Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewatembelea Masista wa huruma wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo, "Casa Regina Mundi Roma". Baba Mtakatifu Francisko hivi karibuni amewatembelea Masista wa huruma wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo, "Casa Regina Mundi Roma". 

Papa Francisko awatembelea Masista wa Mtakatifu Vincent wa Paulo! Wapigwa bumbuwazi!

Hivi karibuni Papa Francisko amemtembelea Sr. Maria Mucci ambaye kwa miaka mingi amekuwa akitoa huduma katika Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican, ambayo kwa sasa Baba Mtakatifu anaitumia kama makazi yake. Kwa sasa Sr. Maria Mucci mwenye umri wa miaka 74, amelazwa kwenye nyumba ya Kanda ya Masista wa Mtakatifu Vincent wa Paulo hapa Roma. Utu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko anaendelea kutumia kipindi hiki cha likizo ya kiangazi kwa ajili ya matendo ya huruma: kiroho na kimwili kama sehemu na mwendelezo wa maadhimisho ya Mwaka Mtakatifu wa Jubilei ya Huruma ya Mungu. Hivi karibuni, Baba Mtakatifu aliwatembelea Masista wa huruma wa Shirika la Mtakatifu Vincent wa Paulo waliko kwenye nyumba ya “Casa Regina Mundi” iliyoko mjini Roma. Lengo la ziara hii binafsi, lilikuwa ni kwenda kumtembelea na kumwamkia Sr. Maria Mucci ambaye kwa miaka mingi amekuwa akitoa huduma katika Hosteli ya Mtakatifu Martha iliyoko mjini Vatican, ambayo kwa sasa Baba Mtakatifu Francisko anaitumia kama makazi yake.

Kwa sasa Sr. Maria Mucci mwenye umri wa miaka 74, amelazwa kwenye nyumba ya Kanda ya Masista wa Mtakatifu Vincent wa Paulo hapa Roma. Sr. Mucci alianza kutoa huduma kwenye Hosteli ya Mtakatifu Martha hata kabla ya kuweka nadhiri zake za kitawa. Katika siku za hivi karibuni, alihamishiwa jikoni na yeye ndiye aliyekuwa mtaalam wa kuhakikisha kwamba, Baba Mtakatifu Francisko anapata lishe bora na kwa wakati, ili aweze kutekeleza vyema utume wake wa kufundisha, kuongoza na kuwatakatifuza watu wa Mungu. Mwezi Oktoba 2018 Sr. Maria Mucci alifanyiwa operesheni kubwa ambayo hadi wakati huu, imemlazimisha kuendelea kulala kitandani, huku akiendelea na matibabu zaidi.

Ni katika muktadha wa moyo wa shukrani, upendo na unyenyekevu pamoja na kuthamini huduma Sr. Maria Mucci si tu anapokuwa jikoni, bali hata katika maisha yake ya sala, Baba Mtakatifu Francisko ameamua kwenda kumtembelea Sr. Maria Mucci. Kwa mshangao mkubwa, Sr. Maria Mucci alipomwona Baba Mtakatifu mbele yake, aliwaambia Masista wenzake kwamba, anamshukuru Mungu kwa ugonjwa wake, ambao umemsukuma hata Baba Mtakatifu Francisko kwenda kuwatembelea wote katika ujumla wao. Baba Mtakatifu akiwa nyumbani humo, alijionea mwenyewe tisheti iliyokuwa na mabaka ya damu ya Mtakatifu Yohane Paulo II, siku ile alipo shambuliwa kwa risasi kwenye uwanja wa Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican. Mara baada ya ziara hii fupi, Baba Mtakatifu Francisko aliwabariki watawa, wafanyakazi pamoja na wageni wote waliokuwemo kwenye nyumba hii!

Papa: Sr. Mucco

 

 

31 July 2019, 12:08