Tafuta

Vatican News
Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 27 Juni 2019 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Waziri mkuu Marjan Sarec wa Slovenia. Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi tarehe 27 Juni 2019 amekutana na kuzungumza kwa faragha na Waziri mkuu Marjan Sarec wa Slovenia.  (AFP or licensors)

Papa Francisko akutana na kuzungumza na Waziri Mkuu wa Slovenia! Elimu!

Baba Mtakatifu Francisko pamoja na mgeni wake Waziri mkuu wa Slovenia Bwana Marjan Šarec katika mazungumzo yao ya faragha, wamegusia uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizi mbili na kwamba, umefika wakati wa kuendelea kuboresha na kuimarisha mahusiano haya ya kidiplomasia kwa kujikita katika mambo msingi yenye mafao kwa pande hizi mbili. Elimu imepewa mkazo zaidi.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baba Mtakatifu Francisko, Alhamisi, tarehe 27 Juni 2019 amekutana na kuzungumza na Waziri mkuu wa Slovenia Bwana Marjan Šarec ambaye, baadaye amekutana na kuzungumza pia na Kardinali Pietro Parolin, Katibu mkuu wa Vatican aliyekuwa ameandamana na Askofu mkuu Paul Richard Gallagher, Katibu mkuu wa Mambo ya Nchi za Nje na Ushirikiano wa Kimataifa mjini Vatican. Baba Mtakatifu pamoja na mgeni wake Waziri mkuu wa Slovenia Bwana Marjan Šarec katika mazungumzo yao ya faragha, wamegusia uhusiano mwema uliopo kati ya nchi hizi mbili na kwamba, umefika wakati wa kuendelea kuboresha na kuimarisha mahusiano haya ya kidiplomasia kwa kujikita katika mambo msingi yenye mafao kwa pande hizi mbili.

Viongozi hawa wawili wameridhishwa na mchango wa Kanisa Katoliki katika ustawi, maendeleo na mafao ya wananchi wote wa Slovenia, hususan katika sekta ya elimu. Ni matumaini ya viongozi hawa kwamba, ushirikiano wa nchi hizi mbili utaweza kuboreshwa zaidi kadiri ya wakati. Mwishoni, wamekita mawazo yao kwa kupembua masuala ya kimataifa na kikanda mintarafu mradi wa Umoja wa Ulaya pamoja na changamoto mamboleo zinazoendelea kujitokeza kila kukicha!

Slovenia
27 June 2019, 14:35