Tafuta

Vatican News
Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki Limechapisha Hati kuhusu Jinsia Katika Elimu: Kauli mbiu "Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke. Kusikiliza! Kufikiri na Kushauri! Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki Limechapisha Hati kuhusu Jinsia Katika Elimu: Kauli mbiu "Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke. Kusikiliza! Kufikiri na Kushauri!  (ANSA)

Hati Kuhusu Elimu ya Jinsia katika Sekta ya Elimu! Majadiliano!

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki: Hati kuhusu jinsia katika elimu, inaongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke”. Kuelekea njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu. Lengo la hati hii ni kufanya upembuzi yakinifu mintarafu kinzani zinazojitokeza katika sekta ya elimu, hasa kwa kuhusiana na masuala ya mahusiano ya kijamii na tendo la ndoa!.

Na Padre Richard A. Mjigwa, C.PP.S. – Vatican.

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Jumatatu, tarehe 10 Juni 2019, katika Maadhimisho ya Siku kuu ya Bikira Maria Mama wa Kanisa, limechapisha Hati kuhusu jinsia katika elimu, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke”. Kuelekea njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu. Lengo la hati hii ni kufanya upembuzi yakinifu mintarafu kinzani zinazojitokeza katika sekta ya elimu, hasa kwa kuhusiana na masuala ya mahusiano ya kijamii na tendo la ndoa. Melekezo yanayotolewa katika mitaala ya masomo yanakinzana na imani na uwezo mzuri wa kufikiri. Matokeo yake ni mwelekeo tenge wa maisha ya ndoa na familia; ukoloni wa kiitikadi unaotaka kuondoa tofauti kati ya mwanaume na mwanamke.

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linakaza kusema, utume wa elimu unatekelezwa katika mazingira yenye changamoto kubwa, kwa muhtasari tu, zinaweza kuwekwa kwenye kundi la “Nadharia ya Jinsia” inayotoka kuondoa tofauti za kijinsia katika jamii na hivyo kubomoa msingi wa maisha ya ndoa na familia. Nadharia hii imeanza kupenyeza katika mitaala ya masomo na katika masuala ya kisheria inayowapatia watu haki binafsi ya kufanya mahusiano ya ndani kinyume kabisa cha maumbile kati ya mwanaume na mwanamke. Matokeo yake, utambulisho wa mwanadamu unaendelea kubadilika kila kukicha! Changamoto hii haina budi kuvaliwa njuga kwa kuzingatia haki msingi katika elimu zitakazosaidia kuweka uwiano mzuri wa kidugu, kwa kujenga na kuimarisha umoja wa kweli na amani duniani.

Ni katika muktadha huu, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki limekwisha kutoa Hati ya Mwongozo wa Upendo wa Kibinadamu: Maelekezo Kuhusu Elimu ya Jinsia. Mwongozo huu unachota utajiri wake kutoka katika utu wa binadamu, mawasiliano na watu wengine na njia sahihi ya mtu kushuhudia upendo wake. Kumbe, elimu ya ngono ni sehemu muhimu sana ya ukuaji wa mtu mzima: kiroho na kimwili ili hatimaye kuweza kutekeleza dhamana na majukumu yake katika jamii katika hali ya ukomavu. Kuna haja ya kutambua na kuheshimu umoja na tofauti zinazojitokeza kati ya mwanaume na mwanamke na kwamba, wote wanahitajiana na kukamilishana katika utu wao kama binadamu mintarafu mpango wa Mungu katika kazi ya uumbaji. Ni katika muktadha huu, Elimu ya Jinsia haina budi kumgusa mtu mzima: Kiutu, kisaikolojia, kijamii na kiroho.

Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linapenda kutoa mwongozo utakaowasaidia wadau katika sekta ya elimu na malezi kwa vijana, kukabiliana na changamoto hizi katika mwanga wa upendo wa binadamu; kwa kusikiliza kwa makini na baadaye kutoa ushauri, ili utekelezaji wa majukumu yao uwe ni kadiri ya imani inayoshuhudia wito wa binadamu katika kutekeleza mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu lazima litofautishe kuhusu “dhana ya jinsia” inayotaka kuratibu hata jinsi ambavyo watoto wanapaswa kukuzwa na kulelewa. Upande wa pili, ni kutambua “Jinsia” kama tofauti kati ya mwanaume na mwanamke wanaoishi katika tamaduni za watu, sehemu mbali mbali za dunia wanaotambua umoja na tofauti zao, ili hatimaye, kuweza kukamilishana kama binadamu!

