Tafuta

Vatican News
Mwenyeheri Edvige Carboni alirutubisha maisha yake kwa tafakari ya Fumbo la Msalaba na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Mwenyeheri Edvige Carboni alirutubisha maisha yake kwa tafakari ya Fumbo la Msalaba na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. 

Mwenyeheri Edvige Carboni: Fumbo la Msalaba & Ekaristi Takatifu

Mwenyeheri Edvige Carboni alipata nguvu na ari ya kusonga mbele kwa kutafakari upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba kiasi kwamba, likawa ni mwanga, matumaini na faraja katika maisha yake. Alikuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu, akataka kujisadaka kutangaza upendo wa Kristo, chanzo cha mateso, kifo na ufufuko wake, ili kumkomboa mwanadamu!

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Kardinali Giovanni Angelo Becciu, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la kuwatangaza waamini kuwa Wenyeheri na Watakatifu, Jumamosi tarehe 15 Juni 2019 kwa niaba ya Baba Mtakatifu Francisko ameongoza Ibada ya Misa Takatifu kwa ajili ya kumtangaza Mtumishi wa Mungu Edvige Carboni kuwa Mwenyeheri. Ibada hii imeadhimishwa huko Pozzomaggiore, Kisiwani Sardegna, Kusini mwa Italia. Ni mwanamke aliyebahatika kuwa na alama za “Madonda Matakatifu ya Yesu” mwilini mwake! Akadhulumiwa na kunyanyasika, kiasi cha kudharauliwa hata na wanafamilia wake. Mwenyeheri Edvige Carboni alizaliwa tarehe 2 Mei 1880 na kubatizwa siku mbili baadaye.

Mwenyeheri Edvige Carboni alizaliwa na kulelewa kwenye familia iliyokita maisha yake kwenye tunu msingi za Kiinjili na kiutu, kiasi cha kutamani kujitoa na kujisadaka kwa ajili ya Mungu na jirani zake. Akiwa na umri wa miaka mitano, akaweka nadhiri ya usafi kamili na akaendelea kujitakatifuza kwa maisha ya sala, tafakari ya Neno la Mungu na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu. Darasani, alipasua sana masomo na nje ya darasa akajifunza kazi za mikono. Baada ya kupokea Komunio ya kwanza, akasadaka maisha yake kwa ajili ya kufundisha Katekesi Parokiani kwake, huku akiongozwa na Padre Luigi Carta. Kunako mwaka 1906 akajiunga na Utawa wa Tatu wa Mtakatifu Francisko na hatimaye, mwaka uliofuatia akaweka nadhiri.

Moyoni mwake, alitamani sana kujiunga na Shirika la Watawa wa Mtakatifu Vincent wa Paulo, lakini kutokana na ukata wa familia hakufanikiwa kutekeleza ndoto yake! Maishani alijaribu kufanya kazi mbali mbali ili kuweza kutoa huduma kwa familia yake, iliyokuwa inaogelea katika umaskini na magonjwa. Lakini bado alibahatika kuwa na neema na baraka ya kujisadaka kwa ajili ya huduma ya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote waliokuwa wanasukumizwa pembezoni mwa jamii. Kuanzia mwaka 1910 hadi mwaka 1925 akajaribiwa sana kutoka katika undani wa maisha yake ya kiroho, akaonekana kuwa na alama za “Madonda Matakatifu ya Yesu”.

Akaendelea kusali na kujiaminisha mbele ya Mungu, kiasi kwamba, alama za “Madonda Matakatifu ya Yesu” mwilini mwake, zikaanza kuonekana na viongozi wa Kanisa, kiasi cha Parokia kusambaratika na hata yeye mwenyewe kuonekana kuwa ni muongo, kiasi hata cha kuundiwa tume ya uchunguzi na matokeo yake, Mwenyeheri Edvige Carbon, akaibuka kidedea na watesi wake wakashikwa na aibu. Akaendelea kusaidiwa katika maisha na utume wake kiasi cha kuvutiwa sana na tasaufi ya Fumbo la Msalaba, ari na mwamko wa kimisionari sanjari na amani! Alisali sana kuombea kukomeshwa kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Akaendelea kujisadaka kwa ajili ya familia, maskini  na waathirika wa Vita Kuu ya Pili ya Dunia.

Mwenyeheri Edvige Carboni akafariki dunia tarehe 17 Februari 1952 akiwa amejikabidhi chini ya ulinzi na huruma ya Kristo Yesu. Kardinali Giovanni Angelo Becciu, katika mahubiri yake, amekazia umuhimu wa waamini kushikamana na kuambatana na Kristo Yesu, ambaye ni Mzabibu wa kweli na Baba yake wa mbinguni ndiye mkulima, ili waweze kuzaa matunda na Mwenyezi Mungu kutukuzwa. Maisha ya watakatifu na wafiadini ni amana na utajiri wa maisha ya kiroho na kitamaduni unaowawezesha kutekeleza wito na utume wao kama Wakristo! Waamini wanahamasishwa kuandika kitabu cha maisha, ili waweze kuwa ni mashuhuda jasiri wa kweli za Kiinjili pamoja na tunu msingi za maisha ya kiutu.

Hii ni changamoto ya kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya huduma ya Injili ya upendo kwa maskini na wale wote wanaosukumizwa pembezoni mwa jamii, ili kuwashuhudia na kuwatangazia Injili ya matumaini! Kardinali Giovanni Angelo Becciu anakaza kusema, Mwenyeheri Edvige Carboni alipata nguvu na ari ya kusonga mbele katika maisha, wito na utume wake kama Mkristo kwa kutafakari upendo unaobubujika kutoka katika Fumbo la Msalaba kiasi kwamba, likawa ni mwanga, matumaini na faraja katika maisha yake. Alikuwa na Ibada ya Kuabudu Ekaristi Takatifu akataka kujisadaka bila ya kujibakiza kwa ajili ya kutangaza na kushuhudia upendo wa Kristo, chanzo cha mateso, kifo na ufufuko wake, ili kumkomboa mwanadamu kutoka katika lindi la dhambi na mauti!

Mwenyeheri Edvige Carboni, alijaliwa kuwa na fadhila ya unyenyekevu na upendo wa dhati, uliorutubishwa kwa sala na tafakari ya Neno la Mungu, kiasi cha kujikabidhi na kujiaminisha mbele ya Mwenyezi Mungu. Alikuwa ni mwanamke mwenye huruma na kwamba, alitumia muda wake mwingi kwa ajili ya kuwakumbuka na kuwaombea watesi wake kama ushuhuda wa imani tendaji uliochota utajiri wake kutoka katika Katekesi makini! Kwa hakika, alikuwa ni mwanamke mnyenyekevu na mwenye nguvu; mkarinu na mvumilivu; mchapakazi na mwenye upendo mkubwa kwa maskini. Kwa ufupi, alikuwa ni mwanamke mwenye upendo na unyenyekevu ulioshuhudiwa katika maisha ya sala. Huu ni mwaliko kwa waamini katika ulimwengu mamboleo, kuiga tunu hizi msingi katika maisha, wito na utume wao, kama amana na utajiri unaobubujika kutoka kwa Mwenyeheri Edvige Carboni, mfuasi mwaminifu wa Kristo Yesu na Kanisa lake!

Kard. Becciu
15 June 2019, 14:19