Tafuta

Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki linafanyika mjini Roma kuanzia tarehe 26-29 Juni 2019: Kauli mbiu: Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali. Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki linafanyika mjini Roma kuanzia tarehe 26-29 Juni 2019: Kauli mbiu: Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali. 

Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki 2019: Roma!

Kuanzia tarehe 26 Juni hadi 29 Juni 2019, Kanisa linaadhimisha Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki zinazoongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali”. Huu ni muda muafaka wa kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kadiri ya maeneo ya kijiografia mintarafu teknolojia ya kidigitali.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Mawasiliano kwa kushirikiana na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Baraza la Maaskofu Katoliki Italia, kuanzia Jumatano tarehe 26 Juni hadi 29 Juni 2019 linaadhimisha Kongamano la Siku za Kimataifa za Machapisho ya Kikatoliki zinazoongozwa na kauli mbiu “Tufanye kazi kwa pamoja ili kukabiliana na changamoto za kidigitali”. Huu ni muda muafaka wa kushirikishana uzoefu, mang’amuzi na changamoto mbali mbali zinazojitokeza kadiri ya maeneo ya kijiografia mintarafu teknolojia ya kidigitali.

Wajumbe watapata fursa ya kujadiliana pamoja na kufanya kazi kwa makundi, ili hatimaye, kuibuka na mbinu mkakati wa machapisho ya Kikatoliki, kwa endelea kusoma alama za nyakati kutokana na mabadiliko makubwa ya watumiaji wa mifumo ya mawasiliano ya kijamii, hali ya uchumi pamoja na soko la kidigitali. Kongamano hili linahudhuria na wadau kutoka katika viwanda 50 vya uchapaji vinavyosimamiwa na kuendeshwa na Kanisa Katoliki sehemu mbali mbali za dunia. Kati ya wawezeshaji wakuu ni pamoja na: Dr. Paolo Ruffini, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano, Fra Giulio Cesareo, O.F.M. Conv. Mkurugenzi wa Kitengo cha Uchapaji cha Vatican, LEV.

Wamo pia akina Padre Marko Ivan Rupnik, SJ., atakayepembua kwa kina kuhusu: Uchapishaji wa kazi za kidini katika muktadha wa utamaduni mamboleo. Utume wa shughuli za kichungaji na za kikanisa zinazoendeshwa na viwanda vya uchapaji vya Kanisa Katoliki. Kutakuwepo na kipindi cha majadiliano ya kina yatakayoratibiwa na wataalam kutoka Ufaransa na Afrika ya Kusini. Wajumbe watapata nafasi pia ya kuangalia: taratibu, kanuni na sheria za shughuli za uchapaji katika maeneo husika mintarafu mwelekeo wa kidigitali kama unavyotolewa na makampuni makubwa kama vile: Google pamoja na Amazon.

Kumbe, kuna umuhimu kwa wajumbe kuangalia pia machapisho yanayotolewa mintarafu ulimwengu wa kidigitali. Dr. Andrea Tornielli, Mhariri Mkuu wa Baraza la Kipapa la Mawasiliano na Dr. Andrea Monda, Mkurugenzi mkuu wa Gazeti la L’Osservatore Romano ni kati ya vigogo kutoka Vatican watakao ratibu majadiliano ya kina wakati wa kongamano hili! Wajumbe wa kongamano hili watapata fursa ya kuhudhuria Ibada ya Misa Takatifu kwenye Kanisa kuu la Mtakatifu Petro mjini Vatican wakati wa Sherehe za Watakatifu Petro na Paulo miamba wa imani, hapo tarehe 29 Juni 2019. Katika Ibada hii, Baba Mtakatifu Francisko atatoa Pallio Takatifu kwa Maaskofu wakuu wapya walioteuliwa katika kipindi cha Mwaka 2018-2019.

Machapisho ya Kikatoliki
22 June 2019, 13:41