Kumbe, majadiliano haya yanasimikwa katika mchakato wa: Kusikiliza, kufikiri na kushauri. Walengwa wakuu wa Hati hii ni wadau wote wanaojisadaka na kujitosa katika elimu na malezi katika shule na taasisi zinazoendeshwa na kusimamiwa na Kanisa Katoliki. Ni mwaliko pia kwa wadau wa elimu wenye mwono wa maisha mintarafu tunu msingi za Kikristo. Hati hii ni nyenzo muhimu sana kwa wazazi, walezi, wanafunzi, viongozi wa shule, wakleri, vyama vya kitume miongoni mwa waamini walei pamoja na watu wote wenye mapenzi mema! Kardinali Giuseppe Versaldi, Mwenyekiti wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki anasema, Hati hii inalenga kujibu kilio na matamanio halali kutoka kwa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuwasaidia wadau wanaotoa kipaumbele cha kwanza kwa Elimu Katoliki kutekeleza vyema dhamana na wajibu wao katika malezi na makuzi ya watoto na vijana wa kizazi kipya.

Tema hii ilichambuliwa kwenye Mkutano mkuu wa Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, Mwezi Februari 2017. Haya ni matokeo ya ushirikiano na mshikamano wa wataalam na mabingwa katika masuala elimu, falsafa na sheria, kwa kuonesha mbinu mkakati wa kuwasaidia wadau katika sekta ya elimu kwa vijana wa kizazi kipya! Lengo ni kuepuka mipasuko na kinzani ambazo zingeweza kujitokeza katika utekelezaji wa “dhana ya jinsia”. Hati kuhusu jinsia katika elimu, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke”. Kuelekea njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu imechapishwa!

Kardinali Giuseppe Versaldi anasema, Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki linawaalika wadau mbali mbali kukabiliana na suala ya jinsia kwa kutumia mbinu mkakati wa majadiliano yanayofumbatwa katika utamaduni wa kusikiliza, kufikiri na kushauri mintarafu mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu. Mkazo ni utu, heshima na haki msingi za binadamu bila kusahau utu na tunu msingi za maisha ya wanawake. Kimsingi, wanawake wanapaswa kuheshimiwa na kuthaminiwa katika utu wao, kwani wao wana mchango mkubwa katika medani mbali mbali za maisha ya kijamii! Wanawake wengi wanaendelea kujisadaka kutoa huduma inayotukuka katika ustawi na maendeleo ya familia zao, na wengi wao wanajisadaka bila ya kujibakiza katika huduma kwenye sekta ya elimu, huduma kwa wazee na watoto wanaoishi katika mazingira magumu na hatarishi, bila kusahau mchango wao katika maisha na utume wa Kanisa!

Kwa hakika, wanawake ni moto wa kuotea mbali katika mchakato wa uinjilishaji. Hati hii ni sehemu ya mwendelezo wa Waraka uliotolewa na Baraza la Kipapa la Elimu Katoliki, tarehe 1 Novemba 1984 kuhusu: “Educational Guidance in Human Love: Outlines for sex education”. Hati hii mpya inakita hoja zake katika mwono wa Kikristo mintarafu utu wa mwanadamu! Hati hii wanakabidhiwa Marais wa Mabaraza ya Maaskofu Katoliki sehemu mbali mbali za dunia, ili kuhakikisha kwamba, hati hii inawafikia wadau wote wa elimu wanaoendelea kutoa kipaumbele cha kwanza kwa Elimu Katoliki, wakiwa wanaongozwa na mwono wa Kikristo kuhusu maisha.

Kwa upande wake,  Profesa Roberto Zappalà, Mkurugenzi wa Taasisi ya Elimu ya Gonzaga kutoka Milano, Italia, anasema, Hati kuhusu jinsia katika elimu, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke”. Kuelekea njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu ni mchango muhimu sana unaotolewa kwa wadau katika sekta ya elimu kwa ajili ya watoto na vijana wa kizazi kipya. Kipaumbele cha pekee ni kuhusu “dhana ya jinsia, tendo la ndoa kama changamoto pevu katika sekta ya elimu; mambo yanayokinzana na uelewa wa jinsia na tendo la ndoa kadiri ya mpango wa Mungu katika maisha ya mwanadamu.

Mtakatifu Paulo anawaonya Wakristo wa Efeso akiwataka wasiwe tena watoto wachanga, wakitupwatupwa huku na huku na kuchukuliwa na kila upepo wa mafundisho kwa hila za watu, kwa ujanja, kwa kufuata njia zao za udanganyifu. (Ef. 4:14). Baba Mtakatifu Mstaafu Benedikto wa XVI aliwahi kusema, mwelekeo huu ni kumong’onyoka kwa utu na heshima ya binadamu, kunakowafanya watu kusahau kwamba, mtu mzima ameumbwa: mwili na roho na wala si mkusanyiko wa viungo mbali mbali vinavyoweza kutenganishwa kwa ajili ya kuridhisha matakwa ya mtu binafsi. Ni katika muktadha huu, Mama Kanisa anapenda kuwaalika wadau katika sekta ya elimu mintarafu suala ya “dhana ya jinsia” katika elimu kujielekeza zaidi katika utamaduni wa kusikiliza, kufikiri na kutoa ushauri.

