine. Vatican inaendelea kuunga mkono dhana ya Serikali mbili huko kwenye Nchi Takatifu yaani Serikali ya Israeli na Serikali ya Palestina. Kwa bahati mbaya eneo hili limekuwa ni sababu ya kinzani na mipasuko mikubwa kwa Jumuiya ya Kimataifa kwa baadhi ya nchi kukumbatia masilahi ya kiuchumi zaidi. Kardinali Pietro Parolin anasema, Hati ya Udugu wa Kibinadamu inawataka waamini kujikita katika kutenda mema; kuendeleza na kudumisha majadiliano ya kidini; kwa kuheshimiana na kuthaminiana kama ndugu wamoja, licha ya tofauti zao msingi. Waamini wawe na ujasiri wa kushirikiana na kushikamana kwa ajili ya huduma kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii.

Baba Mtakatifu Francisko na Dr. Ahmad Al-Tayyib, Imam Mkuu wa Msikiti wa Al- Azhar, wameonesha dira na mwongozo wa hija ya: haki, amani na upatanisho miongoni mwa waamini wa dini mbali mbali. Hii ni dhamana inayowafumbata na kuwaunganisha watu wote wenye mapenzi mema, daima wakijitahidi kuongozwa na dhamiri nyofu. Lengo ni kujenga mazingira yatakayowawezesha watu kuishi katika ulimwengu unaosimikwa katika haki, upendo na mshikamano. Huu ni mwaliko wa kuondokana na kufuru ya kutumia jina la Mwenyezi Mungu kwa ajili ya mafao binafsi, sababu za kuanzisha vita, ghasia, chuki na mipasuko ya kijamii. Maisha ni zawadi kubwa kutoka kwa Mwenyezi Mungu inapaswa kulindwa, kuheshimiwa na kuendelezwa na wote. Huu ni mwanzo wa ujenzi wa utamaduni wa watu kukutana, ili kuimarisha madaraja ya amani kati ya watu wa Mataifa; kizazi cha sasa na kile kijacho!

Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican anakaza kusema, hija za kitume za Baba Mtakatifu Francisko zinajikita hasa katika kukuza na kudumisha majadiliano ya kidini na kiekumene kama ilivyoshuhudiwa katika hija za Baba Mtakatifu nchini Morocco na kwenye Nchi za Umoja wa Falme za Kiarabu, Bulgaria, Macedonia ya Kaskazini pamoja na Romania. Baba Mtakatifu anapenda kuimarisha imani, matumaini na mapendo ya watu wa Mungu; hasa wale wanaoteseka kutokana na sababu mbali mbali. Ndiyo maana Baba Mtakatifu anatamani sana kutembelea Sudan ya Kusini na Iraq, ili aweze kuwaimarisha ndugu zake katika imani, matumaini na mapendo. Baba Mtakatifu anatamani kutembelea Japan, lengo ni kusaidia mchakato wa kudhibiti silaha za maangamizi zinazotishia amani, usalama na ustawi wa familia ya Mungu sehemu mbali mbali za dunia.

Kardinali Pietro Parolin kuhusu sera na mikakati ya kisiasa nchini Italia anapenda zaidi kuona kwamba, utu, heshima, haki msingi za binadamu; upendo na mshikamano wa dhati kwa maskini, wakimbizi na wahamiaji zinaimarishwa kama sehemu ya utekelezaji wa Mafundisho Jamii ya Kanisa katika uhalisia wa maisha ya watu! Kama ilivyo katika Jumuiya ya Ulaya, ukarimu ni fadhila inapaswa kukuzwa na kudumishwa na wote. Waamini walei wawe mstari wa mbele katika kuyatakatifuza malimwengu kwa njia ya ushiriki wao katika masuala ya kisiasa. Mkataba wa Kimataifa wa Usalama wa Wahamiaji wa mwaka 2018, yaani “Global Compact 2018”, unalenga kuratibu na kuboresha mchakato wa wahamiaji na wakimbizi duniani, ili kulinda na kudumisha haki msingi, utu na heshima ya wahamiaji!

Mkataba huu unakazia umuhimu wa jamii kusikiliza na kujibu kilio cha wakimbizi na wahamiaji duniani; kwa kukusanya maoni; kwa kupunguza gharama za kuwahudumia wahamiaji sanjari na kudumisha usalama na kuendeleza mchakato wa maboresho ya maisha yao wanapokuwa ugenini! Ushirikiano wa Jumuiya ya Kimataifa katika kukabiliana na wimbi kubwa la wakimbizi na wahamiaji ni muhimu sana kwa wakati huu. Kardinali Parolin anasema, Sinodi ya Maaskofu Ukanda wa Amazonia itajikita katika mambo makuu mawili: mchakato wa utume wa Kanisa katika uinjilishaji wa kina unaogusa mahitaji msingi ya binadamu: kiroho na kimwili pamoja na ekolojia fungamani. Hizi ni nyanja mbili tofauti, lakini zinategemeana kukamilishana katika uhalisia wa maisha ya watu ukanda wa Amazonia! Hili ni tukio la Kikanisa linalopania pia kukuza na kudumisha ustawi, maendeleo na mafao ya familia ya Mungu duniani!

Kardinali Parolin anahitimisha mahojiano haya kwa kusema kwamba, hali ya Venezuela inaendelea kuwa tata kiasi cha kuonekana kana kwamba, Jumuiya ya Kimataifa imeshindwa kupata ufumbuzi wa tatizo la mpasuko wa kisiasa nchini Venezuela. Kuna mapendekezo mengi ambayo yanaendelea kufanyiwa kazi, lakini jambo la msingi kwa sasa ni hekima na busara; ujasiri na utashi wa kisiasa, kwa ajili ya kutafuta na hatimaye kudumisha utu, heshima, haki msingi za binadamu; ustawi, maendeleo na mafao ya wengi. Vatican inaendelea kuisindikiza familia ya Mungu nchini Venezuela, ili hatimaye, amani na utulivu viweze kurejea tena miongoni mwa watu!

Kard. Parolin: Diplomasia
03 July 2019, 15:52