Tafuta

Vatican News
Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa Muda wa Vatican anahitimisha kazi yake rasmi tarehe 21 Julai 2019. Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa Muda wa Vatican anahitimisha kazi yake rasmi tarehe 21 Julai 2019.  (ANSA)

Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa mapito, amaliza muda wake wa kazi

Dr. Alessandro Gisotti anamshukuru Papa, viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kuheshimu utashi na uamuzi wake wa kutekeleza dhamana hii kwa muda mfupi. Tangu tarehe 31 Desemba 2018 alipoteuliwa kuwa Msemaji mkuu wa muda ametekeleza wajibu wake kwa utulivu, baada ya wasemaji wakuu kujuzulu kwa ghafla.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Dr. Alessandro Gisotti, Msemaji mkuu wa mpito mjini Vatican, anayemaliza muda wake rasmi tarehe 21 Julai 2019, katika tamko lake, anapenda kuchukua fursa hii, kumshukuru Baba Mtakatifu Francisko kwa kumwamini na kumpatia dhamana ya kuwa Msemaji mkuu wa muda wa Vatican katika kipindi ambacho kimekuwa na shughuli nyingi. Anapenda kumshukuru pia kwa kumteuwa kuwa ni Mhariri mkuu msaidizi, Idara ya Uchapaji ya Baraza la Kipapa la Mawasiliano. Anamshukuru Baba Mtakatifu kwa kumwongoza vyema kama mtoto wake. Dr. Alessandro Gisotti anamshukuru Baba Mtakatifu, viongozi wakuu wa Sekretarieti kuu ya Vatican pamoja na Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kuheshimu utashi na uamuzi wake wa kutekeleza dhamana hii kwa muda mfupi.

Tangu tarehe 31 Desemba 2018 alipoteuliwa kuwa Msemaji mkuu wa muda amejitahidi kutekeleza dhamana na wajibu wake kwa amani na utulivu, baada ya wasemaji wakuu kujuzulu kwa ghafla. Anamshukuru na kumpongeza Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano pamoja na wafanyakazi wote wa Ofisi ya Msemaji mkuu wa Vatican kwa ushirikiano na mshikamano waliokuwa nao wakati wote wa uongozi wake. Kukosa na kukoseana ni ubinadamu, kusamehe na kusahau ni kuanza hija ya utakatifu wa maisha. Katika kipindi chake cha uongozi, wamemkumbuka kwa heshima na taadhima Dr. Joaquin Navarro Valls aliyejisadaka kama Msemaji mkuu wa Vatican wakati wa uongozi wa Mtakatifu Yohane Paulo II na mwanzoni mwa utume wa Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto XVI.

Hii inaonesha kwamba, mawasiliano ni muhimu na yataendelea kuwa muhimu katika maisha na utume wa Kanisa. Anamtakia kila la heri na baraka tele Dr. Matteo Bruni kwa kuteuliwa na Baba Mtakatifu kuwa ni Msemaji mkuu wa Vatican. Yupo tayari kushirikiana naye wakati wowote atakapomhitaji!

Dr. Gisotti
18 July 2019, 15:06