Utamaduni wa kusikiliza unawataka wadau kuangalia mahali ambapo wanakubaliana na kinzani zinazojitokeza, ili kuweza kushirikishana amana na utajiri uliomo. Huu ni mwaliko wa kusimama kidete: kupambana na nyanyaso na ubaguzi wa kijinsia. Kufikiri: Dhana ya jinsia imepembuliwa kwa kina na mapana; kwa kubainisha ukoloni wa kiitikadi, unaotaka kufutilia mbali tofauti za kijinsia kati ya mwanaume na mwanamke; kwa kutoa mwelekeo potofu unaokita mizizi yake katika ubinafsi, uchoyo na hali ya mtu kukata kujikweza zaidi, kielelezo makini cha mwelekeo wa jinsi ya kufikiri na kutenda katika ulimwengu mamboleo. Mtazamo huu, kwa haraka haraka unaweza kuonekana kuwa kama ndio uhuru wenyewe unatoa fursa ya kila mtu kufikiri na kuamua kile ambacho anadhani kwamba, ni chema.

Hapa watu wanasahau kwamba, kuna kanuni maadili na utu wema unaowaongoza watu jinsi ya kufikiri na kutenda kadiri ya mpango wa Mungu. Profesa Roberto Zappalà anaendelea kufafanua kwamba: Kushauri ni sehemu ya mang’amuzi ya ukweli kuhusu mtu, maana na umuhimu wa tendo la ndoa linalokidhi na kusadifu utu na heshima ya binadamu mintarafu uelewa wa ekolojia ya binadamu inayotambua na kuthamini utu wa binadamu aliyeumbwa kwa sura na mfano wa Mungu. Utu wa binadamu hauna budi kuheshimiwa na kamwe hauwezi kuwa ni kichokoo kinachosiginwa kadiri ya vionjo vya watu! Wanaume na wanawale, wanahimizwa kujifunza kwa dhati kabisa kuhusu ukweli wa miili yao, ili hatimaye, kujenga utamaduni wa kukutana, ili kukamilishana na kutajirishana kadiri ya mpango wa Mungu.

Kimsingi, huu ndio mwono wa Kikristo kuhusu binadamu, unaotambua na kuthamini umuhimu wa tendo la ndoa kama sehemu ya utekelezaji wa kazi ya uumbaji. Ni mwono unaopambana na vitendo vya kikatili, ubaguzi na nyanyaso za kijinsia. Mwono wa Kikristo unaheshimu usawa wa watu pamoja na kuthamini tofauti zao kama amana na utajiri mkubwa unaopaswa kukuzwa na kudumishwa! Profesa Roberto Zappalà anaendelea kufafanua kwa kusema, Hati kuhusu jinsia katika elimu, inayoongozwa na kauli mbiu “Mwenyezi Mungu alimuumba mwanaume na mwanamke”. Kuelekea njia ya majadiliano kuhusu suala la jinsia katika elimu ni sehemu ya mchakato wa ujenzi wa ujenzi wa jamii inayojikita katika amani na utulivu; kwa kuheshimu utu wa binadamu na haki zake msingi bila kusahau uhuru wake.

Mama Kanisa anapenda kujikita katika mchakato wa majadiliano na wadau katika sekta ya elimu, jamii na siasa pamoja na watu wote wenye mapenzi mema, wanaothamini tunu msingi za maisha na utu wa binadamu. Mama Kanisa anatambua na kuthamini mchango unaoweza kutolewa na kila mdau katika sekta ya elimu, lakini pia ni muhimu kwamba, Kanisa nalo liweze kupata jukwaa la kutolea maoni yake na ushauri wake bila kuangukia katika hali ya kutopea kwa imani. Mwishoni, Profesa Roberto Zappalà anakumbusha kwamba, Kanisa ni mtaalam wa utu na heshima ya binadamu. Kanisa linataka kuchangia amana na utajiri wake kuhusu mwono wa mtu na binadamu katika ujumla wake. Anatambua fika kwamba, ni kwa njia ya majadiliano katika ukweli na uwazi; kwa kushindana kwa nguvu ya hoja bila wasi wasi wala makunyanzi wala misimamo mikali ya kiitikadi, Kanisa linaweza kuchangia uelewa makini wa binadamu pamoja na tendo ya ndoa kadiri ya mpango wa Mungu!

Jinsia Katika Elimu

 

10 June 2019, 16:55