Tafuta

Vatican News
Hospitali ya Bambino Gesù imetiliana sahihi Mkataba wa Ushirikiano katika huduma ya afya na tiba kwa watoto wadodgo na Serikali ya Equador: Mkazo: Mafunzo na tafiti. Hospitali ya Bambino Gesù imetiliana sahihi Mkataba wa Ushirikiano katika huduma ya afya na tiba kwa watoto wadodgo na Serikali ya Equador: Mkazo: Mafunzo na tafiti. 

Hospitali ya Bambino Gesù & Equador kushirikiana kwa huduma ya watoto wagonjwa: Mafunzo & Tafiti

Mkataba wa Ushirikiano wa huduma, maendeleo ya kitabibu na tafiti kwa watoto wagonjwa nchini Equador, umewekwa sahihi na Mariela Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na Rocio Gonzàlez de Moreno aliyeongoza ujumbe wa Equador. Lengo ni kuendelea kutoa ushuhuda wa mshikamano wa huduma ya upendo kwa watoto wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya jamii.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Hospitali ya Bambino Gesù inayomilikiwa na kuendeshwa na Vatican, ilianzishwa kunako mwaka 1869 kama Hospitali ya kwanza kwa ajili ya watoto wagonjwa nchini Italia. Kunako mwaka 1924, familia ya Jacqueline Arabela de Fitz-James Salviati wamiliki wa Hospitali hii wakatoa zawadi kwa Vatican na kupokelewa na Papa Pio IX. Tangu wakati huo ikaanza kufahamika kama Hospitali ya Bambino Gesù, Hospitali ya Papa kwa ajili ya watoto wagonjwa. Huduma kwa watoto wagonjwa na maskini anasema Papa Pio XI ni sehemu ya vinasaba vya maisha na utume wa Khalifa wa Mtakatifu Petro.

Hivi karibuni, Hospitali ya Bambino Gesù imewekeana sahihi Mkataba wa Ushirikiano wa huduma, maendeleo ya kitabibu pamoja tafiti makini za sayansi ya tiba kwa watoto wagonjwa nchini Equador “Memorandum of Understanding, MOU”. Mkataba huu ni mwendelezo wa jitihada za Hospitali hii kuendelea kushiriki katika maboresho ya huduma ya afya kwa watoto sehemu mbali mbali za dunia. Hadi sasa Hospitali hii imekwisha kuwekeana Mkataba na nchi ya Jamhuri ya Watu wa Afrika ya Kati, Tanzania na Hospitali ya Rufaa ya Mtakatifu Gaspar, Itigi, Singida, Ethiopia, Siria, Yordan Cambordia, India na China.

Mkataba wa Ushirikiano wa huduma, maendeleo ya kitabibu pamoja tafiti makini za sayansi ya tiba kwa watoto wagonjwa nchini Equador, umewekwa sahihi na Mama Mariela Enoc, Rais wa Hospitali ya Bambino Gesù pamoja na Rocio Gonzàlez de Moreno, “First Lady” aliyeongoza ujumbe kutoka Equador. Lengo kuu ni kuendelea kutoa ushuhuda wa mshikamano wa huduma ya upendo kwa watoto wanaoishi pembezoni mwa vipaumbele vya jamii. Hii itakuwa ni fursa ya kuweza kubadilisha ujuzi, uzoefu na matunda ya tafiti mbali mbali kuhusu maboresho ya huduma ya afya kwa watoto wadogo nchini Equador.

Mkazo ni mafunzo endelevu, ili kuwajengea madaktari uwezo wa kupambana na changamoto mamboleo za afya ya watoto zinazoendelea kuibuka kila kukicha kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi na umaskini. Mama Mariella Enoc amekumbusha kwamba wanapenda kushirikisha ujuzi, maarifa, weledi na kanuni maadili katika huduma ya afya kwa watoto wadogo. Ili kufanikisha azma hii, kuna haja ya kuwekeza zaidi katika mafunzo ya madaktari. Ujumbe wa Rocio Gonzàlez de Moreno umepata nafasi ya kutembelea na kuangalia shughuli mbali mbali zinazoendeshwa na Hospitali ya Bambino Gesù.

Vatican: Equador

 

 

12 July 2019, 15:31